Wakongwe wanaokiwasha WAFCON 2026
Muktasari:
- Baadhi yao wamekuwa kwenye timu za taifa kwa zaidi ya muongo mmoja, wamecheza matoleo kadhaa ya mashindano haya na wengine wamebeba mataji au kufikisha mataifa yao kwenye hatua ambazo hazikuwahi kufika.
WAKATI nyota chipukizi wakiendelea kung’ara katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 nchini Morocco, bado kuna kizazi cha wakongwe ambao umri haujawazuia kuendelea kuwa sehemu ya mipango ya mataifa yao.
Baadhi yao wamekuwa kwenye timu za taifa kwa zaidi ya muongo mmoja, wamecheza matoleo kadhaa ya mashindano haya na wengine wamebeba mataji au kufikisha mataifa yao kwenye hatua ambazo hazikuwahi kufika.
GHIZLANE CHEBBAK
Morocco inaongozwa na mmoja wa wachezaji wenye historia kubwa katika soka la wanawake Afrika, Ghizlane Chebbak, ambaye alianza kuitumikia timu ya taifa mwaka 2007. Akiwa nahodha na kiungo mshambuliaji, Chebbak amekuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya Morocco kutoka timu iliyokuwa ikipambana kupata nafasi kwenye soka la Afrika hadi kuwa moja ya timu zinazowania ubingwa.
Mchango wake mkubwa kwenye WAFCON. mwaka 2022, Chebbak aliiongoza Morocco kufika fainali kwa mara ya kwanza katika historia, huku akifunga mabao matatu katika mashindano hayo.
Morocco ilipoteza fainali 2-1 dhidi ya Afrika Kusini, lakini nafasi hiyo ilitosha kuwapa wenyeji tiketi ya kucheza Kombe la Dunia 2023, ikiwa ni mara yao ya kwanza kufuzu.
Katika WAFCON 2024, Chebbak alifunga mabao matano kwenye mechi sita na kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa mashindano.
Yupo kwenye WAFCON kama mchezaji ambaye tayari ameonyesha uwezo wa kuamua matokeo makubwa. CAF ilimtaja akiwa na umri wa miaka 35 kama moyo wa timu ya Morocco, ikisisitiza uwezo wake wa kudhibiti kasi ya mchezo, ubunifu na uzoefu wake wa kutengeneza nafasi na kuzitumia kufunga.
ASISAT OSHOALA
Mshambuliaji huyo wa Nigeria amekuwa kwenye kikosi cha Super Falcons kwa miaka mingi na amekuwa sehemu ya mafanikio ya taifa hilo katika mashindano makubwa.
Oshoala aling’ara WAFCON kwa mara ya kwanza mwaka 2014, wakati Nigeria ilipotwaa ubingwa wa Afrika, na miaka miwili baadaye akawa mfungaji bora wa WAFCON 2016.
Katika WAFCON 2024 alifunga bao dhidi ya Tunisia na kufikisha mabao 14 katika historia ya WAFCON, huku bao hilo likiwa la nne kwake katika matoleo tofauti ya mashindano hayo.
Kwa upande wa tuzo binafsi, Oshoala ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika mara sita, rekodi ya kipekee katika tuzo za CAF. Amechukua tuzo hiyo mwaka 2014, 2016, 2017, 2019, 2022 na 2023.
Oshoala pia ameandika historia Ulaya akiwa Barcelona, ambako alifunga mabao 85 katika mechi 101 za ligi kwa mujibu wa takwimu zilizorekodiwa za klabu.
GABRIELLE ONGUENE
Onguene ni mfano wa mchezaji ambaye amedumu kwa muda mrefu bila kupoteza nafasi yake kwenye kizazi kipya.
Alianza kuitumikia timu ya taifa takribani miaka 16 iliyopita na WAFCON 2026 imekuwa mara yake ya nane kushiriki mashindano hayo.
Mchango wake mkubwa katika historia ya Cameroon ulionekana WAFCON 2016, wakati Indomitable Lionesses ilipofika fainali. Onguene alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano hayo, lakini Cameroon ilipoteza fainali dhidi ya Nigeria.
Kinachomtofautisha Onguene na baadhi ya wakongwe wengine ni kwamba licha ya kucheza mashindano mengi, bado yupo kwenye mashindano akiwa na kiu ya taji ambalo amekuwa akilishihidia likienda kwa Nigeria na timj zingine.
REFILOE JANE
Afrika Kusini nayo ina mkongwe wake, Refiloe Jane, ambaye alianza kucheza timu ya taifa mwaka 2012. Kiungo huyo amekuwa sehemu ya safari ya Banyana Banyana kwa zaidi ya muongo mmoja na amekuwa miongoni mwa viongozi wa timu hiyo.
Jane alikuwa sehemu ya kikosi kilichofanya historia WAFCON 2022, wakati Afrika Kusini ilipotwaa ubingwa wa Afrika kwa mara ya kwanza. Baada ya kufika fainali mwaka 2018 na kupoteza dhidi ya Nigeria, Banyana Banyana ilirudi mwaka 2022 na kuifunga Morocco 2-1 katika fainali mjini Rabat, ikatwaa taji lake la kwanza.
Akiwa na uzi wa Afrika Kusini Jane amecheza zaidi ya mechi 100 za kimataifa, huku rekodi zilizosasishwa zikimuweka kwenye orodha ya wachezaji waliocheza zaidi kwa Afrika Kusini. Takwimu hizo zinamfanya kuwa mmoja wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa zaidi katika kikosi cha sasa.
Umuhimu wake haukuishia kwenye idadi ya mechi. Jane amekuwa kiungo anayesaidia timu kudhibiti mchezo na amekuwa sehemu ya kizazi kilichobadilisha Banyana Banyana kutoka timu iliyokuwa ikifika fainali bila taji hadi kuwa mabingwa wa Afrika.
RACHEL NACHULA
Nachula ni mmoja wa wachezaji wakongwe waliopitia vipindi tofauti vya ukuaji wa Shepolopolo. Nachula amekuwa sehemu ya safari ya Zambia kuelekea kuwa moja ya timu zenye nguvu katika soka la wanawake Afrika.
Mshambuliaji huyo amekuwa na uzoefu wa kucheza nje ya Zambia, ikiwa ni pamoja na Zaragoza CFF nchini Hispania ambako alicheza mechi 42 na kufunga mabao 12.
Umuhimu wake kwa Zambia ulionekana pia kwenye safari ya kufuzu WAFCON 2026. Katika hatua za kufuzu dhidi ya Namibia, Zambia ilishinda jumla ya mabao 7-2 baada ya kushinda 4-2 ugenini na 3-0 nyumbani, huku CAF ikiitaja Nachula pamoja na Racheal Kundananji kama sehemu muhimu ya safu ya mbele iliyobeba matumaini wakati Barbra Banda hakuwepo.
Hiyo ndiyo sababu uzoefu wa Nachula bado una thamani hata kama Zambia sasa ina nyota wakubwa kama Banda na Kundananji. Yeye ni miongoni mwa wachezaji waliokuwepo kabla kizazi hicho kipya hakijawa maarufu na amekuwa sehemu ya safari iliyoipeleka Zambia kutoka kuwa mshiriki wa kawaida hadi kuwa timu inayoheshimiwa Afrika.
NAJAT BADRI
Ukimtoa Chebbak Morocco inamtegemea mkongwe Najat Badri, ambaye alianza kuitumikia timu ya taifa mwaka 2007 na amekuwa sehemu ya mabadiliko ya soka la wanawake nchini humo.
Badri amekuwa mchezaji wa AS FAR kwa muda mrefu na ameshinda mataji nane ya Ligi ya Morocco na mataji sita ya Kombe la Throne. Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha AS FAR kilichotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake mwaka 2022 baada ya kuifunga Mamelodi Sundowns 4-0 katika fainali.
Kwenye timu ya taifa, Badri alikuwa sehemu ya kikosi cha Morocco kilichofika fainali ya WAFCON 2022, pia alicheza katika Kombe la Dunia 2023, ambako Morocco ilifikia hatua ya 16 bora katika ushiriki wake wa kwanza. Takwimu zinaonyesha kuwa kiungo huyo akiwa amecheza zaidi ya mechi 50 za kimataifa kwa Morocco.
WAFCON 2026 inaendelea kuonyesha ujio wa kizazi kipya haujafuta umuhimu wa wakongwe. Chebbak bado ni nahodha na mfungaji muhimu wa Morocco; Oshoala bado ana rekodi ya kipekee ya tuzo za CAF; Onguene anaingia kwenye WAFCON yake ya nane; Jane ni mmoja wa viongozi wa mabingwa Afrika Kusini; Nachula anaendelea kutoa uzoefu akiwa na Zambia, huku Badri akiwa sehemu ya kizazi kilichojenga Morocco ya sasa.
Kwa pamoja, majina haya yanawakilisha zaidi ya miaka ya kucheza soka. Yamebeba mataji, fainali, mabao, rekodi, kufuzu Kombe la Dunia na uzoefu wa mechi kubwa. Na wakati WAFCON 2026 ikiendelea, kizazi kipya kinaweza kuwa kinachukua nafasi zao taratibu, lakini kwa sasa wakongwe hao bado wana wana mchango mkubwa.