Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PAGUMU! Umiliki mpira unavyopoteza dhamana timu kushinda EPL

GUARDIOLA Pict

Muktasari:

  • Mara nyingi, unapocheki takwimu baada ya mchezo na kuona timu moja imemiliki mpira kwa kiwango kikubwa lakini ikapoteza, unashangaa. Kwa kawaida, unaamini timu bora zinapaswa kumiliki mpira zaidi kwa sababu zinapata nafasi nyingi za kutengeneza mashambulizi na kufunga mabao.

LONDON, ENGLAND: KUNA jambo umegundua? Timu zinazomiliki mpira kwa kiwango kidogo zimeanza kushinda mechi nyingi zaidi katika Ligi Kuu England (EPL) kuliko zile zinazomiliki kwa muda mrefu. Je, haya ni mabadiliko ya kawaida ya matokeo au kuna jambo la msingi linaloonekana katika takwimu?

Mara nyingi, unapocheki takwimu baada ya mchezo na kuona timu moja imemiliki mpira kwa kiwango kikubwa lakini ikapoteza, unashangaa. Kwa kawaida, unaamini timu bora zinapaswa kumiliki mpira zaidi kwa sababu zinapata nafasi nyingi za kutengeneza mashambulizi na kufunga mabao.

Na kwa muda mrefu, matokeo katika Ligi Kuu England yaliunga mkono mtazamo huo. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, mwelekeo umeanza kubadilika na kumiliki mpira kwa kiwango kidogo kuliko mpinzani kunaweza kuwa njia yenye nafasi kubwa zaidi ya kushinda.

Opta imekuwa ikikusanya takwimu za umiliki wa mpira katika ligi hiyo tangu msimu wa 2005/06. Katika msimu huo, timu zilizomiliki mpira kwa zaidi ya asilimia 50 zilishinda mechi 149, huku zile zilizomiliki chini ya asilimia 50 zikishinda mechi 152.

GUARD 04

Hata kwa kuzingatia mechi ambazo tofauti ya umiliki wa mpira ilikuwa kubwa zaidi, matokeo yalikuwa karibu sawa. Timu zilizomiliki mpira kwa zaidi ya asilimia 55 zilishinda mechi 80, dhidi ya ushindi mara 77 wa timu zilizomiliki chini ya asilimia 45.

Katika misimu 19 iliyofuata, timu zilizomiliki mpira zaidi zilishinda mechi nyingi zaidi kuliko zile zilizomiliki kidogo. Hata hivyo, mwelekeo huo ulianza kubadilika katika msimu wa 2024/25, ambapo idadi ya ushindi kwa timu za makundi hayo mawili ilikuwa karibu sawa.

Msimu wa 2025/26 ulikuwa na mabadiliko zaidi. Timu zilizomiliki mpira kwa zaidi ya asilimia 50 zilishinda mechi 137, huku zile zilizomiliki chini ya asilimia 50 zikishinda mechi 139. Kwa kuangalia mechi ambazo tofauti ya umiliki ilikuwa kubwa, timu zilizomiliki mpira kwa zaidi ya asilimia 55 zilishinda mechi 83, huku zilizomiliki chini ya asilimia 45 zikishinda mechi 89. Hii ilikuwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2005/06 kwa kundi la pili kushinda mechi nyingi zaidi.

 Katika msimu wa 2026/27, baada ya mechi 34 zilizokuwa zimechezwa, timu zilizomiliki mpira kwa zaidi na chini ya asilimia 50 zilikuwa na ushindi 17 kila upande. Hata hivyo, ushindi 15 wa timu zilizomiliki mpira kwa kiwango kidogo ulikuwa kwa zile zilizokuwa na umiliki wa chini ya asilimia 45. Je, hali hii inaashiria mabadiliko ya mbinu za soka England au ni matokeo ya kawaida yanayotokana na mazingira ya mchezo?

Inawezekana baadhi ya takwimu zimeathiriwa na timu kupata bao la kuongoza na kisha kupunguza umiliki wa mpira ili kulinda ushindi. Hata hivyo, hali hiyo ilikuwepo pia katika misimu iliyopita, wakati takwimu zilikuwa tofauti.


GUARD 01

ATHARI ZA PEP GUARDIOLA

Haiwezekani kuzungumzia mwenendo wa umiliki wa mpira katika Ligi Kuu England bila kutaja athari za Pep Guardiola. Ingawa timu zilikuwa zikimiliki mpira kabla ya kuwasili kwake, kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich aliendeleza zaidi mtindo huo Manchester City.

Kati ya msimu wa 2005/06 na msimu wake wa kwanza Man City 2016/17, ni mara nne tu ambapo timu ilifikia wastani wa umiliki wa mpira wa angalau asilimia 60 katika msimu mzima. Timu hizo zilikuwa Chelsea, iliyofikia asilimia 60.2 mwaka 2008/09; Arsenal, iliyofikia asilimia 60 msimu 2010/11 na asilimia 60.1 ule wa 2011/12; pamoja na Manchester United, iliyofikia asilimia 61.4 msimu wa 2014/15.

Katika kila mmoja wa misimu minane ya kwanza baada ya Guardiola kutua Man City, kulikuwa na angalau timu tatu zilizofikia wastani huo.

Katika misimu yake 10 akiwa City kulikuwa na matukio 28 ya timu kumiliki mpira kwa wastani wa zaidi ya asilimia 60 katika msimu mzima, likiwemo City yenyewe katika kila msimu. Hata hivyo, katika misimu ya 2024/25 na 2025/26, ni City pekee iliyofikia kiwango hicho. Huenda mabadiliko hayo yalionyesha jinsi mtindo wa soka ulivyokuwa ukibadilika.

GUARD 05

Baada ya michezo mitano ya msimu huu, Man City, Brighton na Tottenham zilikuwa na wastani wa umiliki wa mpira unaozidi asilimia 60. Hata hivyo, Tottenham ilikuwa mkiani mwa msimamo, jambo lililoonyesha kuwa kumiliki mpira kwa kiwango kikubwa hakutoshi kuhakikisha ushindi.

Kati ya mechi 50 za mwanzo 2026/27, katika mechi 22 kulikuwa na timu iliyomiliki mpira kwa angalau asilimia 60. Hata hivyo, timu hizo zilishinda mara nane tu, sawa na asilimia 36.4. Kiwango hicho kilikuwa cha tatu kwa uchache katika historia ya ligi kwa timu zenye umiliki huo. Rekodi ya chini zaidi iliwekwa msimu uliopita, ambapo kiwango cha ushindi kilikuwa asilimia 34.1.


GUARD 02

UMILIKI WA MPIRA UNAPOTEZA UFANISI?

Tangu 2005/06, timu zilizomiliki mpira kwa angalau asilimia 60 zimeshinda mechi 1,470 za Ligi Kuu England. Man City ilichangia ushindi 263, sawa na asilimia 17.9. Katika kipindi cha Guardiola akiwa City, timu zilizomiliki mpira kwa zaidi ya asilimia 60 zilishinda mechi 862, huku City ikichangia 205 (sawa na asilimia 23.8). Mabadiliko makubwa yalionekana baada ya msimu wa 2023/24. Katika mechi 202 ambazo timu moja ilimiliki mpira kwa angalau asilimia 60, timu zilizokuwa na umiliki mkubwa zilishinda mechi 108 (sawa na asilimia 53.5).

Msimu mmoja baadaye, takwimu zilishuka hadi mechi 146 na ushindi 57, sawa na silimia 39. Mabadiliko hayo yanaweza kuwa sehemu ya mageuzi ya kawaida ya mbinu za soka. Huenda pia timu zimeamua kuwa badala ya kujaribu kucheza kama Man City na kushindwa, ni bora kutumia mbinu tofauti ili kupata ushindi.

Katika msimu wa 2024/25, makocha waliopendelea soka la kumiliki mpira walijumuisha Guardiola, Enzo Maresca, Mikel Arteta, Ange Postecoglou, Russell Martin na Arne Slot. Kwa upande mwingine, Andoni Iraola, Thomas Frank, Sean Dyche, David Moyes, Oliver Glasner, Nuno Espirito Santo na Kieran McKenna walikuwa miongoni mwa makocha ambao timu zao hazikulenga kutawala umiliki wa mpira kwa kiwango kikubwa.

Mwezi Januari 2025, Guardiola alikiri kuwa kulikuwa na mabadiliko ya mbinu, akisema soka la kisasa lilikuwa likionekana katika namna Bournemouth, Brighton na Newcastle zilivyokuwa zikicheza, kama ambavyo Man City ilikuwa ikifanya hapo awali.


GUARD 03

MASHAMBULIZI YANAYOONGEZEKA

Ligi Kuu England imeshuhudia ongezeko la mashuti na mabao yanayotokana na mashambulizi ya kushtukiza. Hayo ni mashambulizi ya haraka yanayoanzia eneo la ulinzi wakati safu ya ulinzi ya mpinzani ikiwa bado haijajipanga kikamilifu. Kabla ya msimu wa 2024/25, hakuna msimu tangu 2006/07 uliokuwa na wastani wa zaidi ya mashuti 1.49 kwa mechi kutokana na mashambulizi hayo, au mabao 0.22 kwa mechi.

Katika misimu miwili iliyopita, wastani ulikuwa mashuti 1.79 na 1.75 kwa mechi, pamoja na mabao 0.29 na 0.23 kwa mechi.

Baada ya mechi 50 za msimu huu, wastani ulifikia mashuti 2.08 na mabao 0.34 kwa mechi, viwango vya juu zaidi vilivyorekodiwa. Hata hivyo, takwimu hizo zinaweza kubadilika kadri msimu unavyoendelea.

Matumizi ya ulinzi wa kumfuatilia mchezaji mmoja mmoja na presha ya juu yamechangia mabadiliko hayo. Mbinu hizo zinaweza kusaidia timu kuupokonya mpira mpinzani katika maeneo ya juu na kutengeneza nafasi za kufunga bila kuhitaji kumiliki mpira kwa muda mrefu. Hata hivyo, presha inaposhindwa kufanya kazi, inaweza kuacha nafasi kwa wapinzani kufanya mashambulizi ya haraka.

Katika msimu huu, ni timu saba tu zilizokuwa na wastani wa umiliki wa mpira unaozidi asilimia 50. Kati ya hizo, nne zilikuwa katika nusu ya juu ya msimamo na tatu katika nusu ya chini, hali inayoonyesha kuwa umiliki pekee hauwezi kuwa mafanikio ya timu. Brighton ni mfano mzuri. Ilianza msimu vizuri, lakini kipigo chake pekee katika mechi tano za mwanzo kilitokea dhidi ya Chelsea, licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 74.1.

Katika mchezo uliofuata uliotajwa kuwa bora kabla, Brighton iliifunga Arsenal, mabingwa watetezi, kwa mabao 3-0 ikiwa na umiliki wa mpira wa asilimia 40.1 tu. Chelsea iliifunga Brighton ikiwa na umiliki wa asilimia 25.9 na kuifunga Fulham ikiwa na asilimia 38.1. Hata hivyo, ilipoteza dhidi ya Brentford licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 59.8, na kutoka sare na Hull City ikiwa na umiliki wa asilimia 68.3.

Hii haimaanishi kuwa soka la kumiliki mpira limepitwa na wakati. Arsenal ilitwaa ubingwa wa msimu uliopita ikiwa na wastani wa umiliki wa asilimia 56.3, wa nne kwa ukubwa katika ligi. Pia, timu 11 kati ya 20 zilikuwa na wastani wa umiliki unaozidi asilimia 50.

Katika msimu huu, Man City na Brighton, ambazo zilikuwa miongoni mwa timu zinazoongoza kwa umiliki wa mpira, pia zilikuwa miongoni mwa timu tatu za juu kwenye msimamo wa ligi. Kwa hiyo, mwelekeo hauonyeshi kuwa umiliki wa mpira hauna umuhimu tena.

Badala yake, unaonyesha kuwa timu zinaweza kutumia mbinu tofauti kupata matokeo, huku mashambulizi ya haraka na matumizi mazuri ya nafasi yakizidi kuwa muhimu.

Huenda hali hii ikafanya kupunguza uzito ambao mashabiki wanatoa katika umiliki wa mpira kama kigezo cha kupima ubora wa timu. Baada ya yote, katika soka, jambo muhimu zaidi ni matokeo ya mwisho ya mchezo na idadi ya mabao yanayofungwa.