Prime
NIONAVYO: Waamuzi ligi kuu ni changamoto
Muktasari:
- Mdahalo huo ulihusisha wadau wengi na ulikuwa na joto kiasi cha kuamsha hisia za wengi, hasa wanaokerwa na matukio ya waamuzi wa soka.
JANA usiku nilibahatika kuhudhuria mdahalo kwa njia ya mtandao ulioendeshwa na gazeti dada la Mwananchi kupitia ukurasa wake wa X ambao zamani uliitwa Twitter.
Mdahalo huo ulihusisha wadau wengi na ulikuwa na joto kiasi cha kuamsha hisia za wengi, hasa wanaokerwa na matukio ya waamuzi wa soka.
Kazi ya uamuzi wa soka ni kazi kama nyingine za kitaalam ambazo si kila mtu anaweza kuamka asubuhi na kufanya bila ya kuwa na mafunzo pia vigezo fulani.
Shabiki wa mpira anapokuwa uwanjani au kwenye runinga anataka kuona mchezo ukifanyika kwa uhakika, kwani anaamini unaendeshwa na watu wenye werevu na weledi.
Baada ya kuwasikia ‘wadau’ wa soka nimekuja kugundua si waamuzi pekee wenye dosari, lakini hata umma unaowahukumu waamuzi nao una upungufu.
Jaribu kufikiria mwalimu anapofundisha darasani akaonyeshwa mubashara na runinga, nini yangekuwa maoni ya watazamaji? Bila shaka wengi wangemhukumu mwamuzi kwa jinsi kila mtu anavyoongozwa na uwezo wake wa kuielewa taaluma ya ualimu, uzoefu na hata mihemko.
Sheria za mchezo wowote ndizo hutofautisha mchezo husika na michezo mingine. Tofauti ya soka na mpira wa kikapu unaipata kutoka kwenye tofauti ya sheria za michezo hiyo.
Kwa maana hiyo sheria ya mchezo ndiyo kiini cha mchezo husika. Mtu akikosea katika kutafsiri sheria za mchezo husika basi anaupotosha mchezo na kufanya uchezwaji wake na hata maamuzi panapo ushindani yakashindwa kuwa sawia.
Waamuzi wa Ligi Kuu wamekuwa wakilaumiwa kiasi cha baadhi ya wadau kupendekeza mechi zenye ushindani mkubwa zichezeshwe na waamuzi kutoka nje ya nchi.
Ni ukweli usiopingika kuwa waamuzi wetu wanazo changamoto,lakini waamuzi wasio na changamoto tutawapata katika taifa gani. Kote ulimwenguni vilio vinafanana. Vilio dhidi ya maamuzi ya waamuzi, vilio dhidi ya upendeleo na hata vilio dhidi ya teknolojia ya usaidizi wa video (VAR).
Unajiuliza kama hawa wenzetu waliotangulia wanalia kama sisi, sasa tukimbilie wapi?
Mamlaka zinazohusika na mchezo wa mpira wa miguu zinatakiwa kuweka umuhimu sana kwenye elimu ya uamuzi. Haijalishi umetoa mafunzo kwa makocha, madaktari na hata wataalam wangapi, kama ligi haina waamuzi wazuri basi yote hayo ni kazi isiyo na maana. Elimu kwa waamuzi, hasa elimu sahihi ni muhimu ili kuhakikisha kiini cha mchezo kinafanya kazi kwa weledi wa hali ya juu.
Wako waamuzi wa Ligi Kuu ambao akichezesha mchezo unaona kuwa anapungukiwa na utaalamu. Mwamuzi anapokuwa na upungufu wa taaluma inapelekea yeye kutokuwa na hakika ya maamuzi yake na hivyo kuyumba katika maamuzi yake.
Hawa wanatakiwa kutathminiwa na kupewa mafunzo na mbinu za kufidia mapungufu yao na ikiwezekana wakashushwa kwenye ligi za chini kama sehemu ya mafunzo yao.
Hata hivyo, wako waamuzi ambao wanaonekana kuumudu mchezo katika mechi moja na kushindwa katika mechi nyingine.
Hapa ndipo wadau wanapokuwa na wasiwasi huenda mwamuzi alikuwa amepewa maelekezo au kuna msukumo kutoka mahali unaomfanya kwa makusudi asichezeshe mchezo kwa mujibu wa sheria 17.
Ligi Kuu ya Tanzania ni moja ya ligi zinazofanya vizuri katika Afrika. Kiwango cha kuwa miongoni mwa Ligi Bora 10 barani Afrika hakiwezi kuja bila kuwa na ufanisi katika uamuzi.
Kuna waamuzi wengi wanafanya vizuri lakini wale wachache ambao kibinadamu au kwa makusudi wanafanya vibaya wamesababisha waamuzi wote kuwa waanga wa usemi wa samaki mmoja akioza basi wote wameoza.
Wakati tunanyoosha kidole kuwalaumu waamuzi wetu, tunatakiwa pia kuangalia mazingira wanayofanyia kazi ikiwa ni pamoja na malipo na upatikanaji wa teknolojia saidizi.
Waamuzi wetu bado wanafanya kazi ambayo ni ya kujitolea katika ngazi ya mchezo wa kulipwa.
Waamuzi wanalipwa posho wakati wataalam wengi na wachezaji walio katika Ligi Kuu wanalipwa mishahara.
Zaidi ya hapo, waamuzi wetu bado wanafanya kazi kwa teknolojia ambayo haijafikia ile ya Kombe la Dunia la 1986 iliyoshindwa kuliona goli la mkono la Diego Maradona.
Hata hivyo, mashabiki wanawahukumu wataalam hawa wa sheria za mpira kwa kurejea teknolojia ya marudio ya televisheni.
Mazingira ya maamuzi ya mpira wa miguu ni magumu na yanahitaji majibu ndani ya sekunde chache na mwamuzi hana faida ya marudio ya televisheni kama ilivyo kwa shabiki.
Yote kwa yote, elimu, motisha, utaratibu mzuri wa kupanga madaraja ya waamuzi, udhibiti wa nidhamu, pia kupatikana kwa teknolojia wezeshi kutaweza kusukuma mbele kiwango cha waamuzi wa ligi kuu.
Hatuwezi kuwa na waamuzi wasiofanya makosa, lakini hayo niliyotaja yakizingatiwa, dhamira nzuri ya utendaji wa haki itaonekana. Inawezekana.
Mwandishi wa Makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).Unaweza kutuma maoni yako kupitia namba yake hapo juu.