Prime
Kama Folz hafai, aliyemwajiri ndiye aliyekosea
WAKATI Kocha Miguel Gamondi alipoondolewa Yanga, niliandika maoni yangu, uongozi ulifanya kosa kubwa kuachana na kocha wakati ikikaribia kuanza hatua muhimu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gamondi alikuwa ameshajitengenezea ufalme wake kwenye timu, akijihusisha na wachezaji katika mambo mengi ya kijamii hivyo kutengeneza uhusiano mzuri uliokuwa unarahisisha kazi yake ya kufundisha.
Alishajenga kikosi imara kilichokuwa kipana kutokana na kutumia asimilia kubwa ya wachezaji isipokuwa wachache kama Kibwana Shomari, ambaye alipata shida kurudi kikosi cha kwanza hadi Muargentina huyo alipoondoka.
Uongozi ulimtimua Gamondi baada ya Yanga kupoteza mechi mbili za Ligi Kuu Bara, ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja baada ya Ibrahim Bacca kuonyeshwa kadi nyekundu mapema, ilishindwa kwa bao 1-0 na Azam FC katika mechi ambayo wanajangwani walitawala sehemu kubwa ya mchezo licha ya kuwa pungufu.
Balaa jingine likaja ilipokutana na Tabora United. Yanga ikiwakosa mabeki wanne wa kikosi cha kwanza, Bacca, Chadrack Boka, Dikson Job na Yao Kouasi, iliingia uwanjani ikimtumia Aziz Andambwile kama beki wa kati. Lakini kiungo huyo akaumia dakika ya nane na hivyo Khalid Aucho kulazimika kurudi kucheza beki wa kati pamoja na Mwamnyeto.
Yanga ikafungwa mabao 3-1 katika siku ambayo nadhani wachezaji walikuwa wakiombea mchezo uishe.
Kipigo hicho kikawa ndiyo sababu ya kuachana na Gamondi. Zikatafutwa sababu kibao, ikiwa ni pamoja na kumsingizia kuendekeza starehe pamoja na wachezaji na nidhamu ilipotea kikosini.
Lakini, kama kawaida, taarifa ya kuachana naye haikuwa na visingizio hivyo. Ikampata Saed Ramovic ambaye alitanguliziwa sifa nyingi zilizopenyezwa na uongozi kufuta kivuli cha Gamondi. Na kwa kuwa Ramovic aliichukua timu wiki moja kabla ya hatua ya makundi kuanza, hakuweza kufanya lolote kubwa na timu ikashindwa kuvuka kwenda robo fainali kama alivyofanya Gamondi msimu uliotangulia.
Ramovic hakuwa na sababu tena ya kuendelea kukaa nchini. Ikadaiwa amepata mkataba mnono Arabuni na akaondoka zake na kumwachia mlango David Fadlu ambaye aliondoka mwishoni mwa msimu baada ya kupata dau zuri.
Ramon Fols alikuja kipindi kizuri kwa kocha yeyote. Akikuja wakati timu ikijiandaa kwa msimu, lakini tatizo kwake likawa ni kukosa wachezaji muhimu ambao walikuwa na timu zao za taifa zilizoshiriki fainali za Mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
Alianza vizuri mechi za matayarisho ya msimu, lakini sare dhidi ya Mbeya City ikarejesha shinikizo kwa kocha. Aina tofauti ya mchezo ikilinganishwa na za watangulizi wake, iliudhi mashabiki ambao wanataka waone pasi nyingi zikipigwa wakati wa kwenda goli la mpinzani tofauti na Fols.
Pamoja na kushinda mechi za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, bado mashabiki wakaona hawaridhishwi na Mfaransa huyo na hicho kipigo cha Jumamosi cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Silver Strikers ndiyo kimeongeza petroli kwenye moto ulioanza kufifia.
Pamoja na kufungwa bao 1-0 ugenini, Yanga ilitawala sehemu kubwa ya mchezo na makosa ya kiungo wa nyuma kuzubaa na kutotimiza majukumu yake ndiyo yaliyosababisha mtoaji wa pasi muhimu kupata mpira akiwa peke yake na kumpa mtoaji wa pasi ya mwisho.
Yanga imeachana na Fols wakati ikijiandaa kwa mechi ya marudiano itakayofanyika wiki hii. Itakuwa ngumu kwa kocha mpya kuweza kuingiza falsafa zake vichwani mwa wachezaji ndani ya siku chache ili wawe na uwezo kuiondoa Strikers ya Malawi.
Na kama kocha mpya atakuwa na falsafa tofauti, hali ndio itakuwa ngumu zaidi kwa Yanga na inaweza ikaishia hatua mbaya ambayo haijawahi kutokeza katika miaka ya karibuni. Miaka mitatu iliyopita Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho. Mwaka uliofuata nusura iingie nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kama si mauzauza ya refa.
Mwaka jana ikashindwa hata kufika robo fainali na kuna hatari mwaka huu ikaishia raundi za awali, kitu kinachoonyesha timu inazidi kuporomoka.
Viongozi wamefanya maamuzi sahihi kwa muda mrefu na timu imekuwa ikifanya vizuri, lakini kwa kocha naona sasa wameanza kukosea, hasa kuishi na kocha na pia kuwa waoga kunapotokea shinikizo. Na inawezekana kabisa kuna viongozi ambao huanzisha taarifa zinazoonyesha kuwa kocha hatakiwi ili kumuwekea shinikizo aondoka, lakini taarifa kama hizo humyumbisha kocha na kudhoofisha timu.
Kutimuatimua makocha hakuwezi kujenga timu imara bali kunajenga timu isiyoaminika na inayoendeshwa kwa woga. Kusimama na kocha ni kusimamia maamuzi ya kumuajiri, kutimuatimua kocha ni kukwepa lawama za maamuzi mabovu.
Uamuzi wa kumtimua Fols ni wa kisiasa zaidi kwa ajili ya kuridhisha mashabiki na wanachama. Kama kweli Fols hafai, basi kosa lilifanyika wakati wa kumuajiri. Aliyemtafuta ndiye aliyekosea. Umakini unatakiwa katika kuajiri kocha lakini kikubwa zaidi ni muda wa kuajiri.