NIONAVYO: Bila waamuzi wazuri, VAR haitoshi

Muktasari:

Tukio litakalofanya mchezo huo ukumbukwe ni mpira alioupiga langoni nyota wa Yanga Azizi Ki ukaonekana kumpita kipa wa Mamelodi, Williams na kuvuka mstari wa goli, kudunda ndani na kurudi uwanjani. Kinyume cha matarajio ya wengi, mwamuzi alipeta na mchezo ukaendelea.

Mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini na Yanga ya Tanzania utabaki katika kumbukumbu za wapenzi wa Yanga, Mamelodi na wapenzi wa soka kwa ujumla kama goli la mkono la Maradona dhidi ya England katika Kombe la Dunia 1986 linavyokumbukwa na Waingereza na ulimwengu wa soka duniani.

Tukio litakalofanya mchezo huo ukumbukwe ni mpira alioupiga langoni nyota wa Yanga Azizi Ki ukaonekana kumpita kipa wa Mamelodi, Williams na kuvuka mstari wa goli, kudunda ndani na kurudi uwanjani. Kinyume cha matarajio ya wengi, mwamuzi alipeta na mchezo ukaendelea.

Kama kuweka chumvi kwenye kidonda kibichi, Rais wa CAF ambaye familia yake inamiliki klabu ya Mamelodi, Dk Patrice Motsepe, alinukuliwa akiwa Zanzibar akisema kwa maoni yake lile lilikuwa ni bao halali.

Maoni ya Rais wa CAF yalikuja wakati Yanga ishazuiwa kuingia nusu fainali na Mamelodi imefuzu kama moja ya timu nne zinazowakilisha Afrika kwenye mashindano yenye fedha kubwa ya klabu bingwa ya dunia 2024 huko Marekani. Mwamuzi wa kati anabaki kuwa na kauli ya mwisho.

Mchezo wa Mamelodi Sundowns dhidi ya Yanga ni mfano wa michezo mingi inayoendeshwa chini ya usimamizi na mfumo wa VAR lakini uamuzi unaenda kombo au tuseme unakuwa si sahihi kwa asilimia 100, kinyume cha matarajio ya wapenzi wa mpira wa miguu.

Ni muhimu tukajua VAR ni nini? VAR au kwa kirefu Video Assistant Referee ni mwamuzi msaidizi anayetumia nyenzo za kielektroniki kumsaidia mwamuzi mkuu (wa kati) katika kufanya uamuzi au kurekebisha uamuzi yake. Kumbe sasa VAR ni mwanadamu? Ndiyo, VAR ni mwanadamu, ni mwamuzi msaidizi kama walivyo washika kibendera pale mchezo unapoendelea.

Huyu VAR ana faida ya kuufuatilia mchezo akiwa na wasaidizi wengine wanaoweka macho yao kwenye runinga kuhakikisha matukio na uamuzi yanakuwa sahihi. Mwamuzi huyo msaidizi huwasiliana na mwamuzi wa kati kumwelekeza mambo kadhaa kama kuna bao au sio bao, penalti au sio penalti, kadi nyekundu ya moja kwa moja au kadi nyekundu hata njano iliyotolewa kimakosa kwa asiyehusika.

Kwa hiyo kwa ufupi VAR, ni mwamuzi msaidizi anayetumia mfumo wa kielektroniki kumsaidia mwamuzi wa kati na mfumo anaoutumia ndio unaitwa mfumo wa VAR (VAR System).

Teknolojia ya mfumo wa VAR ilianza kufanyiwa majaribio mwanzoni mwa miaka ya 2010 nchini Uholanzi.Chama cha mpira cha taifa hilo, KNVB, kiliruhusu mfumo huo kutumika katika michezo ya Ligi Kuu ya nchi hiyo ijulikanayo kama Eredivisie.katika msimu wa 2012/13.

Inasemekana majaribioyalikwenda vizuri kiasi cha kuliomba Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na bodi ya soka ya kimataifa (IFAB) zitoe ruhusa ya mfumo kufanyiwa majaribio. Haikuwa rahisi kwa FIFA, hasa rais wake wakati huo, Sepp Blatter, kukubali matumizi ya VAR kwenye mpira wa miguu.

VAR ilionekana kama kuingilia mtiririko wa asili wa mpira wa miguu.

Baada ya mabadiliko ya uongozi wa FIFA mwaka 2016, IFAB iliruhusu mfumo wa VAR kufanyiwa majaribio na kuanzia hapo ligi na mashindano mbalimbali ya kimataifa yakatumika kufanya majaribio ya mfumo huo.

Mambo yalienda kwa kasi na mchezo wa kwanza wa timu za taifa chini ya mfumo wa VAR wenye baraka za FIFA ukazikutanisha Ufaransa na Italia. Machi 3, mwaka 2018 IFAB ikaingiza VAR katika kitabu cha sheria za mpira (Laws of the Game).

Baada ya hapo FIFA ikatangaza rasmi kuruhusu mfumo wa VAR kutumika kwenye mashindano ya Kombe la Dunia, Russia 2018.

Baada ya Kombe la Dunia la Russia 2018, FIFA ilitoa ripoti ya kuridhika na matumizi ya mfumo wa VAR huku ikitoa ushahidi wa kupungua kwa matukio kama ya penalti kulinganisha na mashindano yaliyotangulia.

Hata hivyo, kumekuwa na upinzani dhidi ya uwapo wa mwamuzi wa mfumo wa VAR.

Yamekuwepo matukio kama lile la Stephane Azizi Ki na mengine mengi ambayo hayashughulikiwa vizuri na VAR.VAR pia imeshutumiwa kutokuwa na mwendelezo sawia (inconsistency) katika matukio yanayofanana.

VAR pia imekuwa chanzo cha mikanganyiko katika baadhi ya michezo kama tulivyoona hapo juu.VAR inapunguza raha ya mchezo kwa walioko uwanjani na hata walioko nyumbani, kwa mfano inabidi wasubiri mwamuzi achungulie kwenye runinga iliyoko pembeni mwa uwanja ndipo wapate ruhusa ya kushangilia au wasishangilie bao.

Pia waamuzi wasaidizi walioko uwanjani wamekuwa wakiagizwa kutoinua kibendera mpaka tukio lifike mwisho na kuhakikiwa na VAR. Hayo yote yanapoteza muda na mvuto wa mchezo.

Hapa Tanzania matumizi ya VAR kwenye Ligi Kuu yanatarajiwa kuanza mwakani.

Ili kujiandaa na hilo serikali kupitia Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa na pia Waziri anayeshughulika na michezo imeliweka hilo hadharani na huku bunge likiondoa ushuru kwa watakaoingiza vifaa vinavyohusiana na mfumo wa VAR.

Inasemekana baadhi ya wadau wa ligi wameanza kuleta mifumo hiyo.

Kama ilivyokuwa katika mataifa ya Kaskazini mwa Afrika na kwingineko ambayo tayari yanatumia teknolojia hiyo katika mpira, hapa Tanzania matarajio ya wadau ni makubwa kwamba VAR itaboresha ligi yetu na kuchangia katika maendeleo ya mpira.

Ukweli ni kwamba mfumo wa VAR hutegemea kwa kiasi kikubwa mwamuzi msaidizi anavyotafsiri matukio na jinsi anavyowasiliana na mwamuzi wa kati. Mwamuzi wa kati halazimiki kuufuata au kuutumia ushauri wa VAR.

Mwamuzi wa kati anabaki kuwa wa mwisho.

 Tangu mfumo wa VAR uanze kutumika katika Ligi Kuu ya England (EPL), umepata lawama nyingi hasa kutoka kwa mameneja wa klabu. Makocha kama Mikel Arteta wa Arsenal wanaamini VAR imeingilia sana mchezo kiasi cha kuweza kuathiri hata msimamo wa ligi unapofika mwisho wa msimu.

Kuingia msimu wa 2024/25 wa ligi ya EPL, ilibidi mameneja wa klabu waitwe na kuonywa kuwa wachukue tahadhari wanapotoa maoni yao kuhusu mfumo huo, vinginevyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

Ajabu, tayari VAR imeshaanza kuvurunda mapema na walimu wanapata ugumu kuzuia maoni binafsi kuhusu VAR.

Kwa ujumla, kuongezeka kwa matumizi ya VAR na mfumo wa VAR kwa ujumla bado kunategemea zaidi elimu, uelewa, tafsiri, utashi na uamuzi wa kibinadamu.

Yako mazuri yaliyokuja na VAR lakini bado ina upungufu na hata kero nyingi.

Elimu, weledi na werevu kwa waamuzi bado ni muhimu zaidi hata itakapoanza kutumika VAR katika ligi yetu.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.