Prime
Njia mbadala ya Azam FC kuvunja ufalme wa Simba, Yanga
UKIONA Azam FC inacheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Chamazi, na viti vyote vikiwa vimejaa ujue siku hiyo moja ya timu mbili za Kariakoo, Simba na Yanga, zipo hapo kucheza na wenyeji.
Lakini, ukiona viti vingi vitupu, ujue Azam inacheza na timu nyingine yoyote kati ya 14 za Ligi Kuu ya soka ya NBC. Hata ikiwa mechi kali namna gani kama vile dhidi ya Singida Black Stars au JKT ama Coastal Union, bado viti vingi vitakuwa vitupu.
Ungetegemea kuwa miongo miwili ingetosha kuwatambulisha matajiri hao wa Mbagala na kusomba watu kila wakati wanapocheza nyumbani kwao, lakini miaka 22 tangu wazaliwe mwaka 2004 hawajaweza kujaza uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 10,000.
Miaka 22 ilitosha kuzalisha mashabiki wapya wasio na chembechembe za Usimba na Uyanga na hivyo kuwa Azam kindakindaki, lakini bado klabu inasumbuka kutafuta wafuasi wake wa dhati.
Ungetegemea ile hali halisi kama ya barani Ulaya kwamba timu kutoka eneo fulani ina mashabiki kutoka eneo hilo wanaoiwaza kila wakati timu yao na kuipenda kwa dhati, lakini Azam haijaweza kufanya hivyo.
Eneo la Mbagala ni moja kati ya maeneo yenye watu wengi jijini Dar es Salaam ambao ni wakazi au wanaokwenda huko kwa shughuli za biashara na ajira. Eneo la Chamazi pia limejaa wakazi, sawa na eneo jingine la Mbande ambalo pia limechangamka sana.
Ungetegemea kizazi kipya cha maeneo hayo kingetekwa na ubora wa timu ya Azam uwanjani, ustadi wa uongozi katika kujenga wigo mpana wa mashabiki na mbinu pia za kuwasogeza karibu wakazi wakati wakiwa katika umri mdogo kiasi kwamba wanapofikia ujanani wanakuwa hawaelewi kitu kingine zaidi ya Azam FC.
Sijawahi kusikia uongozi wa Azam ukizungumzia kitu kama idara ya ushirikishaji mashabiki (fans engagement department), ambayo klabu za kisasa ni lazima iwe nayo kwa lengo la kuwaweka watu karibu na timu.
Niliwahi kusikia aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Yanga, Senzo Mbatha akizungumzia mpango wa kumbadili Haji Manara kutoka idara ya habari na kuwa mkuu wa idara kama hiyo, lakini sijui mpango huo uliishia wapi.
Lakini cha muhimu hapa ni jinsi ya klabu yenye misuli ya kifedha kama Azam inavyoweza kutumia uwezo wake kuwavuta karibu mashabiki na kuhakikisha mechi zake za nyumbani zinajaa viti na zinakuwa na hamasa.
Idara ya ushirikishaji mashabiki hufanya kazi zinazohusiana na shughuli za kijamii, hasa za maeneo yanayozunguka makao makuu ya klabu, mazingira mazuri ya uwanjani wakati wa mechi yanayoweza kusababisha mashabiki wajione wamethaminiwa, ununuzi wa tiketi na mauzo ya bidhaa ndani ya uwanja na pia mawasiliano kati ya mashabiki na timu.
Pia, idara hii hufanya kazi ya kupaza sauti za mashabiki ili wajione wanasikilizwa na uongozi katika uamuzi wao na hivyo kuiamini timu. Hii ndio idara ambayo ni daraja kati ya uongozi na mashabiki. Ungetegemea kuona viongozi na baadhi ya wachezaji nyota wa Azam wakishiriki katika matukio ya kijamii ya maeneo yanayozunguka Azam kama kushiriki vipindi vya michezo shuleni, kugawa mipira kwa shule, kutembelea vituo vya watoto wenye hali ngumu au kutumia runinga zao kubwa uwanjani kwao kuonyesha mechi ambazo Azam inacheza nje ya mkoa au nje ya nchi au fainali za mashindano makubwa.
Katika mauzo ya tiketi ungetegemea usikie mashabiki labda 20 watakaonunua tiketi kwanza watapata zawadi fulani au fursa ya kuonana na wachezaji baada ya mchezo na kupiga nao picha.
Ungetegemea kuona mashindano ya timu za mitaani za maeneo yanayozunguka Chamazi yakidhaminiwa na Azam na mambo mengine mengi.
Kuna kazi nyingi ambazo idara ya ushirikishaji mashabiki inaweza kufanya ili kuwasogeza mashabiki karibu zaidi na timu na kujenga kizazi kipya ambacho kitaepuka timu za Simba na Yanga.
Idara ya habari haina budi kuachana na ubishi wa nani zaidi kati vigogo hao wa Kariakoo na Azam FC kwa kuwa kila ubishi huongeza ukubwa wa klabu hizo maradufu badala ya kuzidogosha.
Idara inatakiwa ijikite zaidi na kusifu ubora wa timu, mazingira mazuri ya uwanja, unafuu wa tiketi na kushirikiana na idara ya ushirikishaji mashabiki kujenga mfumo bora wa mawasiliano na mashabiki kabla, wakati na baada ya mechi.
Azam isibweteke na uwingi wa mashabiki wanaoishangilia wakati ikicheza na moja ya timu za Kariakoo. Badala yake ijenge wigo mkubwa wa mashabiki wake watakaokuwa wanajaza uwanja wa Chamazi kila inapocheza na si wakati ikicheza na mapacha wa Kariakoo tu.