Prime
Kamati ya Saa 72 iangalie vizuri ratiba, kisha ikumbuke Uchaguzi Mkuu
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amekuwa ni mhamasishaji mkubwa wa wananchi kutoka Jimbo la Catalonia kupigania uhuru wao kutoka Hispania.
Amekuwa akijitokeza kwenye maandamano ya kudai kura ya maoni ili kujua kama wananchi wa Hispania wako tayari kuiacha Catalonia kuwa na uhuru kamili, na amekuwa akiwahamasisha Wakatalunya kujitokeza kupiga kura iwapo mchakato huo utaendeshwa.
Alishiriki katika kura ya maoni isiyokuwa rasmi 2014 na kupiga kura ya kutaka Catalonia iwe huru na baadaye kushiriki kura nyingine kubwa zaidi iliyoandaliwa 2017 na ambayo ilitawaliwa na vurugu zilizosababisha wananchi wengi kujeruhiwa.
Na alishiriki katika kura zote akitokea miji mingine aliyokuwa akifanyia kazi. Alishiriki kura ya maoni yam waka 2014 akitokea jijini Munich ambako alikuwa kocha mkuu wa vigogo wa Ujerumani, Bayern Munich.
Mwaka 2017 alisafiri kutoka jijini Manchester ambako ni kocha mkuu wa City kwenda Barcelona kupiga kura ya kutaka jimbo hilo liwe huru. Kwake, kupiga kura ni haki ya msingi ya kidemokrasia kwa kila raia, hivyo anaitumia ipasavyo kushiriki uamuzi unaohusu nchi na maisha yake.
Ndivyo Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi maarufu kama Kamati ya Saa 72 inavyotakiwa ielewe masuala ya haki za msingi za wananchi wake na kuonyesha kwa vitendo kuwa inazijali.
Serikali ilishatangaza kuwa Oktoba 29, 2025 nchi itakuwa na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani na hivyo wananchi wote watatakiwa kuwa sehemu walizojiandikisha ili waweze kutumia haki hiyo ya kikatiba.
Hata vyuo vya elimu ya juu kwa sasa vimefungwa hadi Novemba ili kuwawezesha wanafunzi kushiriki katika kuchagua viongozi wa kitaifa, kijimbo na katika kata zao.
Haki hii inapatikana mara moja katika kipindi cha miaka mitano, labda itokee dharura ya mshindi kufariki dunia au kujivua cheo.
Na hii si siku ya mapumziko ya kitaifa, bali ni siku maalumu kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kushiriki mchakato huo na ndio maana wafanyakazi hawataenda kazini siku hiyo ili watumie fursa hiyo kupiga kura.
Viko vituo vyenye wananchi wachache ambavyo kazi ya kupiga kura inaweza kuisha mapema hata kabla ya Magharibi, lakini zipo sehemu ambazo wapigakura ni wengi hivyo haitawezekana kwa wakazi wa maeneo hayo kumaliza kazi hiyo mapema.
Na kwa maana hiyo, klabu za soka zinaundwa na wachezaji kutoka maeneo tofauti na ambao katika kipindi cha miaka mitano wanaweza kuwa wamebadili klabu mara mbili au tatu na hivyo haitawezekana kwao kushiriki kupiga kura katika klabu walizopo sasa kama haziko eneo moja na sehemu walikojiandikisha.
Na hata linghekuwa ni eneo moja, bado klabu lisingewaruhusu waondoke asubuhi kwenda vituo tofauti katika eneo hilo kwa ajili ya kupiga kura na kurudi kambini mchana kusubiri mechi.
Maana yake ni kwamba kuanzia Jumapili ya Oktoba 26, ligi zote zilitakiwa zisimame hadi Oktoba 31 kuwawezesha wachezaji kurudi maeneo walikojiandikisha kwa ajili ya kutumia haki hiyo ya kikatiba. Hata kama mwamko huo wa kutumia haki zao hawana, ni muhimu kuonyesha kuheshimu zao.
Hii ingekuwa ni wiki ya uchaguzi ambayo wachezaji wote wa ndani wangerudi makwao hadi watumie haki hiyo, kama ambavyo Guardiola hufanya pale kunapotokea kuna uchaguzi au upigaji kura za maoni kuhusu uamuzi mkubwa wa nchi.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatakiwa lihimize waendeshaji wake kuwa wanapaswa kujali mambo ya msingi ya kitaifa na hivyo kuwa na sera ambayo inataka shughuli zisizo za kila siku kama semina, mafunzo na majaribio hazifanyiki wakati taifa linafanya uamuzi mkubwa kuhusu hatima yake.
Kitendo cha kupanga mechi siku ya Oktoba 29 kinaonyesha ni kiasi gani kamati hiyo inayosimamia na kuendesha ligi haina mtazamo mpana kuhusu masuala ya uchaguzi.
Nimeona moja ya mechi zitakazochezwa siku hiyo ni Yanga DC na Mtibwa Sugar jijini Dar es salaam. Kumekuwa na majibu mepesi yasiyotumia ubongo kufikiri. Kuna mtu anadai eti “kura tutapiga asubuhi na jioni tunaende uwanjani”.
Huyu amejifikiria kama shabiki, hajawaza kama wachezaji nao watatakiwa washiriki kupiga kura na wametokea sehemu tofauti hapa Tanzania.
Sasa sijui Clement Mzize kama amejiandikisha, atarudi Iringa kupiga kura asubuhi halafu awahi mechi mchana? Sijui wachezaji wa Kagera wote wamejiandikisha kupiga kura Dar es salaam? Na kama wamejiandikisha Dar, viongozi watakuwa tayari kuwaruhusu asubuhi kwenda kupiga kura halafu warudi mchana wakiwa wamebeba tuhuma kibao kwamba walikuwa kupokea mzigo?
Tunahitaji kuoanisha masuala ya kitaifa na michezo ili kulinda haki za wapenzi wa michezo na wanamichezo wenyewe. Inahitajika Wiki ya Uchaguzi ili kuupa thamani uchaguzi. Hayo mengine kuhusu uchaguzi hayawezi kuzuia mpira wa miguu kuutambua umuhimu wa uchaguzi.