Prime
Anko Mafiksi; Alizika mgomba kisa mapenzi
PENZI likiwa zito linaweza likakupa upofu, ukawa huambiwi wala kusikia la mtu. Kwa kifupi, penzi halibagui watu maarufu ama wa kawaida, ukipitia hali hiyo unaweza ukakosana na ndugu ama marafiki kama watajaribu kukushauri jambo hadi pale ufahamu wa kawaida utakapokukaa sawa bila kutumia hisia.
Nyuma ya Kamera awamu hii imepiga stori na mchekeshaji maarufu nchini, Anko Mafiksi ambaye jina lake halisi anajulikana kama Idriss Shabani Amanzi, mzaliwa wa Ifakara Mjini, Mwembe Tokwa alimaarufu kwa Mkwawa mkoani Morogoro.
Jamaa amepitia vioja katika mapenzi, vitakavyokuacha mdomo wazi na kukufunza jambo kabla hujaingia katika mtego wa hisia kuliko kutumia akili ya kuepuga msongo wa mawazo.
Anasimulia aliwahi kufanya kitu cha ajabu ambacho akikitafakari baada ya kutumia akili timamu, hisia zikiwa zimekaa pembeni anajikuta anajishangaa.
Anasema alipata mwanamke mkoani Tanga, akahama kwake na kwenda kuishi ukweni ambako alikiona cha moto.
“Nilikutana na mwanamke wa kitanga ambaye maneno yake yalinigeuza kuwa mtu wa ajabu, wakati jamii ikinishangaa, mimi nilikuwa najiona nipo kwenye ulimwengu wetu wawili, alikuwa mlaghai wa maneno na vitendo, mbwa alikuwa akipita mbali akimuona anaanza kuniambia pole bebi kwa kelele za mbwa, basi nikawa najiona kidume si mimi sasa,” anasema Anko Mafiksi na kuongeza;
“Kwa kuwa nilikuwa sina pesa, ili kuonekana kidume nikawa napasua kuni na kuchota maji, kila siku, nikimaliza anaenda kunipashia maji anaweka na hiriki, halafu nikioga anakuja kunipaka mafuta mwilini na kuniambia maji hayajakuunguza bebi, ila nikipasua mikuni na kubeba midumu haongei chochote.
“Kubwa zaidi walikuwa na mgonjwa alikuwa kibonge sana, hivyo kazi yangu ilikuwa ni kumuogesha, kumbeba kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kuna wakati nilikuwa najiona nisije nikatia aibu, nikajikuta naanguka mimi, hivyo nilikuwa nasubiria nishibe ili niwe na nguvu, kusema ukweli nilikoma.
“Ilikuwa ikitokea nikimpiga mwanamke wangu familia nzima inakuja kunichangia kunichapa kwa kipigo kizito, halafu wananiambia ulilewa utakuwa ulianguka ndiyo maana umeumia, wakati sijanywa pombe, alikuwepo shemeji yangu alikuwa anaitwa Costa, nikifanya kazi ananiachia ngumu, halafu ugomvi ukitokea ndiye wa kwanza kunipiga, kifupi ni kama niliolewa.”
Kilichokuja kumng’oa kwenye penzi hilo, anaelezea mwanamke alipata mwanaume anayefanya kazi Tanesco, hivyo akawa anamsaliti waziwazi pamoja na hilo akawa anavumilia, lakini ilipofikia hatua ya ndugu kumwambia waziwazi alihisi maumivu makali hadi akafanya kitendo cha kustajabisha cha kiimani.
“Alimchagua mwenye pesa akaniacha maskini, iliniumiza sana, nilichokifanya nikarudi shambani kwangu nikachimba shimo, nikakata mgomba na kuuzika nikiusemea maneno kwamba nisimkumbuke tena wala kumuwaza maishani mwangu, baada ya hapo nikasahau na kuendelea na maisha yangu, niliachwa kwa umaskini siyo mambo mengine ya ndani, lakini kwa sasa nimepata penzi jipya, ni mwanamke wa Ifakara, naomba Mungu nizeeke naye,” anasema Mafiksi.
KWANINI ANAIGIZA MAPENZI
Anasema ametokea familia ambayo bibi ni kungwi na babu yake ni ngariba, hiyo ni sababu kubwa inayofanywa aigize ishu za mapenzi, akisisitiza anayajua kindakindaki ndiyo maana akipenda anakuwa king’ang’anizi.
“Nimefanya kazi ya ungariba kwa takribani miaka mitano katika mikoa ya Singida, Dodoma na Manyara, baada ya serikali kutoa elimu nikaacha pia nilikuwa naona huruma. Ukiachana na hilo, nimefunda sana wanawake ili kujua namna ya kuthamini ndoa,” anasema Anko Mafiksi na kuongeza;
“Wanawake wengi hawajui kutumia vizuri ndimi zao, ujue mwanaume anarogwa kwa maneno na siyo dawa, ukimuongelesha vizuri unapewa hati ya nyumba, sasa wanawake wengine wa ajabu wanaomba pesa utadhani mgambo, mbali na wanawake pia nawafunda wanaume baadhi yao wamekuwa wajinga wakisimuliana mambo ya ndani vijiweni, huo ni ushamba, ya chumbani yabakie chumbani.”