NIONAVYO: Tunajua kushiriki, sasa tujifunze kushindana Afcon
Muktasari:
- Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi na majeruhi wapone haraka miili na roho zao. Amina.
Haikuwa wiki nzuri kwa Dar Es Salaam na Tanzania kwa jumla kutokana na vifo vya makumi ya wenzetu waliofukiwa na jengo lililoporomoka Kariakoo.
Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi na majeruhi wapone haraka miili na roho zao. Amina.
Kama faraja msibani, timu ya Taifa, Taifa Stars iliwapa furaha Watanzania baada ya kufuzu kwa mara ya nne Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Morocco mwakani.
Stars ilifuzu baada ya kuifunga Guinea bao 1-0 lililofungwa na Simon Msuva.
Kwenye kundi H, Guinea ilikuwa nafasi ya pili baada ya kuifunga DR Congo bao 1-0, kabla ya mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Msuva kugeuka Peter Tino (mfungaji dhidi ya Zambia mwaka 1979 kufuzu Afcon ya 1980) kwa kuwafunga Guinea bao moja lililotosha kuipeleka Stars Afcon.
Hakuna ubishi kufuzu mwaka 1980, kulikuwa mafanikio makubwa na ya kwanza kwa Tanzania.Ilikuwa ni kufuzu kwa kiwango cha sasa cha Kombe la Dunia kwani kulikuwa na nafasi nane tu kwa Afrika nzima.
Tangu hapo Tanzania imefuzu katika mashindano yenye nafasi 24 mwaka 2019, 2023 na sasa 2025.
Kufuzu fainali za 2025 lilikuwa ni jambo la muhimu sana kwa Tanzania ambayo inaenda kuwa mwenyeji mwenza pamoja na Kenya na Uganda fainali za mwaka 2027.
Kushiriki fainali za mwaka ni kutaijenga timu kiufundi na kisaikolojia ili iweze kufanya vizuri mwaka 2027.
Kuelekea 2027, kuna jambo moja linaushtua moyo wangu. Pamoja na kuingia fainali nne za Afcon, Stars haijawahi kushinda mchezo wowote wa makundi ukiachilia mbali ukweli haijawahi kushika nafasi ya pili kwenye kundi yaani kufuzu.
Tunaweza kusema timu ya mwaka 1980 ilifika hatua ambayo kwa sasa ingekuwa ni hatua ya robo fainali.
Hata hivyo, mwaka huo ni mbali sana kuelezea kiwango cha timu. Siyo siri kufuzu kwetu kwa 2019, 2023 na ya sasa ya 2025 ni matokeo ya kupanuliwa kwa nafasi za kufuzu Afcon.
Kulielewa hili, ni muhimu kujua kufuzu kwetu mara tatu hatujawahi kuongoza kundi na au hata kumkaribia aliyeongoza kundi.
Mara nyingi kama siyo zote tumefuzu mshindi wa kundi akiwa amekwishapatikana.
Matokeo yetu katika hatua tuliyoizoea ya makundi yamekuwa ni ya kinyonge mfano angalia:
-1980, Nigeria 3-Tanzania 1,Misri 2-Tanzania1,Ivory Coast 1-Tanzania 1 -2019, Senegal 2 - Tanzania 0, Kenya 3 - Tanzania 2,Algeria 3 - Tanzania 0 -2023, Morocco 3- Tanzania 0, Zambia 1 - Tanzania 1, Congo DR 1 - Tanzania 1.
Jambo chanya kwenye mashindano ya karibuni yaani yale ya Ivory Coast 2023 ni ile kuweza kutoka sare mara mbili, tena dhidi ya mataifa yaliyowahi kutwaa ubingwa wa Afrika.
Ikumbukwe kundi la Stars lilikuwa na mabingwa wa zamani Morocco, Congo DR na Zambia.
Labda kama si kuruhusu Zambia kusawazisha mwishoni, Stars ingeweza kwenda mbele ya hatua ya makundi kwa mara ya kwanza.
Kama kuna wakati wa Stars kujipima kifua kwa wakubwa, basi mashindano ya mwaka 2025 ndiyo nafasi pekee na ya kuchukuliwa kwa umakini.
Mashindano ya mwaka 2027 yanatulazimisha kwenda zaidi ya hatua ya makundi.
Kwa mwenyeji kutolewa hatua ya makundi, huwa ni fedhea kubwa na huyafanya mashindano yakadorora.Haina maana na itakuwa ni kupoteza rasilimali za umma iwapo timu mwenyeji inatolewa mapema.
Ukiondoa uzembe uliosababisha Stars kushindwa kuifunga Ethiopia katika mzunguko wa kwanza jijini Dar Es Salaam, Stars ya sasa imeonyesha uwezo wa kushindana hasa katika michezo dhidi ya Congo DR na Guinea ambazo ni timu zilizosheheni vipaji lukuki vinavyocheza Ulaya.
Huu ni wakati wa kujitia shime kuhakikisha timu yetu inakwenda Afcon kushindana kwelikweli.Michezo miwili ya mwisho ya Afcon 2023 dhidi ya Zambia na Congo DR itumike kuwatia wachezaji moyo wanaweza kushindana na yeyote.
Kwa vipaji vinavyoibuka vya wachezaji kama Clement Mzize, Adolf Bitegeko, Msindo ukiongeza uzoefu wa kina Baca, Job, Zimbwe, Mudathir, pia wakongwe kama Samatta, Msuva, Mkami, Kapombe na wengine wanaofanya vizuri, yakifanyika maandalizi na uratibu mzuri, Stars inaweza kwenda zaidi ya hatua ya makundi.
Ni kweli huwezi kumnenepesha ng’ombe siku ya mnada. Ni kweli hatuwezi kupata vipaji vingi kutoka Ulaya kama ilivyo kwa nchi za Magharibi na Kaskazini mwa Afrika.
Lakini ubora wa ligi ya Tanzania, mafanikio ya klabu za Tanzania kimataifa na ubora wa timu za vijana vinaweza kuwa vitalu vya kuzalisha wachezaji bora, pengine kuliko hata mataifa yale ambayo tayari yana utitiri wa wachezaji wanaotumika nje ya mataifa yao.
Wakati wa Tanzania kujidhihirisha kama taifa la soka ni sasa. Si taifa la kushangilia kutoka sare au kufuzu, ni taifa la kushindana.
Watu wanaopenda soka tunao labda kuliko taifa jingine lolote.
Serikali ya sasa inaunga mkono maendeleo ya michezo labda kuliko serikali yoyote iliyowahi kuwepo hapa nchini.
Sababu tunayo na nia tunayo,lililobaki ni Taifa Stars kuonyesha uwezo wa kushindana maana kushiriki tuna uzoefu.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).