Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: nilisita kwenda mechi ya Azam na JKT mbweni

Muktasari:

  • Kwa miaka mingi hapa Tazania,ukosefu wa viwanja bora ilikuwa ni moja ya vilio vya wapenzi na wadau wa maendeleo ya mpira wa miguu au kandanda.

MCHEZO wa soka hauwezi kukamilika bila ya kuwepo uwanja. Mindombinu mizuri ya kuchezea ni muhimu sana katika maendeleo ya mchezo huo na hata michezo mingine ya viwanjani.

Kwa miaka mingi hapa Tazania,ukosefu wa viwanja bora ilikuwa ni moja ya vilio vya wapenzi na wadau wa maendeleo ya mpira wa miguu au kandanda.

Sheria namba moja kati ya sheria 17 za mpira wa miguu (17 Laws of the Game) inatamka na kutambua uwepo wa uwanja. Sheria inatamka wazi kuwa uwanja utakuwa wa mstatili na uliowekewa alama zisizo hatarishi.

Alama za uwanjani ni pamoja na zile za mipaka ya nje ya uwanja na mipaka ya maeneo ya ndani kama duara la katikati ya kiwanja, mraba wa penalti nk.

Hizo pointi zote haziwezi kuonekana vizuri kama uwanja si msafi au nyasi za uwanja hazijakatwa kwa urefu unaotakiwa. Pia nyasi ndefu (zilizokatwa zaidi ya inchi 1 kutoka sakafuni) huwa kikwazo kwa mpira kutembea haraka.

Niliposikia mchezo wa Ligi Kuu Bara wa Jumatano wiki hii kati ya JKT Tanzania na Azam FC unafanyika kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo pale Mbweni, nilisita kulikubali wazo la kwenda uwanjani japo Mbweni si mbali sana kutoka nyumbani kwangu.

Nilifikiri sana hali ya uwanja ule ilivyokuwa kwenye michezo ya kuelekea mwisho mwa msimu wa 2023/24 na hasa mchezo wa marudiano kati ya JKT Tanzania na Yanga ambao ulichezwa katika hali iliyokuwa mithili jaruba la mpunga.

Kumbuka uwanja huo ulifungiwa na TFF hapo awali na kisha kufunguliwa Februari 5, hivyo JKT Tanzania na ile ya wanawake ya JKT Queens kuanza kutumia uwanja huo kwa michezo ya raundi ya pili ya msimu.

Baada ya mchezo wa Yanga, uwanja wa Isamuhyo haukutumika tena katika ligi na hata akilini mwa wapenzi wa mpira haukuwemo tena.

Baada ya kujiuliza mara mbili nikaamua kuutazama mchezo wa JKT na Azam kutokea sebuleni kwangu kwenye televisheni. Nilishangazwa sana na utanashati na mwonekano mzima wa uwanja wa JKT na hasa eneo la kuchezea. Tofauti na msimu uliopita,uwanja ulikuwa na alama zote zinaonekana, mpira unatembea na wachezaji hawapati tabu kukimbia uwanjani.Pia niliona kazi inayoendelea ya utengenezaji wa sehemu ya kukalia.Uwanja unavutia kweli.

Ukiona vyaelea vimeundwa,hali ya uwanja wa Mbweni na viwanja vingine ni matokeo ya juhudi kubwa ya Bodi ya Ligi (TPLB) kwa kushirikiana na wadau ambao ni wamiliki, klabu zinazotumia viwanja na mdhamini mwenye haki za matangazo ya mpira, yaani Azam Media. Mara nyingi tumesikia Bodi ya Ligi ikiviwekea vikwazo (kuvifungia) viwanja vinavyoonekana kutokidhi sifa za kuchezewa michezo ya Ligi Kuu, wakati mwingine hata Ligi ya Championship. Hatua hizi,wakati mwingine,ziliwaletea bodi hiyo na TFF lawama lakini wao walijua wanachokifanya, matokeo sasa yanaonekana.

Sheria nambari moja ya mpira wa miguu inasisitiza kuhusu hali ya uwanja kwa ajili ya kurahisisha tafsiri ya sheria, kutembea kwa mpira na usalama wa wachezaji. Kuanzia miaka ya 1990, mahitaji ya viwanja vizuri yamekuzwa na mahitaji ya kibiashara ya picha nzuri kwa vituo vya televisheni.Ikumbukwe kwamba matangazo ya televisheni ni moja ya vyanzo vikubwa sana vya mapato ya mpira wa miguu.Televisheni zenye haki ya matangazo zingependa kuwafikishia watazamaji wao bidhaa inayoonekana kiuhalisia pengine hata zaidi ya mtu aliyekwenda uwanjani.Hapa nyumbani, kuwepo kwa Azam Media kama mdhamini wa matangazo zaidi ya miaka 10 sasa, kumechangia katika mapinduzi ya ubora wa viwanja.

Azam kama wadhamini,wamekwenda hatua zaidi, hata wakadiriki kuingia gharama za nje ya mkataba wao kwa kuweka taa kwenye viwanja kama Mkwakwani, Kaitaba na Majaliwa ili viwanja hivyo viweze kutumika pia wakati wa usiku. Hii imewezesha michezo mingi kuonyeshwa mubashara lakini pia imeleta uwezekano wa uwanja mmoja kuweza kutumika hata kwa michezo miwili katika siku moja.

Pamoja na kwamba bado kuna viwanja vingi ambavyo tunaweza kusema vina viwango vya mchangani,lakini hatua kubwa imepigwa na haishangazi kwamba uwepo wa viwanja vizuri umechangia pia kupanda kwa viwango vya ligi kuu na kuiweka miongoni mwa ligi za juu barani Afrika.

Matumaini ni makubwa kwamba juhudi za TPLB, kamati ya TFF ya leseni za klabu, wamiliki wa viwanja na wadau wengine zikiendelea,viwanja vitakuwa vitovu vya maendeleo ya michezo. Viwanja vizuri vitavutia mashabiki viwanjani na kuingiza kipato kwa wamiliki ,vilabu,sekta ya michezo na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kidogo kidogo tunashuhudia vilabu kutoka mataifa mengine na hata timu za taifa wakiweka kambi za maandalizi hapa nchini na pia kucheza michezo yao ya kirafiki na ya mashindano. Hili ni jambo jema na chanya kwa maendeleo ya michezo na utalii wa michezo. Uchumi wan chi utafaidika pia na mwelekeo huu.

Serikali ya awamu ya sita imeondoa kodi katika uagizaji wa vifaa vya miundombinu ya michezo kama vile nyasi bandia. Huko nyuma tulipata wakati mgumu sana kuingiza vifaa hivyo hata katika miradi iliyokuwa chini ya ufadhili wa FIFA. Bila shaka hata wahisani watatiwa moyo kusaidia miradi ya miundombinu ya viwanja. Hii ni fursa nzuri ya kuviweka viwanja vyetu katika hali timamu na mwonekano mzuri.

Jambo jingine linaloonyesha kuwa bodi ya ligi imedhamiria kuendeleza miundombinu ya mpira ni uwepo wa Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja. Tuzo hii hutolewa kila mwezi kwa meneja wa uwanja wa uwanja unaotumika kwa ligi kuu ambaye kazi yake imeonyesha ubora kwa mwezi unaohusika. Pia katika tuzo za msimu, iko tuzo ya meneja bora wa uwanja.

Huu ni wakati muafaka wa kuzidi kuwakumbusha wamiliki na ikiwezekana kuwafundisha umuhimu na jinsi ya kutunza viwanja. Kozi mbalimbali na mafunzo ya vitendo kwa watunza viwanja (Groundsmen) zitasaidia katika kuhakikisha mafanikio haya yanakuwa endelevu.

 Nitaumia sana ikiwa ifikapo mwezi Mei 2025 Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo utakuwa kwenye hali mbaya kama ulivyokuwa mwisho wa msimu uliopita. Utunzaji mzuri wa viwanja utawezesha mpira kuchezeka vizuri lakini pia utaokoa fedha kwa vilabu kutokwenda mbali kutafuta viwanja vinavyokubalika katika mashindano husika.

Wazidi kufanya vizuri na kutopepesa macho katika kuchukua hatua ikiwemo vikwazo vya kufungiwa kwa viwanja visivyokidhi viwango stahiki.Katika mchezo wa mpira wa miguu,uwanja ni hitaji la kwanza hata kabla ya mpira wa kuchezea na ndiyo maana sheria ya kwanza katika sheria 17 za mpira ni sheria ya uwanja.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.