Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Everton FC na shubiri ya nidhamu ya fedha

KLABU ya Everton inayocheza katika Ligi Kuu ya England imepokwa pointi 10 na kuiporomosha kwenye msimamo wa ligi hiyo maarufu duniani.

Everton, moja ya klabu kongwe za Uingereza ikiwa imeanzishwa mwaka 1878, ilituhumiwa, ikakiri kosa na kutiwa hatiani kwa kuvuka mstari wa matumizi ya fedha (Financial Fair Play) kwa kuwa na madeni makubwa yakilinganishwa na mapato yake.

Inadaiwa, Everton ilipata hasara ya kiasi cha Pauni 371.8 milioni (zaidi ya Sh 1.8 trilioni) katika kipindi cha miaka mitatu, huku kiwango cha hasara kinachoruhusiwa ni kiasi kisichozidi Pauni 105 milioni (zaidi ya Sh335 bilioni) kwa miaka mitatu.

Kwa hatua hiyo, klabu hiyo ya viunga vya Merseyside jijini Liverpool, Kaskazini Magharibi mwa England itahitaji kufanya kazi ya ziada kujikwamua na janga la kushuka daraja.

Ikiwa mmoja wa waanzilishi wa ligi kongwe ya soka kuliko zote duniani, mara ya mwisho kwa Everton kushuka daraja ilikuwa mwaka 1954/55 kwenye ligi ya zamani, lakini hawajawahi kushuka daraja tangu EPL iundwe mwaka 1992.

Mtu anaweza kujiuliza kulikoni klabu inachukuliwa hatua kwa kutumia fedha yake yenyewe? Mathalani hapa kwetu kila siku tunasikia klabu zimenunua wachezaji, zimeajiri makocha, zimepanda ndege n.k lakini, je kuna mwenye muda wa kujua Simba wametumia kiasi gani kwa msimu au Yanga au hata timu za taasisi kama vile JKT Tanzania? Na katika mazingira yetu jambo kama hili lingetokea ingekuwaje? Mashabiki wangefanya nini? Hili ni tukio kubwa kabisa la aina yake katika historia ya Ligi Kuu ya EPL.

Ni tukio ambalo limewashtua mashabiki wa Everton kiasi cha kuchangishana fedha na kufanya maandamano na upinzani mkubwa dhidi ya taasisi ya Ligi Kuu wakiishutumu kwa ufisadi.

Maandamano makubwa yamekuwepo katika jiji la Liverpool kupinga adhabu hiyo. Ndege ilikodishwa kuruka juu ya Uwanja wa Etihad wakati wa mchezo kati ya Manchester City na Liverpool ukianza ikiwa na ujumbe wa kuishutumu Ligi Kuu ya EPL kwa kilichoitwa ufisadi.

Hii yote ni kuonyesha namna pointi 10 hizi zilivyowaumiza na kuwachanganya mashabiki wa Everton ambayo ilikuwa kwenye nafasi ya 14 kabla ya adhabu hiyo na sasa iko kwenye nafasi ya 19 katika msimamo wa ligi hiyo inayoundwa na klabu 20.

Pamoja na adhabu hiyo iliyotolewa na tume iliyokuwa inaichunguza Everton, ziko klabu nyingine za EPL zinazokabiliwa na hatari kama iliyowakumba Everton au hata dhahma kubwa zaidi ya hiyo.

Chelsea ya jijini London na Manchester City ya jiji la Manchester zina tuhuma zinazoonekana nzito kuliko hata tuhuma walizokuwa nazo Everton.

Wengi hawakuona adhabu ya kupokwa pointi 10 ikiinyemelea Everton; ilionekana kama kesi ya kupigwa faini tu. Everton walikuwa na sababu kadhaa ikiwemo biashara yao kuathirika na janga la ugonjwa wa Uviko 19, pia mradi wa ujenzi wa uwanja wao unakula pesa nyingi. Hiyo yote na maelezo mengine ya kihasibu na kisheria hayakuweza kuwatoa Everton kitanzini. Madhara ya adhabu kama hii kwa Chelsea yanaweza yasiwe makubwa kama yale yanayoweza kuwapata Manchester City endapo watatiwa hatiani. Chelsea wana kimbilio la kwamba ukiukwaji wa taratibu za fedha ulifanyika chini ya mmiliki wa zamani Roman Abramovic ambaye uvamizi wa Urusi katika Ukraine uliwezesha kufurushwa klabuni Stamford Bridge.

Manchester City ambayo imechukua ubingwa wa Ligi Kuu mara 4 katika miaka mitano inaweza kupigwa faini, kupokwa pointi hata kunyang’anywa mataji iliyopata huko nyuma. Manchester City imekuwa sio tu kwamba ni chombo cha michezo cha mmiliki wake Sheikh Mansour Bin Zayed wa Abu Dhabi bali pia imekuwa ni taswira yake na zana muhimu ya diplomasia kwa ufalme wake.

Kashfa kama hii haiwezi kumwacha salama Sheikh Mansour na uwezekano mkubwa pale likitokea la kutokea ni kwa tajiri huyo kuitelekeza City na kununua klabu nyingine, labda kwenye ligi nyingine itakayompa heshima anayoitaka.

Bado ni mapema mno kuiongelea City katika wakati uliopita na kesi dhidi yake haiwezi kuwa rahisi kwa sababu wana msuli wa kisheria, kifedha na uhusiano katika Uefa na Fifa.

Hii Financial Fair Play au mstari wa matumizi ya fedha kiungwana ni nini? Hii ni kanuni iliyoanzishwa na Shirikisho la Vyama vya Soka Ulaya (UEFA) mwaka 2009.

Lengo la kanuni hii ni kudhibiti matumizi ya klabu ili zisiishi zaidi ya kipato chao, ikiwa na nia ya jumla ni kudhibiti, kusimamia na kuendeleza uwezo wa kiuchumi wa klabu za soka. Lengo lisilotajwa wazi katika kanuni hii ni pamoja na kuzuia mpira kuendeshwa kwa kutumia fedha zisizo mapato ya soka na zaidi pesa chafu kama za mauzo ya dawa za kulevya, mauzo haramu ya silaha, usafirishaji haramu wa binadamu na shughuli nyinginezo za magenge ya kihalifu.

Mamlaka za soka katika mataifa wanachama wa Uefa zinatakiwa kuhakikisha nidhamu hii inazingatiwa na kuingizwa katika kanuni zao kulingana na mazingira yao. Katika Ligi Kuu ya England, kanuni hizi zimedhibiti na kuzuia klabu zenye tamaa ya kununua mafanikio na kuingia kwenye hatari ya kufilisika.

Hatima ya Everton na Ligi Kuu inabaki katika rufaa ambayo wameshaeleza kusudio la kuikata au vinginevyo wakae kimya na kupambana na hali yao, yaani waende hadi mwisho wa msimu na kujipatia pointi zitakazowawezesha kubaki juu ya mstari wa kushuka daraja.

Kwa hali ilivyo Everton hawana mpira wa kujihakikishia zaidi ya pointi 40 katika michezo iliyobaki kama hawataweza kupandisha kiwango chao. Mmiliki wao mpya 777 Partners, hawezi kutumia fedha kufanya manunuzi kwenye dirisha dogo labda afanye kwanza mauzo ili kuweka sawa mzani wa matumizi ya fedha.

Yote kwa yote hali ni tete ndani na nje ya uwanja kwa klabu hiyo ambayo enzi za udhamini wa SportPesa timu yake ikiwa na Wayne Rooney ilikuja Tanzania na kucheza na Gor Mahia ya Kenya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Pamoja na nia nzuri ya mstari huu wa matumizi ya fedha za soka, bado unaweza kuwa kikwazo kwa maendeleo na mipango ya mpira na zaidi unaweza kuwa mwiba kwa klabu zenye uchumi mdogo na zisizo na raslimali nyingi, kama wachezaji wa kuuza.

Haishangazi sasa kuona klabu za Ulaya zinayumbishwa na ligi moja tu ya Saudi Arabia katika soko la usajili. Wachezaji kama Cristiano Ronaldo, Sadio Mane, Edouard Mendy, Karim Benzema na wengine wengi wameenda kucheza Saudia kwa sababu klabu za kule zinaweza kutumia fedha kadri mifuko yao inavyoruhusu tofauti na ilivyo Ulaya.

*Mwandishi wa Makala hii ni katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania.naweza kumtumia maoni yako kupitia namba yake ya simu iliyoko hapo juu.