NIONAVYO: Ukiacha ushindani... Yanga, Simba ni utalii tosha kwa mashabiki

Muktasari:
- Pamoja na kuwepo wa mvua siku hiyo, bado misafara ya mashabiki na wapenzi wa klabu hizo ilienda Kwa Mkapa ili kuliwahi pambano hilo kuonyesha Dabi ya Kariakoo ni kitu kingine linapokuja soka la Tanzania.
DABI ya Kariakoo hutawaliwa na mbwembwe kabla ya mchezo. Ni mchezo ambao kila kitu siku hiyo husahaulika ikiwamo mechi za kimataifa inazoshiriki timu hizo, kama ilivyokuwa Jumamosi ya Oktoba 19 wakti watani wa jadi na wakongwe wa soka nchini, Simba na Yanga zilipokutana. Katijka mchezo huo uliokuwa wa 113 kwa Ligi ya Bara tangu mwaka 1965, Yanga ilishinda kwa bao 1-0, lililotokana na kujifunga kwa beki wa Simba, Kelvin Kijili dakika za lala salama za mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kuwepo wa mvua siku hiyo, bado misafara ya mashabiki na wapenzi wa klabu hizo ilienda Kwa Mkapa ili kuliwahi pambano hilo kuonyesha Dabi ya Kariakoo ni kitu kingine linapokuja soka la Tanzania.
Kama hujui ni kwamba pambano la Dabi mchezo baina ya timu zinazotokea katika eneo moja la kijiografia au nchi moja au katika mashindano yanayozishirikisha timu mbili zenye upinzani mkubwa.
Neno 'Derby. asili yake ni mashindano ya farasi wenye upinzani kwenye miaka ya 1870 katika mji wa Derby ulioko Derbyshire, Uingereza.

Katika soka timu huanza upinzani kidogo kidogo, unaochochewa na mambo kadhaa zikiwemo tofauti za kidini, kisiasa, kipato na hata historia na utamaduni.
Wachezaji huja na kuondoka, walimu huja na kuondoka, viongozi huja na kuondoka na mashabiki huja na kuondoka lakini utani kati ya timu hizo ubaki pale pale.
Hakuna mchezo wenye maana kwa klabu yoyote zaidi ya mchezo wa mahasimu au watani wa jadi.
Tukiangalia pambano kati ya FC Barcelona na Real Madrid au El Clasico ni mpambano kati ya klabu zilizo kubwa kabisa katika Ligi ya Hispania ijulikanayo kama La Liga. Upinzani huu umedumu kwa miaka zaidi ya 120. Real Madrid imeshinda mara nyingi zaidi.

Timu hizi zinatoka katika maeneo jiografia tofauti, lakini upinzani wao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na ukweli, klabu hivi ndivyo vimetawala kwa kiasi kikubwa katika kuwania ubingwa wan nchi yao. Kuna chembe za kisiasa katika upinzani huu, kwani Barcelona inatokea katika jimbo la Catalonia ambalo limekuwa likitaka kujitenga na Hispania, huku Madrid ikiwa upande wa mfumo unaopinga nchi kugawanywa.
Mchezo kati ya klabu hivi huingiza mamilioni ya pesa kuanzia viingilio, haki za matangazo na bidhaa nyingine. Mji mwenyeji wa pambano hili hupata fedha nyingi kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani. Wachumi wanaliona pambano hili kama moja ya sekta ndani ya Hispania ambayo uchumi wake unakuwa zaidi ya uchumi wa taifa. Mpambano wa El Clasico ni chapa inayouzwa nje ya Hispania na Ulaya ni chapa ya kimataifa.
Mtandao wa kimichezo wa Goal.com umetaja pambano la watani wa jadi wakiliita kwa kimombo Dar Es Salaam Derby au Kariakoo Derby kuwa katika nafasi ya tano kwa ukubwa Afrika. Mpambano huo wa watani wa jadi unawakimbiza kwa karibu mapambano mengine ya mahasimu katika nchi za Tunisia, Morocco, Afrika ya Kusini na Misri (pambano la mahasimu la Cairo) lililo kileleni.
Uwekezaji mkubwa na kuongezeka kwa Azam FC kama moja ya timu tatu zinazowania ubingwa kunaweza kuongeza ladha katika uhasimu wa kimpira huko mbeleni.
Pambano kati ya Yanga na Simba limekuwa na mvuto wa aina yake. Pamoja na utani huu kuwa na miaka zaidi ya 80, lakini utani umeshamiri zaidi kuanzia miaka ya baada ya uhuru yaani miaka 60 iliyopita. Timu hizi zinatokea mitaa ya Msimbazi (Simba) na Twiga na Jangwani (Yanga) ambayo yote iko Kariakoo katika jiji la Dar es Salaam.

Pamoja na kuwa na historia iliyoanzia kwenye siasa, pambano hili limeziacha nyuma historia hizi na kuwa utani wa mpira pekee. Hii pengine ndiyo imepelekea pambano hilikuwa la watani zaidi kuliko mahasimu. Haishangazi familia moja wanatoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kushangilia timu tofauti.
Pambano la Yanga na Simba huchochea mapenzi na maendeleo ya mpira karibu kwa kila kijana. Ni kutokana na pambano hili ndoto za vijana wengi huwa ni kwamba siku moja achezee yanga au Simba. Waswahili wanasema kwa kawaida mtu hupenda Yanga na Simba kwanza kisha hupenda mpira wa miguu.
Niliuangalia mpambano wa wiki lililopita kupitia runinga. Hii ilinipa nafasi ya kuangalia umati uliofurika kuanzia majukwaa maalumu mpaka majukwaa ya kawaida. Kwa haraka niliweza kuona sura za watu waliotoka nje ya Tanzania wakitokea sehemu mbalimbali duniani. Hii sasa imekuwa kawaida ingawa ni jambo kubwa kwa jicho la kiuchumi.
Ukweli wa kwamba pambano hili linakuwa mubashara kwenye runinga ambako watu kutoka sehemu mbalimbali hulitazama. Ukweli wa kwamba hata Dar es Salaam linakofanyikia pambano bado runinga huwa mubashara majumbani kwa watu, kwenye mahoteli, kumbi nyingi za starehe na hata vibanda umiza.
Bado hilo halizuii watu zaidi ya 50,000 kwenda uwanjani. Siku za nyuma nilitembelea baadhi ya miji mikubwa ulaya; wao walizima runinga ikiwa timu za mji mmoja zinapambana kwa maana hawakuwa na uhakika wa kupata watu wa kuujaza uwanja ikiwa mchezo ungekuwa mubashara. Kwa pambano la watani wa jadi la Tanzania ni kinyume kabisa. Ni tukio lenye mizizi haswa mioyoni mwa watu.
Naweza kusema kwa sasa mpambano wa watani wa jadiumefikia kiwango ambacho unaweza kuingizwa kwenye kifurushi cha mtalii (tourist package).
Mathalani mtalii anatua Kilimanjaro kuona Mlima Kilimanjaro na mbuga za Kaskazini, kisha kwenda Dar es Salaam kuangalia mchezo wa Watani wa Jadi na kutoka hapo anaenda kwenye visiwa vya Mafia, Pemba au Zanzibar. Tiketi za mashirika ya ndege hata meli zinaweza kuunganishwa na tiketi ya kuingia uwanjani, hivyo kuongeza wageni na kuitangaza derby ya Dar es Salaam.
Utalii wa matukio kwa sasa ni utalii mkubwa kuliko utalii wa mazingira na maumbile. Rafiki yangu mmoja raia wa Argentina anayefanya kazi Doha, Qatar husafiri kila mwaka na familia yake kushuhudia pambano la Superclasico kati ya Boca Junior na River Plate za jijini Buenos Aires.

Yeye na mke wake wamegawanyika katika upenzi wao kwa timu hizi. Ni kiasi kikubwa cha fedha kufanya safari hiyo lakini mwenye mapenzi na kitu hajali gharama. Miji na majiji yanajitangaza na kuingiza watalii na kipato kupitia matukio hasa ya michezo na utamaduni.
Pamoja na mapato yanayotokana na viingilio,haki za runinga, mauzo ya jezi na bidhaa nyingine za klabu, mchezo huu huingiza fedha kwenye nyumba za wageni, kumbi za starehe na kadhalika. Pia siku ya mchezo huu hutoa ajira za moja kwa moja kwa wahudumu wa mchezo na hata wasafirishaji wakubwa kwa wadogo kama bodaboda.
Ni muda sasa mamlaka za utalii , jiji na sekta binafsi kuliona pambano la watani wa jadi kama fursa katika tukio hili. Mchezo wa watani wa jadi ni tukio linalojirudia kila mwaka kwa miongo mingi sasa.
Dabi ya Kariakoo ni sehemu ya utamaduni wa Dar es Salaam na Tanzania kwa jumla. Mchezo wa watani wa jadi ni bidhaa iliyokamilika hivyo izidi kuongezewa thamani na kutangazwa na manufaa yake yatazidi kupatikana.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).