Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyuma ya wachezaji kutopeana mikono

Muktasari:

  • Katika mahojiano yaliyofanywa na Mwanaspoti na baadhi ya makocha na wachezaji, wanaelezea kuwepo sababu nyingi zinazosababisha kutokea miongoni mwao kutokusalimiana, huku kwa asilimia kubwa vikionekana vinaanzia nje ya uwanja.

JE, umewahi kujiuliza kipi kipo nyuma ya baadhi ya wachezaji wa mpira wa miguu duniani kushindwa kupeana mikono na wenzao kuonyesha mchezo huo ni wa amani na furaha? Mwanaspoti linafichua hilo.

Katika mahojiano yaliyofanywa na Mwanaspoti na baadhi ya makocha na wachezaji, wanaelezea kuwepo sababu nyingi zinazosababisha kutokea miongoni mwao kutokusalimiana, huku kwa asilimia kubwa vikionekana vinaanzia nje ya uwanja.

Huko majuu, tukio hilo lilitokea Februari 27, 2010, wakati Chelsea ilipocheza dhidi ya Manchester City katika Ligi Kuu England. Kabla ya mchezo, wachezaji walipanga mstari kwa ajili ya utaratibu wa kawaida wa kupeana mikono, lakini Wayne Bridge alipofika mbele ya John Terry, alikataa kunyoosha mkono wake.

Bridge aliendelea kupita mbele ya Terry bila kumtazama wala kumpa mkono, huku Terry akionekana kusubiri kwa muda mfupi. Tukio hilo lilinaswa na kamera na picha zake zikasambaa duniani, likawa moja ya matukio yaliyokumbukwa zaidi katika historia ya soka la England.

Kilichokuwa nyuma ya tukio hilo ni kuvunjika kwa uhusiano wa kirafiki kati ya wachezaji hao baada ya Terry kuhusishwa na uhusiano wa kimapenzi na Vanessa Perroncel, aliyekuwa mwenza wa zamani wa Bridge na mama wa mtoto wake. Sakata hilo lilimfanya Bridge ajitenge na Terry, huku akionyesha wazi kuwa hakutaka kulifanya jambo hilo lionekane kana kwamba kila kitu kilikuwa sawa.

Tukija Kibongobongo, kuna wachezaji ambao wamefunguka kuwahi kukutana na mikasa hiyo, ambapo nyuma yake mapenzi yalihusika na kushindwa kuhimili walipokutana na ‘watesi wao’.

WANACHOSEMA WACHEZAJI

Kipa wa zamani wa Simba, Yanga, Azam FC na Geita Gold, Deogratius Munishi ‘Dida’, anasema inatokea mara nyingi uwanjani baadhi ya wachezaji kutopeana mikono, akisisitiza kunakuwa na sababu nyingi nyuma ya kile kinachoonekana uwanjani.

“Unakuta mtaa mmoja mnaishi wachezaji wanne au zaidi na mnacheza timu tofauti, sasa unakuta mmoja amemkopesha mwenzake na hataki kulipa, unategemea kitu gani wakikutana uwanjani, lakini pia kuna suala la mahusiano, vipo vitu vingi sana nyuma yake,” anasema.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Said Makapu, anasema iliwahi kumtokea kutompa mchezaji mwenzake, lakini ishu ilikuwa ni kurushiana maneno.

Anasema: “Ilitokea wakati nipo Mashujaa, kuna mchezaji akasema huna lolote la kufanya, ungekuwa na lolote ungesalia Yanga, lakini baada ya hapo tukayamaliza, ilikuwa ni maneno ya kunitoa mchezoni.”€

Naye kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Said Mohamed ‘Nduda’ anasema: “Ingawa sikumbuki moja kwa moja kama imewahi kunitokea mimi kutompa mchezaji mkono, ila hayo mambo yapo, yanakuwa yametokana na vitu nje ya uwanja.”€

Kwa upande wake, kipa wa Mashujaa FC, Wilbol Maseke, imewahi kutokea kutompa mchezaji mwen-zake mkono, akitaja sababu nyingi zinakuwa zimetokana na nje ya uwanja.

“Inakuwa ni kutofautiana, tena inakuwa ni mchezaji unayejuana naye, ingawa siyo vitu vinavyoweza kuchukua muda mrefu. Sisi ni wanaume, tunaachana navyo, ukipata muda wa kumwambia ukweli ka-ma amekukosea unamwambia,” anasema Maseke.

MAKOCHA

Kocha wa zamani wa Azam FC, Meja mstaafu Abdul Mingange, anakiri wachezaji wanapokuwa na tofauti za nje, zinakuwa na athari kubwa uwanjani wakati wa kutekeleza majukumu yao, hivyo benchi la ufundi linapaswa kuweka umakini wanapoingia dimbani kujua sura zao zinazungumza kitu gani, ili ikiwezekana abadilishwe mapema kabla haijaigharimu timu.

“Katika mpira wa miguu kuna mambo manne muhimu utimamu wa mwili, ufundi, mbinu ya mpira na saikolojia, hivyo vitu vyote ni muhimu sana kwenye soka. Siyo wachezaji pekee ambao wanaweza wakakumbwa na changamoto hiyo, bali hata makocha na viongozi,” anasema Mingange na kuongeza:

“Nina visa vingi vya wachezaji. Kocha ni kama baba, mengine tunayaficha kama siri. Kuna timu nilikuwepo haikuwa na uchumi mzuri, sasa kulikuwa na mchezaji alikuwa na mke na watoto, kitendo cha kutotuma pesa ya matumizi nyumbani kwake kilileta shida na mwenza wake, hivyo akawa ana matukio ya ajabu ajabu sana uwanjani.

“Kuna siku moja kambini kiliibiwa kiroba cha unga na TV ambayo tulikuwa tunatazama wakati wa ma-pumziko. Baada ya kufanya utafiti nikagundua ni yeye alichukua kuipelekea familia yake. Mtu kama huyo akiingia uwanjani unadhani anakuwa na matukio gani?

“Kuna mwingine alikuwa na mawazo sana na mchezaji mzuri ambaye nilikuwa namtegemea kikosi cha kwanza. Nilipokaa naye na kumuuliza kwa nafasi kama baba, alisema alimtambulisha rafiki yake, mke kamsaliti na kumchukua na ni wa timu nyingine. Je, akiingia uwanjani unadhani ni rahisi kusalimiana? Hivyo kunakuwa na matukio mengi nyuma nje na kile kinachoonekana uwanjani. 

Kocha wa makipa wa Mbeya City, Patrick Mwangata, anasema: “Ukiona mchezaji hajasalimiana na mwenzake, kunakuwa na sababu. Kama makocha, unamuita na kumkalisha chini, ili kujua mpira wa miguu ni amani na furaha, ila huwa inatokea”

SAIKOLOJIA

Mwanasaikolojia Charles Nduku alisema ili mchezaji afanye vizuri uwanjani, lazima akili iwe na utayari, vinginevyo kunaweza kukaleta athari mbalimbali.

“Mchezaji anaweza akawa anacheza rafu akaumiza wachezaji wengine na kupewa kadi nyekundu ya kuigharimu timu yake, lakini wakati mwingine hata yeye mwenyewe akajikuta anapata changamoto mbalimbali, ndiyo maana ni muhimu sana wanasaikolojia kuwepo kwenye timu,” anasema Nduku.