Prime
Prince Dube ana mambo mawili Yanga
Mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube alionekana kama mtu anayejilaani kwa kushindwa kutumia vizuri nafasi mbili alizopata katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi Jumamlosi iliyopita.
Nafasi ya kwanza aliipata akiwa karibu mita 18 kutoka golini. Alituliza vizuri mpira na kutaka kupiga shuti kushoto kabisa kwa kipa wa Silver, lakini hesabu zake zilizidi na hivyo mpira kwenda nje kidogo ya lango.
Nafasi ya pili aliipata akiwa ndani ya miguu 12 wakati Pacome Zouzoua alipompa pasi ya kimo cha paka, lakini alipojaribu kutuliza mpira ukatua mbali na hivyo kuokolewa na beki wa “washambuliaji hao wa shaba”.
Hayo ni matukio mawili yaliyosababisha wachambuzi wajumuishe kiwango chake chote kwenye mechi hiyo na kujumlisha na mechi nyingine zote kiasi cha kuhitimisha kuwa mshambuliaji huyo wa Zimbabwe hastahili kuchezea Yanga.
Na kwa mchezaji anayejua wajibu wake huonekana dhahiri. Dube hakutoka uwanjani akiwa anacheka, bali alionyesha huzuni kubwa kuanzia pale benchi hadi mchezo ulipomalizika. Kwa kuangalia picha hizo za marudio unaona ni kwa kiasi gani Dube alikuwa anajutia nafasi alizopata na ni kwa kiasi gani anajua alitakiwa afanye nini. Na zaidi ya yote, akaomba radhi kwa kilichotokea.
Hayo pekee yanatosha kuonyesha kuwa Dube ni mchezaji mwenye weledi na anayejua kuwajibika pale inapobidi. Au kwa maneno mengine haoni kosakosa hizo kuwa sehemu ya mchezo, bali ni yeye kutofanya mambo ya msingi ambayo yangeweza kumsaidia kufanya vizuri pale ilipobidi.
Pamoja na kuwa mshambuliaji hatari, Dube hajawahi kujijengea sifa nchini kama mmoja wa wafungaji hodari na hajawahi kuwa katika kinyang’anyiro cha mfungaji bora wa msimu. Lakini amepata sifa kwa kuwa mwiba mkali kwa klabu kubwa za Yanga na Simba, akifunga mabao muhimu katika mazingira magumu wakati akiichezea Azam FC.
Mabao hayo dhidi ya Yanga na Simba ndiyo yanawafanya wengi wategemee Dube kufunga katika kla mechi au kutumia kila nafasi inayopatikana, lakini wakifumbia macho washambuliaji ambao wameshindwa kufunga zaidi ya mabao manne ndani ya misimi mitatu.
Kwa maana nyingine, sifa ya Dube si ufungaji mabao, ingawa si kisingizio cha kukosa mabao yale Jumamosi. Sifa kuu ya Dube ni ushambuliaji.
Niliwahi kuandika kwenye safu hii kuwa Dube anajua mtu wa tatu anayekimbia wakati anapopewa pasi. Hiyo ni moja ya sifa kuu za washambuliaji. Kwamba kila wakati anapopata mpira, jicho la kwanza ni goli na la pili ni wapi pa kupeleka mpira ili bao afunge mwingine.
Dube anashiriki katika kuiwezesha timu kufunga mabao mengi si kwa kutoa pasi ya mwisho, bali katika kuwezesha wenzake watengeneze bao au wafunge.
Mikimbio yake anapokuwa hana mpira huwazuzua mabeki wengi na ndiyo ilimuwezesha Pacome kufunga bao la pili aliposababisha beki wa Silver ashindwe kujua amfuate nani.
Ni mchezaji anayejua kuchezesha wenzake wakati timu inaposhambulia au kurahisisha kazi kwa wenzake ama kwa kushiriki moja kwa moja ama kwa kushiriki bila ya kugusa mpira. Washambuliaji wa aina hii ni nadra sana kupatikana.
Na ndio maana amekuwa chaguo la kwanza kwa makocha wengi isipokuwa pale tu wanapotaka kumpumzisha.
Na imekuwa hivyo tangu akiwa Azam ambako majeraha yalimfanya awe anakaa nje nyakati fulani.
Cha ajabu, Dube amekuwa begi la mazoezi ya masumbwi kwa wachambuzi. Kila anayetaka kuponda, hutumia dakika chache kuangalia kosakosa mbili tatu za Dube na kutoa uchambuzi wake kuwa “pale hakuna mshambuliaji” . Hakuna anayezungumzia umuhimu wake kama mshambuliaji ama rekodi zake za nyuma, bali matukio mawili au matatu yanatumika kufanya majumuisho. Hii si sawa!
Hivi udhaifu wa Dube ni baada ya kujiunga na Yanga? Huko Azam alikuwa hana kosakosa? Hata msemaji wa Azam alishawahi kusema kuwa kosakosa ni moja ya kasoro za Dube. Lakini kasoro moja haimuondolei ubora mwingine.
Kuna washambuliaji wanakosa mabao ya wazi kumzidi Dube na tena kwenye mechi kubwa za maamuzi kama ile ya Ngao ya Hisani kati ya Simba na Yanga ambayo washambuliaji wawili wa Simba walishindwa kufunga wakiwa wamebakia na kipa pekee, lakini uchambuzi haukuwa wa majumuisho kuwa hawafai.
Ni muhimu sana kwa wachambuzi kutenda haki na kuepuka kufanya majumuisho yanayotia shaka kiasi cha kusababisha msemaji wa Yanga kuwatuhumu kuwa wanalipwa fedha ili waponde wachezaji wao.
Ni vizuri unapoonyesha kasoro za mchezaji, uonyeshe na ubora wake na kuweka mzani kipi ni kikubwa kati ya kasoro na ubora na ni kwa sababu gani anapewa nafasi zaidi kuliko wengine, tena waliotoka mataifa makubwa kisoka.
Bila kutenda haki katika kuchambua inaonekana dhahidi kuwa kasoro za Dube zinakuzwa. Pole sana Dube. Cha muhimu umetambua makossa na kuyajutia, lakini ukubwa wa makossa hayo haujafikia kiwango kinachoelezwa.