NIONAVYO: Stars ina kibarua kizito Afcon 2025 Morocco
Muktasari:
- Katika mashindano hayo yanayoanza Desemba 21, 2025 na kufika tamati Januari 18, 2026 timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imepangwa katika Kundi la C lenye timu nyingine za Tunisia, Nigeria na Uganda.
KIPYENGA cha kuanza mashindano ya mataifa ya Afrika (Afcon) kwa mwaka 2025 kilipulizwa mwanzoni mwa wiki hii jijini Rabat, Morocco.
Katika mashindano hayo yanayoanza Desemba 21, 2025 na kufika tamati Januari 18, 2026 timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imepangwa katika Kundi la C lenye timu nyingine za Tunisia, Nigeria na Uganda.
Kwa mujibu wa takwimu za sasa za FIFA na CAF, Tanzania ndiye mnyonge (underdog) wa kundi na hivyo iliwekwa kwenye chungu cha nne na cha mwisho katika upangaji wa ratiba.
Hata hivyo, uzoefu umeonyesha kuwa viwango vya CAF na Fifa vimekuwa si kipimo cha mwisho au kiashiria cha matokeo katika mashindano haya.
Pamoja na kuwa na alama chache katika viwango, Tanzania pia ina rekodi ambayo si nzuri katika mashindano haya ukilinganisha na washindani katika kundi lake.
Tanzania ilishiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano haya mwaka 1980 ikiwa ni miaka zaidi ya 20 tangu mashindano hayo yachezwe kwa mara ya kwanza Sudan mwaka 1957.
Taifa Stars iliyofuzu kushiriki mashindano ya mwaka 1980 huko Nigeria, inasemekana ndio Taifa Stars iliyokuwa bora katika historia kwani ilifuzu kuwa miongoni mwa timu 8 tu, tofauti na sasa ambapo mashindano yanashirikisha timu 24, yaani takribani nusu ya bara zima la Afrika ambalo lina mataifa 54.
Katika mfumo wa kufuzu kwa timu 24, Taifa Stars mara zote tatu imesubiri kufuzu siku ya mwisho na haijawahi kuongoza kundi.
Kama ilivyokuwa mwaka 1980 hadi sasa, Taifa Stars haijawahi kuvuka hatua ya makundi au hata kushinda mchezo wowote wa hatua ya makundi.
Mashindano ya Afcon 2025, Morocco ni mtihani kwa Taifa Stars kuona kama inaweza kuondokana na jinamizi la kutovuka hatua ya makundi.
Kubwa zaidi kwa Taifa Stars, mashindano ya Morocco yatakuwa ni uwanja muhimu wa kujipima uwezo kuelekea Afcon ya 2027 ambayo Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja watakuwa wenyeji.
Kufanya vizuri kwa Tanzania katika mashindano ya Morocco kutajenga matumaini ya mashabiki na kuongeza shauku kuelekea Afcon 2027.
Kufanya vizuri kwa Taifa Stars kutawajengea wachezaji hali ya kujiamini na hali hiyo wakienda nayo kwenye Afcon ya nyumbani, tunaweza kushuhudia timu yetu ikifika mbali. Hakuna jambo baya kama mwenyeji wa mashindano kutofika mbali.
Kufika mbali kwa mwenyeji wa mashindano kutavutia mashabiki kufurika viwanjani na kufuatilia mashindano.
Pamoja na rekodi isiyoridhisha tuliyoiona hapo juu, Taifa Stars sasa ina nia, sababu na uwezo wa kupambana na Nigeria, Tunisia na Uganda. Uzoefu wa karibuni umeonyesha kuwa timu zenye wachezaji wengi wanaocheza kwenye ligi za nyumbani kama Afrika Kusini na Misri zimekuwa tishio hata kwa timu zenye wachezaji wengi wanaocheza Ulaya.
Wachezaji wanaocheza ligi moja ya nyumbani wana uwezekano mkubwa wa kuelewana na kucheza pamoja vizuri kuliko wachezaji wanaotokea klabu mbalimbali duniani wasio na uelewano. Tuliona pia katika Afcon iliyopita nchini Ivory Coast, Taifa Stars ilizisumbua Congo DR na Zambia zenye wachezaji wengi Ulaya na kama si kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Morocco, hadithi ingekuwa nyingine.
Pamoja na kutokuwa na wachezaji wengi wanaocheza Ulaya, Taifa Stars ina wachezaji wenye majina na uzoefu katika ligi za klabu barani Afrika.
Klabu za Yanga na Simba ni kati ya timu 15 za Afrika zilizofanya vizuri katika mwaka 2024 kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Takwimu na Historia ya Soka (IFFHS).
Shirika hilo pia limeitaja Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuwa Ligi ya 4 kwa Ubora Afrika ikitanguliwa na Misri, Morocco na Algeria.
Kwa wachezaji wengi wa timu ya taifa kucheza kwenye ligi bora wataweza kunoa makali yao na kuwa bora zaidi na ubora huo utakuwa msaada kwa Taifa Stars.
Ligi bora pia imeanza kuvutia wachezaji wa kigeni kuomba uraia wa Tanzania. Hivyo, kwa wale ambao hawajachezea timu za mataifa yao ya asili na wana viwango vitakavyoridhiwa na benchi la ufundi wanaweza kuongeza kitu kwenye timu ya taifa.
Maandalizi ya timu ya taifa kwa ajili ya Afcon 2025 yatafaidika na uwepo wa mashindano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Mashindano ya CHAN yanatajiwa kufanyika mwezi wa Agosti 2025 katika mataifa wenyeji wenza ya Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwa kuwa mashindano hayo yamepishana kwa miezi minne tu, benchi la ufundi linaweza kuwa na mpango mrefu (extended program) kwa timu ya CHAN na ile ya Afcon kwa kuwa wachezaji wengi watakaoshiriki CHAN ndio wanatengeneza uti wa mgongo wa Taifa Stars ya Afcon.
Afcon 2025 Morocco ni kiunzi kirefu kwa Taifa Stars ambacho ikiwa itafanikiwa kukiruka, itakuwa imejisogeza miongoni mwa vigogo wa soka barani Afrika.
Nadharia kwamba Tanzania ni nchi ya wapenda mpira kuliko wacheza mpira inaweza kufika mwisho iwapo Taifa Stars itaanza kufanya vizuri katika Afcon.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mtumie maoni yako kupitia namba yake ya simu hapo juu.