Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Makocha Wetu Waamke au Waamshwe?

Nionavyo Pict

Muktasari:

  • Ramovic amecheza mechi 6 za kimataifa na Yanga akiwa na rekodi ya kushinda 2 kutoka sare 2 na kufungwa 2. Ghafla Ramovic amekuwa nyota kupitia jukwaa la Yanga. Hadithi ni ileile kwa watangulizi wake Gamondi na Nassredin Nabi.

KLABU ya Yanga imeachana na kocha raia wa Ujerumani, Sead Ramovic kwa makubaliano ya pande mbili. Habari hii imeghubika vyombo vya habari vya hapa nchini na pia hat nje ya nchi.

Ikumbukwe kuwa, Ramovic alijiunga na Yanga kuchukua mikoba ya raia wa Argentina, Miguel Gamondi huku timu hiyo ikiwa inamalizia raundi ya kwanza ya Ligi Kuu na pia akaiongoza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako Yanga ilishindwa kuvuka kwenda robo fainali.

Inasemekana Ramovic na msaidizi wake wamepewa donge nono na klabu ya CR Belouzidad ya Algeria ikiwa ni pamoja na fidia ya uvunjaji mkataba kwa Yanga ambayo haikuwekwa wazi.

Awali mtangulizi wa Ramovic, yani Gamondi alisajiliwa na Al Itihad ya Libya inayosemekana kuwa na mikoba mikubwa ya fedha.

N 01

Yanga wamemtangaza aliyekuwa kocha wa Singida BS pia ya Ligi Kuu, Miloud Hamdi ambaye ni raia wa Algeria kuchukua mikoba ya Ramovic.

Katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KenGold, kocha msaidizi Amoallin raia wa Marekani ambaye Yanga walimchukua kutoka KMC ndiye aliongoza benchi la ufundi wakati Hamdi akiwa jukwaani. Upande wa KenGold katika benchi alikaa mzawa, Omar Kapilima wakati jukwaani akiwepo kocha mpya wa klabu hiyo Vladislav Heric ambaye anasubiri vibali vya kazi.

Kwa muda mrefu Yanga hawakuwa na tabia ya kubadilisha makocha sana ndani ya msimu mmoja. Sasa wana kocha wa tatu na msimu uko katikati; tusubiri tuone.

Mabadiliko ya makocha kwa klabu za juu katika Ligi Kuu kama Simba Yanga, Azam, Singida na nyingine kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni ya wageni kuchukua nafasi za wageni; anaondoka kocha wa kigeni anaingia kocha wa kigeni.

Ni wazawa wachache sasa wana uhakika wa kukaa kwenye nafasi ya kocha mkuu katika klabu za Ligi Kuu.

N 05

Bado haijaniingia akilini kwamba hata klabu za ligi za chini zimeingia katika mtazamo huo wa kuajiri makocha kutoka nje ya nchi. Na ukweli ni kwamba makocha wa kigeni ni ghali sana na wengi huja na jopo lao la makocha kama vile wa makipa, wa viungo na hata wachambuzi wa video.

Kinachoshangaza,Tanzania ni moja ya nchi zenye makocha wengi wenye vyeti vya juu vya CAF. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefanya juhudi kubwa kusomesha makocha ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza mpira wa miguu na pia kuweza kufikia matakwa ya kikanuni ya ligi inayotaka makocha wa klabu za Ligi Kuu kuwa na angalau Leseni A ya CAF.

Makocha wengi wamechangamkia hizi kozi, lakini la ajabu si wengi wanaoonekana kuajiriwa. Hapa sielewi kwamba makocha hawaajiriwi au hawaajiriki.

N 04
N 04

Wakati makocha wa Ulaya, Afrika ya Kaskazini, Afrika ya Kusini na hata majirani zetu Burundi na Kenya wanafurika hapa, sisi hatuna kocha anayesikika hata kufundisha nje ya nchi.

Hapa la kujiuliza ni je makocha wanaangushwa au wanajiangusha au wameridhika. Unajiuliza hivi vyeti vya Daraja la juu wanavyovisomea ni kwa ajili ya nini?

Ni ukweli usiopingika kwamba si makocha wote wanaweza kupata nafasi katika klabu kubwa, lakini haiji kabisa akilini kwamba tuna makocha ambao wako tayari kutoka katika nafasi ya kocha mkuu wa klabu A ya Ligi Kuu na kwenda kuwa kocha msaidizi au hata kocha namba 3 katika klabu B.

Kocha wa timu ya taifa anachukuliwa na klabu kama kocha msaidizi;inaingia akilini kweli?

N 03

Tatizo letu liko wapi? Je ni kwa sababu makocha wetu hawana wakala na hawajui namna ya kupata wakala? Kama shida ni hiyo kweli tujiulize wenzetu wa Burundi, Malawi, Kenya, Uganda n.k wanapata wapi mawakala? Je shida ni lugha? Hapana, makocha wetu wanafundishwa kozi za juu kwa kizungu na pia hata hawa makocha wa kigeni wanaokuja hapa miongoni mwao kuna wasioweza kutengeneza sentensi moja ya Kiingereza au Kiswahili kilichonyooka, lakini bado wanaweza kufanya kazi hapa hata kama ni kwa kutumia wakalimani.

Unajiuliza kiko wapi kizazi cha kina Abdallah Kibadeni, Mansour Magram, Paul West Gwivaha, Zakaria Kinanda, Sunday Kayuni, Syllersaid Mziray na wengine waliokuwa wakifundisha na kufanya vizuri ndani na nje?

Haishangazi watu wanapotilia shaka uwezo wa makocha wa timu za taifa. Haishangazi watu wanapotamani timu za taifa kufundishwa na makocha wa kigeni. Watanzania hawaoni kocha mzawa anayefanya vizuri kwenye mpira wa klabu ambao unafuatiliwa sana.

Watanzania wanajiuliza iweje hawa makocha ambao hawawezi kukaa katika benchi la Yanga, Simba, Tabora United n.k waweze kufundisha timu ya taifa kwa mafanikio? Mbona kina Sunday Kayuni, Denis Kitambi, Dan Korosso na hata Juma Pondamali waliwahi kwenda kufundisha soka Botswana na Kenya, wengine wanakwamia wapi? Naona ni fursa ya makocha wazawa kuona wivu kwa wageni kukimbilia Tanzania, wakati wao wanashindwa kwenda hata kwa majirani kwetu tu!

N 02

Hivi karibuni, Ligi Kuu Bara imetajwa kuwa Ligi ya 4 kwa ubora Afrika, huku Yanga na Simba zikiwa kwenye timu 15 bora barani Afrika. Hii  ni nafasi kwa wachezaji na wataalamu wa mabenchi ya ufundi kwenye klabu za ligi kuu kuonekana na kupata kandarasi kimataifa. Kama makocha wetu wanakuwa si sehemu ya mabenchi ya ufundi ya timu zinazowakilisha nchi wataonekana saa ngapi? Tuchukue mfano wa kocha Ramovic ambaye amekaa na Yanga chini ya miezi 3 baada ya kuchukuliwa kutoka timu ndogo ya TS Galaxy inayocheza ligi ya Afrika ya Kusini (PSL).

Ramovic amecheza mechi 6 za kimataifa na Yanga akiwa na rekodi ya kushinda 2 kutoka sare 2 na kufungwa 2. Ghafla Ramovic amekuwa nyota kupitia jukwaa la Yanga. Hadithi ni ileile kwa watangulizi wake Gamondi na Nassredin Nabi.

Umefika wakati TFF iangalie kanuni zake ili kuwapatia baadhi ya nafasi kama za kocha msaidizi kwa makocha wazawa ili wanapokuja makocha wa kigeni wenye ujuzi mkubwa waache sehemu ya ujuzi huo nchini.Pia TFF iangalie ni wapi mapungufu yalipo ili kasi na uhitaji wa maendeleo ya mpira usiwaache nyuma makocha.

Makocha wazawa watie juhudi kwenye kujiendeleza kwa kozi mbalimbali hata zile zilizo nje ya mfumo wa TFF na CAF kama zile za Uefa.Pia makocha watafute mawakala wa kuweza kuwaunganisha na klabu mbalimbali duniani.Makocha wetu watume maombi kwenye klabu mbalimbali hata za nchi Jirani labda nabii hakubaliki nyumbani wanaweza kufanikiwa.

Ni wakati muafaka sasa kwa TFF,Chama cha makocha TAFCA,makocha na wadau wote wa maendeleo ya soka nchini kuangalia namna nzuri ya kuendeleza na kuwatumia makocha wazawa.


Mwandishi wa Makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).Unaweza kutuma maoni yako kupitia namba yake hapo juu.