Paul Pogba ndani ya mbio za Ngamia
Muktasari:
- Utajiri wake wa mamilioni ya dola unatokana na mishahara mikubwa kutoka katika klabu kubwa kama Manchester United na Juventus, mikataba mikubwa ya udhamini wa kimataifa ikiwemo ushirikiano wa muda mrefu na Adidas pamoja na mafanikio yake ya kimataifa akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa.
RIYADH, SAUDI ARABIA: PAUL Pogba kwa sasa hana timu baada ya kutemwa na Monaco ya Ufaransa kutokana na tatizo la majeraha linalomkabili kwa muda mrefu.
Hata hivyo, nyota huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa takribani Dola 125 milioni, ana biashara na shughuli nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kumfanya aishi maisha mazuri.
Utajiri wake wa mamilioni ya dola unatokana na mishahara mikubwa kutoka katika klabu kubwa kama Manchester United na Juventus, mikataba mikubwa ya udhamini wa kimataifa ikiwemo ushirikiano wa muda mrefu na Adidas pamoja na mafanikio yake ya kimataifa akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa.
Kinachomfanya atembee kifua mbele zaidi kwa sasa ni kwamba anamiliki sehemu ya klabu ya mbio za ngamia ya Al Haboob nchini Saudi Arabia, huku akilenga kununua ngamia mwenye thamani ya Dola 5 milioni kwa ajili ya timu yake.
Nyota huyo amepata mchezo mpya nje ya soka baada ya kushindwa kutamba katika miaka ya karibuni kwenye soka.
MBIO ZA NGAMIA ZIKOJE?
Mbio za ngamia ni shughuli ya michezo inayotawaliwa na familia za kifalme na watu wa tabaka la juu katika eneo la Baraza la Ushirikiano la Ghuba ikiwemo Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu, ambako matukio hayo huchukua wiki kadhaa yakihusisha zaidi ya washiriki 85 na zawadi zinazofikia Pauni 4 milioni, huku siku ya mchezo ikifananishwa na fainali unazozijua katika soka.
Mchezo huo ulianza kujipatia umaarufu zaidi ya miaka 1,000 iliyopita wakati makabila yaliyokuwa yakigombana katika Rasi ya Arabia hayakusuluhisha migogoro yao kupitia mashindano ya kupigana kwa mikuki, badala yake mbio za ngamia, huku washindi wakiwapatia wamiliki wao eneo muhimu la fukwe ambalo lilikuwa muhimu kwa biashara na maisha.
Mwaka jana ulikuja na mshindani mpya, timu ya Al Haboob ambayo inalenga kuonyesha kwamba mchezo huo pia unaweza kuwa biashara yenye faida. Ni wazo lililoanzishwa na wanaume wawili kutoka Saudi Arabia, Omar Almaeena na Safwan Modir, pamoja na mwekezaji asiyetarajiwa, Pogba.
Mchezaji anamiliki sehemu ndogo ya Al Haboob ambayo wenzao wanaomiliki ngamia wameielezea kuwa ni sehemu “nzuri” na ameeleza nia yake ya kuwa na zizi lenye ngamia nyota mwenye thamani ya Dola 5 milioni.
“Ushiriki wa Paul unalenga kukutanisha kati ya michezo na watu mashuhuri duniani,” Almaeena anaiambia City AM.
“Hayupo tu kama balozi na kwa ajili ya masoko, bali amewekeza kwenye timu kama mwanahisa na anaelewa thamani ya jambo hili. Anaelewa namna tunavyoweza kukuza hili na kutumia jukwaa lake.”
Mchezo wenyewe wa mbio za ngami umebadilika kutoka katika asili yake ya kikabila, ambapo kwa sasa unaweza kugharimu kiasi cha Pauni 40,000 tu kununua ngamia mwenye ushindani, huku fedha zikipatikana baada ya kuvutia macho ya mazizi ya kifalme kwenye matukio mbalimbali nchini Saudi Arabia na Qatar.
Almaeena na Modir wanaeleza kwamba mara kwa mara watu wa tabaka la juu wamekuwa wakinunua washindi 10 bora wa mbio kubwa, kwa sehemu ili kuimarisha mazizi yao na pia kudhoofisha washindani wao.
Kwa wamiliki wa sasa, hii inawakilisha faida kubwa mara mbili, mara nyingi inayokaribia Pauni 1 milioni ikiwa watafanikiwa kupata Pauni 500,000 kwa kushinda mbio kubwa na kiasi kama hicho kwa kuuza ngamia wao kwa mzabuni anayetoa bei ya juu zaidi.
Modir anaongeza: “Tutaendelea kuwahamasisha watu zaidi kuingia katika mbio hizi kwa kutumia mfumo wa biashara tunaoufanya.”
Mtazamo wao unalenga upanuzi wa soko na wanataka kukabiliana na wakimbiza ngamia walioimarika ambao wana miaka mingi ya kihistoria katika mchezo huo.
Kuhusu mvuto wa Pogba, Modir anasema: “Sasa una kundi zima la mashabiki wa soka ambao wamepata fursa ya kufahamu mbio za ngamia.”
Wamiliki hao wa Al Haboob wanadai kwamba kampuni kubwa na benki maarufu za Ghuba sasa zinaunga mkono mbio hizo kutokana na Pogba kuziongezea hadhi.
Almaeena na Modir wakiwa na Pogba wana mipango mikubwa, huku wakiamini kwamba, “kuna uwezekano kwamba ndani ya miezi 14 ijayo tutakuwa na mbio mahali fulani barani Ulaya.” Mbio hizo zinaweza kwenda sambamba na mwekezaji mwingine mashuhuri wa michezo kuiunga mkono Al Haboob.
“Tunatumaini tutamvutia Shaquille O’Neal kuwekeza,” Modir anasema na kuongeza: “Hilo ni jambo tunalolitamani: Shaq kwenye uwanja wa mbio.” O'Neal ni mmoja wa mastaa wa kikapu duniani walioacha rekodi nyingi bora katika mchezo huo.