Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Rubiales atanusurika na nusu-busu la Kifo?

FAINALI za Kombe la Dunia la Mpira wa miguu kwa upande wa wanawake lilitamatika hivi karibuni kwa Hispania kuichapa England kwa bao 1-0.

Ni tukio la aina yake katika historia ya mpira wa wanawake ambao unazidi kusonga mbele kadri siku zinavyokwenda. Japo haujafikia kiwango cha wanaume, lakini umeongezeka kwa umaarufu, yaani kuchezwa na kutazamwa sehemu nyingi duniani hata katika nchi zilizokuwa na misimamo ya kihafidhina kuhusu wanawake kucheza mpira wa miguu. Kombe la Dunia la Australia na New Zealand limeacha kumbukumbu na rekodi nyingi mpya katika ulimwengu wa soka. Labda mwenye kumbukumbu itakayodumu maisha yake yote ni Rais wa Chama cha Soka cha Hispania (RFEF). Luis Manuel Rubiales Bejar ambaye ana kumbukumbu nzuri ya taifa lake kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, hivyo kufikia rekodi ya ile timu ya wanaume iliyotwaa ubingwa wa pekee miaka 13 iliyopita nchini Afrika ya Kusini. Kama hiyo haitoshi, Rubiales hatasahau kadhia iliyomkumba kufuatia nusu busu alilompa  mchezaji wa mabingwa hao wapya wa dunia Jenni Hermoso wakati wakisherehekea ubingwa huo. Picha za televisheni na za mnato duniani kote zilimnasa Rubiales akiwa na furaha kubwa kiasi cha kukosa staha hasa kwa mtu wa nafasi yake.

Baada ya tukio la busu kunaswa duniani kote, mchezaji Jenni Hermoso alikuja hadharani na kutamka jinsi alivyochukizwa na usherehekeaji huo usio na staha alioufanya mkuu huyo wa mpira na kwamba busu hilo lilikuwa la kulazimishwa. Tamko la mchezaji huyo likawa kama limetia mafuta ya petroli kwenye mbuga za savanna. Wito ulianza kusikika kutoka ndani na nje ya nchi kulaani busu la Rubiales. Serikali, Kamati  ya Utendaji na vyama vya mpira vya mikoa vilipaza sauti kumtaka mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 47 ajiuzulu.

Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), limekwenda hatua zaidi kwa kufungua shauri la kinidhamu dhidi ya Rubiales, ambaye enzi zake alicheza mechi 53 za La Liga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Fifa, Jorge Ivan Palacio, kwa kutumia mamlaka aliyopewa na ibara ya 51 ya kanuni za nidhamu za shirikisho hilo (FIFA Disciplinary Code), amemsimamisha Rubiales kujihusisha na shughuli zote za soka kwa siku 90 kupisha uchunguzi wa suala hilo. Fifa pia imemzuia Rubiales na maofisa wa chama cha mpira kuwasiliana kwa namna yoyote na mchezaji Hermoso au mawakala wake.

Shirikisho la Soka la Hispania limeliomba Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) kuifungia nchi hiyo kwa madai ya serikali kujiingiza katika suala hilo ambalo ni la kimpira. Kama hatua hiyo ingechukuliwa na Uefa, basi klabu za Hispania zingeondolewa kwenye mashindano ya Ulaya ambayo kiukweli hunogeshwa na timu za huko hasa Real Madrid na Barcelona.

Nafasi ya Rais wa Chama cha Soka ni nafasi kubwa na yenye nguvu katika maisha ya kila siku ya mpira wa miguu. Nafasi ya urais wa chama cha mpira wa miguu inaweza kumpa mtu marafiki wengi na maadui wengi pia. Pamoja na vidole vyote anavyonyooshewa rais huyo, bado kuna wanaoyaona hayo yote kama sehemu ya njama za maadui wake katika siasa za mpira zinazoendelea ndani na  nje ya nchi.

Mpira wa miguu una siasa zake ambazo kwa walio nje si rahisi kuziona kwa sababu vyombo vya habari mara nyingi hutoa taarifa za matukio bila kuingia undani wa tukio au sababu ya tukio kushikiwa bango. Kile kinachoonekana huchukuliwa kuwa ndicho kiini kumbe wakati mwingine huwa ni matokeo ya mvutano wa kisiasa. Kosa au tukio lolote linalompata adui basi hutumika kama njia ya kuchukulia ushindi. Hata katika hili haitashangaza kusikia kuhusika kwa namna moja au nyingine kwa maadui wa Rubiales walioko ndani ya Hispania Uefa na hata Fifa katika shinikizo la kumtaka ang’atuke madarakani.

Kashfa za namna hii siyo ngeni katika ulimwengu wa michezo hasa katika mpira wa miguu. Wako waliowahi kujikuta katika hali hii na kunusurika lakini pia wako ambao hazikuwaacha salama. Mwezi Februari mwaka huu rais wa chama cha mpira cha Ufaransa, Noel Le Graet alilazimika kujiuzulu baada ya tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia zilizoanzishwa na malalamiko ya wakala Sonia Soud.

Masuala ya kijinsia katika uendeshaji wa mpira wa wanawake yamekuwa ni changamoto kubwa sana hasa wakati huu mpira wa wanawake unapokua kwa kasi. Mazoea ya uendeshaji wa mpira wa kiume na ubabe wa kiume umekuwa ukipigwa vita sana. Kwa upande mwingine watu wanaona kwamba harakati za kijinsia zilizojuu katika Ulaya zimejipenyeza mno katika mpira wa miguu kiasi cha kuufanya usitawalike hasa kwa upande wa mpira wa wanawake.

Rais Rubiales amekataa kujiuzulu na kusema atajitetea mpaka mwisho kuthibitisha kwamba hakutenda kosa. Ametuma mkanda wa video kwa Fifa kuonyesha mchezaji alivyokuwa akifurahia picha yake akipigwa busu na rais huyo; lengo likiwa kuonyesha kwamba nusu busu hilo lilikuwa la makubaliano katika hali ya furaha iliyopitiliza. Mkutano mkuu wa dharura wa RFEF umeitishwa Jumatatu ijayo kujadili suala hilo na pengine kulitolea uamuzi.

Mama mzazi wa Luis Rubiales amejifungia kanisani kwenye usharika mmoja kusini mwa Hispania akiweka mgomo wa kula kushinikiza mwanae atendewe haki. Bi Angeles Bejar amemtaka mchezaji Jenni Hermoso arudi kwenye kauli yake ya kwanza iliyoeleza kuwa busu halikuwa la kulazimishwa ili aweze kumtoa hatiani mwanae huyo ambaye katika umri wa miaka 47 hajapata ndoa.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.