Prime
Mtego wa FVS unavyowapa jeuri waamuzi
Kumeibuka mijadala kuhusu matumizi ya teknolojia ya msaada wa video kwa mwamuzi wa mpira wa miguu (Football Vedio Support, FVS) baada ya utaratibu wa kuangalia marudio ya matukio kuanza kutofautiana kwa mechi moja hadi nyingine.
Awali mwamuzi wa kati alikuwa akienda hadi kwenye runinga iliyo kwenye meza pembeni ya uwanja kwenda kuomba marudio ya video ya tukio aliloamua ili awe na uhakika zaidi. Alichokuwa akifanya ni kuomba aone pande zote.
Na kwa kuwa mwendeshaji wa mashine ya kuonyesha marudio ya picha za video hana elimu au mafunzo ya uamuzi, refa hakuwa akijadiliana naye lolote zaidi ya kuomba afanyiwe kile anachokitaka.
Ghafla katika baadhi ya mechi kukaibuka majadiliano kati ya mwamuzi wa kati na mwamuzi wa akiba, ambaye kwa taratibu zetu hutoka mkoa huohuo unakochezewa mechi.
Na ghafla katika baadhi ya mechi kunaonekana hakuna teknolojia hiyo, jambo lililoibua maswali kwamba hivi ni ,mechi gani ni muhimu kuliko nyingine?
Kinachoonekana ni kukurupuka kuanza kuitumia teknolojia hiyo bila ya maandalizi ya kutosha, ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa waamuzi, mwongozo kwa timu na hata kuwa na mazungumzo na kampuni iliyopewa haki aa kurusha matangazo kwa televisheni kwa kuwa picha zake ndio hutumiwa kwa marudio hayo.
Elimu kwa umma, ambayo ni muhimu sana, pia haikuwepo na ndio maana kumekuwepo mijadala mingi redioni na mitandaoni kuhoji matumizi bora ya teknolojia hiyo. Mijadala ikiwa hasi, hasa kutokana na wanaojadili kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu jambo hilo, inaondoa thamani ya teknolojia hiyo na ladha ya ligi.
Tamko la kuanza kutumia teknolojia hiyo halikushereheshwa na lilifanywa kama sehemu tu ya mazungumzo ya kawaida kuhusu shughuli za mpira wa miguu na lilikuja ghafla sana.
Pengine hiyo ni ishara kubwa kwamba hakukuwa na maandalizi ya kutosha. Wapo wanaosema kuwa si waamuzi wote wanaochezesha mechi za Ligi Kuu waliopata mafunzo ya matumizi ya teknolojia hiyo.
Na hata hao waliopata hiyo elimu, walipewa na wataalamu wa kuendesha mashine na si wakufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) na ndio maana kumekuwa na matumizi yanayotofautiana.
Protoko za FVS zinataka refa wa kati asaidiwe na mwendeshaji mashine ya marudio tu ambaye kazi yake ni kumuonyesha mwamuzi tukio katika kasi tofauti, mnato, kutoka pande tofauti na kutenganisha skrini.
Kanuni inasema mwendesha mashine si lazima awe refa au mtu mwenye mafunzo ya uamuzi, bali fundi anayejua mambo hayo ya video. Hapo tunaweza kupata watu wa ajabu wa kuthubutu kumwambia refa afanye nini, kwa kuzingatia soka letu na utamaduni wetu.
Lakini mwamuzi wa akiba ataenda kuangalia marudio ya tukio iwapo goli litafungwa ili ajihakikishie kuwa hakukuwa na matatizo na baadaye amtaarifu refa. Pengine hili ndilo linawafanya waamuzi wa akiba kuvuka mipaka na kutaka kumshauri refa kila mara anapokwenda mezani.
Lakini lililo kubwa zaidi ni ile kanuni inayosema kuwa “uamuzi wa awali hauwezi kubadilishwa isipokuwa tu pale picha za marudio zitakapoonyesha uthibitisho wa dhahiri (clear evidence) kwamba uamuzi ulikuwa na kosa la wazi na dhahiri au kwamba kuna tukio halikuonekana”.
Kanuni hiyo ya sita kwa mujibu wa Fifa inaendelea kusema “kwa kuwa VS inahusisha idadi ndogo ya kamera, picha za marudio hazitakuwa ndio uamuzi wa mwisho na hivyo uamuzi wa kwanza unaweza usibadilishwe”.
Ukiangalia idadi ndogo ya kamera zinazotumika Ligi Kuu ya NBC ni wazi kuwa zinatumika chache na hivyo kama waamuzi watakuwa makini au watataka kufanya makusudi, wana uwezo wa kuendelea na maamuzi yao pale watakapoombwa kwenda kuangalia marudio.
Na hapo ndipo kulipotakiwa mazungumzo ya kina na mtangazaji wa mechi za Ligi ya NBC, Azam Media, kuhusu uwezekano wa kuongeza kamera ili kuboresha matumizi ya VS kwa kuwa zinazotumika sasa ni chache na zinaweza kusababisha waamuzi kuendelea na misimamo yao kwa kuwa wana kinga ya kanuni za Fifa.
Pia kukosekana kwa FS kwenye baadhi ya mechi kumehusishwa na uchache wa vifaa, jambo linalosababisha mashine moja kukimbizwa mikoa ya karibu na hivyo kunapokuwa na umbali mrefu inakosekana. Hili pia ni la kukosa maandalizi ya kutosha kwa ajili ya ujio wa teknolojia hiyo.
Awali niliona FVS kuwa inaweza kuwa ahueni kwa waamuzi ambao kwa takriban misimu mitatu wamekuwa wakitawala mijadala mbalimbali ya uchambuzi wa mechi za Ligi Kuu, kiasi cha kutuhumiwa kupendelea timu, kucheza michezo ya kubahatisha au kuonekana hawana mafunzo sahihi.
Lakini habari hizi za baadhi yao kutopata mafunzo na mtoaji mafunzo kutokuwa mtu mwenye elimu ya uamuzi, zinaanza kunipa wasiwasi. Ni muhimu sana kwa Shirikisho la Soka (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kuwa na maandalizi ya kutosha zinapotaka kutambulisha jambo jipya.
Teknolojia inayosaidia mwamuzi kufanya uamuzi haikupaswa ianzie kwenye mechi rasmi za Ligi Kuu, bali mashindano yanayohusisha timu chache kama Kombe la Mapinduzi, Ligi ya Muungano, mashindano ya vijana au mengine ambaypo hayaamui bingwa wa nchi.
Badala ya vyombo vya habari kujadili teknolojia hiyo baada ya kutumika, ilitakiwa kuwepo mijadala ya teknolojia hiyo muda mrefu kabla ya msimu kuanza. Leo hii unasikia mtangazaji anasema kila kocha ana nafasi nne za kuomba marudio wakati protoko za VS inasema kila kocha ana nafasi mbili.
Kama kuna mabadiliko kati ya VS inayoelezwa na Fifa na hii tunayoitumia, kulitakiwa kuwepo taarifa rasmi na sababu za kuongeza fursa kwa makocha kuomba marudio. Lakini kama makossa ya watangazaji, basi ni mamlaka kutokaa na wadau ili kuwaelimisha kuhusu uamuzi huo.
Nachokiona hadi sasa ni kwamba mijadala yote kuhusu kasoro za teknolojia hiyo ni mamlaka za soka kutokuwa na maandalizi ya kutosha ya ujio wa Football Video Support. Kama tulikimbilia kutumia VS ili kuacha alama, ni muhimu tupige hatua nyuma kuangalia wapi tulikosea na kurekebisha.