Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Kombe la Dunia 2030 litafanyika angani

BARAZA linaloongoza Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) limepitisha Kombe la Dunia la Mwaka 2030 kufanyika katika mataifa sita na mabara matatu, huku kwa mara ya kwanza mataifa sita yakienda moja kwa moja kucheza Fainali za Kombe la Dunia.

Michezo mitatu ya kwanza itafanyika Uruguay, Argentina na Paraguay huku michezo iliyobaki ikienda kwa waandaaji wa pamoja Morocco, Hispania na Ureno.

Hili sio jambo la kawaida katika mashindano yenye historia ndefu na ambayo kwa miaka mingi hayakuwa na mabadiliko makubwa kama haya. Baraza la Fifa linasema kuwa ilikuwa ni muhimu kusherehekea karne moja ya Kombe la Dunia (miaka 100) kwa kupeleka mchezo mmoja kwenye Uwanja wa Centenario ulioko Montevideo, Uruguay ambako mashindano ya kwanza yalifanyika mwaka 1930 na taifa hilo kubeba taji.

Mabingwa wa sasa wa fainali hizo, Argentina watapata mchezo mmoja kwenye ardhi yao, huku Paraguay yaliko makao ya Shirikisho la Vyama vya Soka vya Amerika ya Kusini (Conmebol) ukichezwa mchezo mmoja.

Hata uenyeji wa mataifa matatu kutoka mabara mawili tofauti sio jambo la kawaida katika utamaduni wa Kombe la Dunia. Pamoja na kwamba Morocco iliyoko Afrika haiko mbali na Ureno na Hispania zilizoko Ulaya, bado utamaduni wa Kombe la Dunia ilikuwa ni kila bara kuwa na zamu yake.

Wachambuzi wa matukio wanaona kama Morocco, ambayo iliomba na kukosa uenyeji wa 2026 (ilipopigwa kumbo na maombi ya Marekani, Canada na Mexico imeuza zamu ya Afrika. Baraza la Fifa limeshakutangaza kuwa zamu ya Afrika na Ulaya itakuwa imepita hivyo maombi yatakayopokewa ni ya Asia na Oceania ambako Saudi Arabia na Australia zinapewa nafasi ya kuomba kuandaa.

Ukweli ni kwamba tangu Gianni Infantino imeingia madarakani amejaribu kufanya mabadiliko mengi na kulifanya Kombe la Dunia na hata Fifa iende kinyume cha utamaduni wake.

Wachambuzi na wanaharakati wa soka hasa Kombe la Dunia wanayaona mabadiliko haya kama yanayoua hadhi ya mashindano hayo makubwa duniani. Yanaonekana kama ni mabadiliko yanayolenga kuimarisha nafasi ya Infantino katika kiti cha utawala kuliko kuimarisha mpira wenyewe.

Dunia inajua wazi vita kubwa zilizokuwapo huko nyuma hasa linapokuja suala la kupata mwenyeji wa Kombe la Dunia.

Uenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2006 ulizipambanisha Ujerumani na Afrika ya Kusini kiasi cha kuchukua sura ya kisiasa.

Baada ya Afrika Kusini kufanyiwa mizengwe na kukosa mbele ya Ujerumani ilikuwa ni muhimu sana kwa Rais Sepp Blatter kuhakikisha Afrika iliyokuwa inampa kura nyingi inaandaa Kombe la Dunia 2010 na ikawa hivyo.

Gianni Infantino anajua wazi kwamba anguko la mtangulizi wake, Blatter lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na nchi za Russia na Qatar kupewa Fainali za Kombe la Dunia mbele ya England na Marekani. Wachambuzi wanachukulia kuwa hata uenyeji wa Marekani wa 2026 ulitolewa kama namna ya kutuliza hasira za taifa hilo mwenyeji wa Kombe la Dunia la 1994.

Hivyo kinachofanyika ni kumwonjesha kidogo kila mwombaji na kuridhia maslahi mengine ya mashirikisho yanayounda Fifa.

Mfano mzuri wa namna maslahi yalivyozingatiwa ni pale nchi za Argentina, Chile, Paraguay na Uruguay ambazo ni wanachama wa Conmebol ziliomba uenyeji na kunyimwa, lakini shirikisho hilo limepewa michezo mitatu ya Argentina, Paraguay na Uruguay hivyo litakaa kimya na zamu yao itapita.

Mfano mwingine ni Ulaya (Uefa) ambayo kupitia Urusi (Russia 2018) iliandaa mashindano hayo karibuni, hivyo zamu yao ingekuwa mbali lakini wakajifungamanisha na Morocco ambayo ilikosa maombi ya 2026 hivyo kuridhishwa kwa kupewa uenyeji wenza na kuiridhisha Afrika (CAF) ambayo mara ya mwisho iliandaa mwaka 2010.

Hivyo Conmebol wana furaha, Uefa wana furaha, CAF wana furaha na Infantino ana furaha zaidi. Hizo ndizo siasa za mpira.

Maandalizi ya pamoja ya Kombe la Dunia yalianza miaka 21 iliyopita pale mataifa ya Japan na Korea Kusini yalipoandaa kwa ushirikiiano Fainali za Dunia za 2002. Kwa kufanya hivyo mataifa yote mawili yaliingiza timu zao moja kwa moja huku Korea Kusini ikiibuka taifa la kwanza la bara Asia kufika robo fainali za michuano hiyo.

Maandalizi ya pamoja hufanya maombi kuweza kupita kwani mataifa yanaweza kugawana majukumu. Hata hivyo Kombe la Dunia la mwaka 2030 litahitaji uratibu wa hali ya juu na bila shaka litahitaji fedha nyingi kwa upande wa Fifa na timu shiriki kuweza kuyafanya yenye mafanikio.

Miundombinu ya michezo katika mataifa sita wenyeji si tatizo. kwa nyakati tofauti yote yamewahi kuandaa mashindano makubwa. Hata hivyo, umbali na mifumo tofauti ya uhamiaji na kodi inaweza kuwa usumbufu kwa waandaaji na mashabiki pia. Kwa mfano umbali kutoka Paraguay hadi Morocco ni kilometa 8200 ambayo ni saa kama 10 kwa usafiri wa ndege.

Morocco ndio taifa pekee la Afrika lenye mpaka wa ardhi na Ulaya na hata kwenye mpaka wa maji Morocco iko kilometa 12 kutoka Hispania, lakini kwa usafiri wa ndege za kimataifa wako umbali wa kilometa karibu 1000. Kumbuka pia, raia wa Morocco wanahitaji viza kuingia Hispania. Kwa maana nyingine kuanzia kwa Infantino na waandaaji walioko Zurich watahitaji kusafiri kilometa zaidi ya 11,000 (zaidi ya saa 12) kwenda Montevideo kusherehekea Miaka 100 ya Fifa kisha kusafiri kilometa 10,000 (zaidi ya masaa 11) kwenda Madrid na kisha kilometa 950 (zaidi ya saa 1) kwenda Afrika (Morocco).

Hali hiyo itazikabili pia timu zitakazoshiriki fainali hizo za mwaka 2030. Muda wao mwingi utatumika angani, yaani kutoka nyumbani kwao kwenda kambini na kwenda kwenye vituo vya michezo yao.

Pamoja na nia za wazi na za nyuma ya pazia za kuandaa Kombe la Dunia kwa mabara matatu na mataifa sita, Fifa na mataifa wenyeji watakuwa na kazi ya kupanda mlima kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika na Kombe la Dunia halipotezi hadhi kama mashindano makubwa kabisa ya soka duniani.

Je, huu ni uamuzi wa busara? Tusubiri tuone.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.