NIONAVYO: Mpira wa mdomoni unauponza mpira wa uwanjani
Muktasari:
- Sijapata nafasi ya kuongea na Kasongo kujua kama alichokusudia kimefanikiwa au ni mpango gani alionao kuhakikisha klabu na maofisa wake wanaachana na sanaa ya uchekeshaji.
MWANZONI mwa msimu wa Ligi Kuu Bara, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPBL), Almas Kasongo alinukuliwa akisema kwamba katika msimu huu bodi hiyo haitawavumilia wasemaji wa klabu ambao ni wachekeshaji (comedians).
Sijapata nafasi ya kuongea na Kasongo kujua kama alichokusudia kimefanikiwa au ni mpango gani alionao kuhakikisha klabu na maofisa wake wanaachana na sanaa ya uchekeshaji.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilikuwa limekuja na mradi wa club licensing au leseni za klabu ambao ulikuwa ni mkakati wa kuhakikisha taasisi za mchezo wa mpira wa miguu zinakuwa na taswira chanya mbele ya umma na pia zinakuwa na uwazi ili wawekezaji ambao ni mashabiki, wanachama, wabia na wadau wengine kama kampuni waone rasilimali zinazoingia katika klabu na faida yake. Walitaka umma ujue kinachoendelea ndani ya klabu.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilianza vizuri na suala la klabu kuwa na maofisa habari waliofunzwa na wenye weledi.
Semina nyingi zilifanyika na sasa zinafanyika kuhakikisha kuwa vitengo vya habari vya klabu zinaleta tija iliyokusudiwa kwa klabu husika na mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla.
Ghafla katika miaka ya hivi karibuni suala la weledi katika vitengo vya habari vya klabu likawa kama limetoweka. Kwa uwazi kabisa niseme kuwa tatizo hili hasa lilianzia na liko zaidi kwenye klabu za Simba na Yanga.
Kunaweza kuwa na matatizo sehemu nyingine lakini hayaonekani sana kama yale ya Simba na Yanga.
Na klabu hizi ndiyo zimeipa hadhi ligi yetu na mpira wetu, ndizo taswira ya mpira wa Tanzania.
Klabu za Yanga na Simba zimefanikiwa kufanya vizuri kimataifa katika miaka ya karibuni. Kwa mpira wa sasa, kufanya vizuri uwanjani kunategemewa kulete uwekezaji katika klabu husika. Na kusema ukweli siku hizi mpira wa miguu una pesa nzuri pale timu inapofanya vizuri.
Hata hivyo, kufanya vizuri tu uwanjani hakuwezi kumsukuma mtu kuandika hundi ya udhamini kwa klabu yako.
Huu ni ulimwengu wa nipe nikupe. Wawekezaji hawatoi pesa kwa timu kufanya vizuri, la muhimu kwao ni timu iwatangaze kwa taswira chanya.
Hivi karibuni kumekuwa na habari za mdhamini mvalishaji wa klabu ya Simba kutoa barua ya kusudio la kumburuta mbele ya vyombo vya sheria ofisa habari wa klabu ya Yanga kwa tuhuma za kudharau au kudhalilisha bidhaa anazowavalisha Simba.
Kama hiyo haitoshi, Yanga nayo ikaja na madai mengine ya kudhalilishwa na Ofisa Habari wa klabu ya Simba. Nimeona na nyingine japo sijathibitisha, ya Azam kuwa na kusudio la mtindo uleule dhidi ya ofisa habari wa klabu ya Yanga. Vyovyote itakavyokuwa, huu ni ushahidi kwamba klabu na mamlaka za mpira zimeshindwa kudhibiti vitendo vya maofisa habari.
Matokeo yake ni nini? Matokeo yake ni kuchafuka kwa mchezo wa mpira wa miguu na kurudisha nyuma maendeleo ya taasisi za mpira wa miguu.
Mpira wa miguu ni sekta muhimu ya kibiashara. Katika ulimwengu wa sasa, michezo sio michezo tena. Michezo ni uchumi. Inasikitisha sana kampuni zinawekeza pesa nyingi sana katika klabu ya Yanga lakini muda mwingi wa matamshi ya idara ya habari ya Yanga ni kuwapiga vijembe Simba. Ofisa Habari wa Simba vivyo hivyo, muda wake mwingi ni kuongelea Yanga kuliko bidhaa za mdhamini.
Kadhia anayoipata mvalishaji wa Simba, Sandaland ni matokeo ya kudekezwa kwa vitengo vya habari vya klabu hizo mbili.
Kuna wakati najiuliza ikiwa hawa watoa habari ambao wamekuwa wasema chochote walipewa hadidu za rejea wakati wanaajiriwa. Au waliambiwa ingia uwanjani ucheze utakavyoona? Mchezo wa mpira wa miguu una sifa ya kuchezeshwa kwa kanuni na taratibu; inakuwaje vitengo muhimu vya kuiunganisha klabu na umma havina kanuni na taratibu? Viongozi wa klabu husika wanafurahia hiki kinachoendelea?
Ni wangapi wanamjua Toby Craig, Ofisa Mkuu wa Habari na Masoko wa Manchester United? Wala hasikiki lakini anafanya kazi ya kuifanya nembo ya Manchester United iongezeke thamani hata kama pale uwanjani mpira umeshuka.
Craig havumi, pamoja na uzoefu wa kuendesha habari na masoko katika klabu za Manchester City, Chelsea na Manchester United. Unamjua Bi Kate Laurens wa Arsenal? Au Bi Susan Black wa Liverpool? Hawa wote ni weledi wa kiwango cha kimataifa lakini huwasikii wakitoa neno lisilokusudiwa na klabu. Neno la mtumishi wa taasisi linatafsiriwa kuwa msimamo wa taasisi.
Kazi ya kitengo cha habari ni kutoa taarifa za utendaji wa klabu kama taasisi kadri inavyohitajika. Masuala ya uwanjani, msemaji wake ni kocha na wala si ofisa wa kitengo cha habari.
Ni wakati sasa klabu zinatakiwa kuwapa hadidu za rejea maofisa habari wake na kuhakikisha kuwa wanazifuata. Ofisa habari aweze kukusanya habari, kuhakiki habari, kusambaza habari kwa usahihi, kwa wakati na kwa uwazi.
Taasisi zinazokwenda kufanikiwa katika nyakati hizi ni taasisi zitakazoweza kuwafikia wadau wengi duniani kwa taarifa nzuri na za kuvutia lakini zaidi za kueleweka. Klabu zinapaswa kujitangaza kama chapa za kibiashara na kuelewa kwamba chapa hiyo haiuzwi tu nyumbani bali pembe nne za dunia. Kuweza kufanikisha hili, ni muhimu kufanya uwekezaji katika rasilimali watu na teknolojia katika vitengo vyao vya habari na kuhakikisha nidhamu katika upashaji wa habari.
Wanasema mdomo uliponza kichwa. Hakuna jinsi nyingine ya kuuona mwelekeo wa taasisi zaidi ya kinachoandikwa na kutamkwa na wasemaji wa taasisi. TFF na klabu wajue dunia itapima na kuhukumu mpira wa Tanzania kupitia midomo misafi au michafu ya maofisa wa habari.
Ikiwa kuna ulazima wa kuendeleza utani wa jadi wa Yanga na Simba kupitia wasema chochote na wasema hovyo, basi klabu ziunge mkono vikundi vya sanaa na hamasa vya mashabiki lakini si kujichafua kupitia maofisa habari. Kinachotokea sasa kati ya Sandaland na Ally Kamwe, Yanga na Ahmed Ally na mengine ni maandishi ukutani kwa wahusika kusoma hatari ijayo.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.