Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Trump II na hatima ya michezo

Trump Pict
Trump Pict

Muktasari:

  • Kurejea kwa Rais Trump kuwa rais wa taifa la Marekani, kunaonekana kumewagusa viongozi wa Ulaya ambao walikutana jijini Budapest, Hungary kujadili mustakabali wa umoja huo na miradi au hata sera za usalama za Ulaya katika mkesha wa mabadiliko huko Marekani.

BAADA ya kuitumikia Marekani kama Rais wa 45, Donald John Trump amechaguliwa tena kuwa rais wa 47 wa Marekani.

Kurejea kwa Rais Trump kuwa rais wa taifa la Marekani, kunaonekana kumewagusa viongozi wa Ulaya ambao walikutana jijini Budapest, Hungary kujadili mustakabali wa umoja huo na miradi au hata sera za usalama za Ulaya katika mkesha wa mabadiliko huko Marekani.

Kuingia na kutoka kwa viongozi wa mataifa na wale wa serikali ni jambo la kawaida, lakini si kawaida taasisi za kimataifa kukaa ili kujadili ujio wa kiongozi mpya katika moja ya mataifa ya mbali.

Kuna msemo kuwa "Rais wa Marekani ni rais wa dunia". Unaweza kuwa si msemo mzuri kwa tunaotamani kuwa na dunia yenye usawa lakini ina ukweli mwingi kwani anayeongoza taifa hilo kubwa kiuchumi duniani kwa namna moja au nyingine anaathiri sera za hata nje ya taifa lake zikiwemo hata za sekta ya michezo.

TR01
TR01

Pamoja na nguvu ya ushawishi kimataifa, mabadiliko ya kiongozi wa nchi yoyote huathiri sera na mwenendo wa sekta ya michezo katika nchi husika. Uamuzi mkubwa wa kibajeti, kuandaa mashindano makubwa na wakati mwingine hata kushiriki mashindano makubwa kama ya Olimpiki na Kombe la Dunia kunaweza kutegemea utashi wa kisiasa wa kiongozi aliyeko madarakani.

Hapa Afrika tunayo mifano ya viongozi kama Paul Kagame wa Rwanda na Daktari Samia Suluhu Hassan wanavyochagiza maendeleo ya michezo.

Hakuna ubishi kwamba Marekani ni moja ya mataifa yenye nguvu za kimichezo duniani. Marekani imekuwa ikifanya vizuri na kunyakua medali na tuzo nyingi za michezo ikiwamo mpira wa kikapu, gofu, mpira wa miguu wa Kimarekani, tenisi, soka, riadha, ngumi na mingine mingi.

TR02
TR02

Marekani imeandaa mashindano ya kimataifa ya Olimpiki ya majira ya joto na ya baridi mara 8 ikiwa ni rekodi kubwa ambayo haijafikiwa na taifa jingine duniani. Kana kwamba haitoshi, Marekani inatarajiwa kuandaa Kombe la Dunia la mpira wa miguu, au soka kama wanavyoiita wao, kwa mara ya pili ifikapo mwaka 2026 ikiwa ni miaka 32 tangu waandae kwa mafanikio fainali za Kombe la Dunia za 1994. Fainali za mwaka 2026 pia zitagongana na sherehe za miaka 250 ya tangazo la uhuru wa taifa la Marekani/ USA la mwaka 1776.

Rais mteule Donald Trump anatarajiwa kukabidhiwa ofisi na mrithi aliye pia mtangulizi wake, rais wa 46, Joseph Biden ifikapo Januari 2025. DJ Trump ni mnazi mkubwa wa soka, mpira wa miguu wa kimarekani, gofu na pia mchezo wa ngumi. Kama ulikuwa hujui, rais Trump alicheza soka akiwa chuo kikuu katika miaka ya 1960. Rais Trump pia amecheza michezo mingine akiwa chuoni, jeshini na hata katika ngazi ya kulipwa. Kama mfanyabiashara, Trump alikuwa na bifu sana na vyama vya kitaifa hasa kile cha futiboli ya Kimarekani (NFL) na kile cha mpira wa kikapu (NBA).

TR03
TR03

Hii ilitokana na Trump kuwa mwanaharakati na pia kutamani kumiliki klabu kubwa za michezo hiyo bila ya mafanikio. Ziko rekodi nyingi za mashauri mahakamani na majaribio kadhaa ya Trump kununua klabu za Ligi ya NFL.

Trump pia aliwahi kuajiriwa na mwanamasumbwi Mike Tyson kama mshauri wake wa masuala ya kifedha mwaka 1988. Inasemekana Trump alitumia kiasi cha dola za Kimarekani milioni 11 kuandaa pambano la Mike Tyson na Michael Spinks na yeye pia kujiingizia dola 26 milioni kutokana na pambano hilo ambalo Tyson alilimaliza kwa sekunde 91. Mara tu baada ya pambano, makubaliano yakafanyika ya Trump kuwa mshauri na mpanga mikakati mkuu wa Tyson.

Katika kipindi chake cha kwanza katika Ikulu ya White House, Rais Trump anasemekana kuendeleza visasi dhidi ya vyama kama NFL na haijulikani kama bifu hilo limekwisha mpaka muda huu.

Kimataifa, Donald Trump si mgeni wa biashara na siasa za michezo. Matukio makubwa ya kimichezo yanayotarajiwa kufanyika Marekani mwaka 2026 na 2028 yaani Kombe la Dunia la soka na Michezo ya Olimpiki yalikabidhiwa kwa Marekani katika kipindi ambacho Donald Trump alikuwa madarakani.

TR04
TR04

Kuna urafiki mkubwa kati ya Donald Trump na Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Giani Infantino, ambaye kwa siku za hivi karibuni ameweka makazi yake huko Florida, Marekani, yaliko pia makazi ya DJT. Kamati za sheria na maadili za FIFA pia zimeweka makao yao huko Miami, Florida. Haikushangaza, kwa Infantino kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumpigia simu ya pongezi DJT mara baada ya kuchaguliwa.

Kukiwa na mashindano makubwa ya kimataifa, Klabu Bingwa ya Dunia, Kombe la Dunia na Olimpiki 2025, 2026 na 2028 mtawalia, Donald Trump atapata jukwaa la kuzitangaza sera zake kitaifa na kimataifa. Tusitegemee kila kitu kwenda sawa panapo uwepo wa Donald Trump. Hii inaweza kuwa nafasi ya kuimarika uhusiano kati ya Marekani na Chama cha Kimataifa cha Olimpiki (IOC) na pia Marekani na Fifa. Hili pia linaweza kuwa jukwaa na mwanzo wa mtafaruku kati ya Trump na vyama hivyo.

Sera za Trump kwa mfano kuhusu uhamiaji, zinaweza kuathiri ujio wa mashabiki kutoka nchi wanachama wa IOC na FIFA kushuhudia mashindano hayo makubwa. Masuala ya haki za binadamu kama kuwa na michezo jumuishi yanaweza pia kumgonganisha Trump na vyama hivyo. Trump ameshatamka wazi kutosapoti ushoga na ubadilishaji wa jinsia katika matukio ya hivi karibuni, FIFA na IOC wameonekana kukumbatia na kushirikisha jamii hiyo iitwayo LGBTQ. Bendera za mashoga na waliobadilisha jinsia (upinde wa mvua) zimeonekana kwenye viwanja vya michezo. Trump mwenyewe alisikika akilaani ushirikishaji wa alama za mashoga katika sherehe za ufunguzi wa Olimpiki ya majira ya kiangazi jijini Paris, Ufaransa mwaka huu kama "uwendawazimu mkubwa".

TR05
TR05

Suala jingine linaloweza kuamsha vinasaba vya Trump ni matumizi na mgawanyo wa fedha kati ya serikali ya shirikisho na majimbo yanayoandaa matukio. Trump ameshaeleza chuki ya wazi dhidi ya New York na majimbo mengine na kama ilivyo kawaida yake hakawii kulipiza visasi kupitia michezo hii. Labda tuwekeze katika umri wa miaka 78 na ushee atakaokuwa nao Trump, huenda baadhi ya vita akaziweka pembeni.

Kwa ujumla ni kuwa ujio wa Trump umemuibua tena mwanamichezo mwenye mapenzi makubwa sana na michezo. Ujio wa Trump umemuibua tena mtu mtata asiyeona haya kugombana na mamlaka za michezo hasa linapokuja suala la maslahi anayoyaamini. Trump ni baraka au ni balaa kwa michezo? Muda utaeleza.

 Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.