Ibrahim Class aongoza kimataifa
Muktasari:
- Chombo hiko kimemtaja Ibrahim Class Mgender kuwa ndiye bondia anayeongoza katika nafasi za kimataifa akishika nafasi ya 19 katika uzani wa Super Featherweight.
HALI ya viwango vya mabondia wa Tanzania duniani imekuwa ya kupanda na kushuka. Kwa mujibu wa Tathmini ya viwango vya WBC, chombo kikubwa cha ngumi duniani kinachotoa viwango vya mabondia na kuandaa mapambano ya ubingwa.
Chombo hiko kimemtaja Ibrahim Class Mgender kuwa ndiye bondia anayeongoza katika nafasi za kimataifa akishika nafasi ya 19 katika uzani wa Super Featherweight.
Tathmini ya viwango vya WBC, pamoja na orodha zinazokusanya nafasi za WBA, WBC, IBF, WBO na The Ring, inaonyesha kuanzia June hadi mwezi Julai Tanzania ina mabondia watano wanaoonekana kwenye viwango vya bora vya mashirikisho makubwa, ingawa hakuna Mtanzania anayeshikilia ubingwa wa dunia au kuwa ndani ya 10 bora ya dunia kwa Julai 2026.
IBRAHIM CLASS
Anayeongoza kwa sasa ni Ibrahim Class anayeshika nafasi ya 19 katika uzani wa Super Featherweight kwenye WBC. Hii ni hatua kubwa kwa bondia huyo ambaye amekuwa akipanda katika miaka ya hivi karibuni.
Mgender alikuwa nafasi ya 20 kwenye viwango vya WBC vya mwezi Mei, lakini Julai amepanda hadi nafasi ya 19. Jambo kubwa zaidi ni kwamba amekuwa akifanya hivyo akiwa ameshikilia mkanda wa WBC International katika uzani huo.
Kilichofanya Mgender kupanda nafasi moja juu ni matokeo yake ya mwezi April mwaka huu. Bondia huyo alikutana tena na Mthai Kritiphak Duangnut katika pambano la kuwania mkanda wa WBC International, baada ya pambano lao la kwanza kumalizika kwa sare.
Kwenye pambano hilo bondia huyo alishinda kwa TKO ya raundi ya tano Class ndiye namba moja Tanzania kwa sasa.
IBRAHIM MAFIA
Anayefuata kwenye listi hiyo ni Ibrahim Mafia, ambaye aliwahi kuwa miongoni mwa mabondia waliopanda kwa kasi zaidi kwenye viwango vya WBC, kwa sasa yupo nafasi ya 27 katika uzani wa Bantamweight. Hii ni tofauti kubwa ukilinganisha na Agosti 2025 alipofika nafasi ya 10 duniani katika uzani huo.
Mafia hakufika hapo kwa bahati mbaya. Mwaka uliopita alipanda kutoka nafasi ya 17 hadi 13 na baadaye kufika 10 baada ya ushindi wa knockout dhidi ya Alliu Bamidele Lasisi wa Nigeria. Mwanaspoti wakati huo liliripoti kupanda kwake kama moja ya hatua kubwa za bondia huyo katika mchezo wa ngumi za kulipwa.
Mafia alianza kushuka baada ya kipigo cha TKO dhidi ya Mfilipino Alvin Camique, kilichotokea Oktoba 2025. Kabla ya pambano hilo alikuwa akishika nafasi ya 11 kwenye viwango vya WBC vya Bantamweight, lakini kipigo hicho kiliathiri safari yake ya kupanda viwango.
Baadaye WBC pia ilimvua mkanda wake wa WBC Africa Bantamweight kutokana na ukiukwaji wa taratibu za mashirikisho hayo.
YOHANA MCHANJA
Mchanja sasa yuko nafasi ya 34 katika uzani wa Flyweight kwenye WBC. Viwango vya Juni bondia huyo alikuwa nafasi ya 33, maana yake ameshuka nafasi moja ndani ya mwezi mmoja.
Mwaka 2025 aliwahi kutajwa akiwa kinara wa uzani wa Flyweight kwenye baadhi ya viwango vilivyotumika Tanzania, huku akiwa na mkanda wa WBO Global.
Mchanja, ambaye anasimamiwa na Mafia Boxing mwaka 2025 alikuwa na mapambano 25, sasa ana jumla ya mapambano 28 katika ngumi za kulipwa, akishinda 21, kupoteza sita na kutoka sare mara moja.
Hivyo kushuka nafasi moja ina maana kwamba hivi karibuni hakupata mechi ya kimataifa ambayo ingemuweka kwenye kileleni.
Mwaka 2025 alimshinda kwa pointi mpinzani wake Miel Farjado kutoka Ufilipino katika pambano la raundi 12 lililofanyika Ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar na kumfanya bondia huyo kupanda viwango.
Lakini tangu hapo Mchanja hakuwa na muendelezo mzuri kwenye mapambano ya kimataifa jambo lililomfanya kushuka kwenye viwango.
FADHILI MAJIHA
Jina jingine ni Fadhili Majiha, bondia ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na hadhi ya Tanzania One.
Kwa sasa Majiha yupo nafasi ya 34 katika uzani wa Super Bantamweight kwenye WBC, akishuka nafasi moja kutoka 33. Lakini historia yake inaonyesha uwezo wa kupanda zaidi ya hapo. Box-Rank inaonyesha kuwa Majiha aliwahi kufika nafasi ya saba katika WBC Super Bantamweight mwezi Machi 2025.
Mwezi Februari mwaka huu, Majiha alikuwa ametajwa na The Respondents kuwa bondia namba moja Tanzania kwa mujibu wa BoxRec, akiwa nafasi ya 291 duniani na wa 22 Afrika kwa ujumla.
Ushindi wake wa knockout ya raundi ya kwanza dhidi ya Harjot Singh wa India Januari 31 ulitajwa kuwa moja ya matokeo yaliyomsaidia katika viwango hivyo.
Lakini kinachomtofautisha Majiha na baadhi ya wenzake ni kwamba tayari ana uzoefu wa kucheza mapambano makubwa na kubeba mikanda ya kikanda.
Fadhili Majiha, mwenye rekodi ya mapambano 53, ameshinda 35, amepoteza 14 na kutoka sare mara nne, huku ushindi wake 15 ukiwa kwa KO. Pambano lake la mwisho lilikuwa Januari 31, 2026, alipomtwanga Harjot Singh kwa TKO ya raundi ya kwanza.
HASSAN MWAKNYO
Kwa rekodi ya sasa, Hassan Mwakinyo amecheza mapambano 28, akishinda 25, kupoteza tatu, huku 18 kati ya ushindi wake ukiwa kwa KO/TKO. Ushindi mkubwa wa kimataifa ulikuwa dhidi ya Sam Eggington kwa TKO raundi ya pili England mwaka 2018, lakini baadaye alipoteza kwa Liam Smith kwa TKO raundi ya nne mwaka 2022 na Michel Soro kwa TKO raundi ya tisa Juni 2026.
Mwakinyo mwaka huu umekuwa wa changamoto zaidi kwake. Ingawa bondia huyo bado ni jina kubwa katika ngumi za Tanzania na ana mikanda kadhaa ya kikanda katika historia yake.
Lakini Juni 10 mwaka huu alikutana na Michel Soro katika pambano la kuwania mkanda wa IBO Middleweight, na Mtanzania huyo akapigwa raundi ya tisa na kupoteza pambano.
Kabla ya hapo, ABU Juni ilimtaja Mwakinyo kwamba ni bondia namba moja katika Middleweight Afrika, jambo linaloonyesha kuwa bado alikuwa na heshima kubwa katika viwango vya bara. Lakini matokeo dhidi ya Soro yameathiri kwenye safari yake ya kurejea kwenye viwango vya juu vya kimataifa.
Hapo ndipo changamoto kubwa kwa mabondia wa Tanzania.Si kushinda tu, bali kushinda mapambano yanayoweza kubadilisha nafasi yako kwenye viwango.
Kwa sasa, Box-Rank inaonyesha Tanzania ina mabondia watano wanaoonekana katika viwango vya mashirikisho makubwa Majiha, Class Mgender, Ibrahim Mafia, Mchanja Yohana na Mwakinyo. Lakini hakuna aliyopo ndani ya 10 bora au mwenye ubingwa wa dunia katika orodha hiyo ya Julai 2026. Hii inaonyesha Tanzania bado iko kwenye safari ya kutafuta mrithi wa kizazi cha mabondia waliowahi kufika mbali zaidi kwenye viwango vya dunia.
Habari njema ni kwamba Class anaonyesha dalili za kuwa kwenye nafasi nzuri. Mkanda wa WBC International na nafasi ya 19 ni msingi mzuri wa kuanza kusukuma kuelekea 15 bora, 10 bora na hatimaye nafasi ya kuwania ubingwa wa dunia.
WASIKIE HAWA
Akizungumza na Mwanaspoti, Dorothea Teddy anasema mwaka huu hakuna bondia wa kike Tanzania aliyeingia kwenye orodha hiyo kutokana na kutopata mechi mara kwa mara.
“Hatupati mechi za mara kwa mara hiyo ndio sababu ila mabondia wanawake wapo, ingekuwa angalau kwa baada ya miezi mitatu hadi minne kuna bondia wa kike anapigana nje ingesaidia angalau kutusogeza.”
Kuhusu kushuka kiwango Mwakinyo anasema watu hawafahamu kuhusu ngumi lakini ni jambo la kawaida kwenye mchezo huo.
“Kushushwa ni vitu vya kawaida kwa sababu watu hawajui kuhusu ngumi, unawekwa kwenye rank ikiwa unapigana mara kwa mara, ikiwa hupigani ina maana unawapisha wanaopigana mara kwa mara, haimaanishi kuwa ni bondia mbaya.”