Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: 2025 kutoa mwelekeo wa mpira Wetu

Nionavyo Pict

Muktasari:

  • Mwaka 2024 ulikuwa mwaka wenye matukio mchanganyiko katika michezo, hususani soka au mpira wa miguu. Kwa manufaa ya wasomaji wa safu hii, tutaongelea zaidi soka kama mchezo unaochezwa katika mikoa yote, wilaya, kata, shehia, vijiji, mitaa na vitongoji vyote vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpira wa miguu ni mchezo unaojumuhisha matabaka yote nchini.

Ni msemo wa kawaida kwamba “mpira una maajabu yake”, lakini kuna msemo wa kiufundi zaidi kwamba “mpira unavyoupiga ndivyo unavyokwenda”. Kiufundi, jambo lolote ni matokeo ya juhudi, maarifa na mazingira. Sawa, yako matukio huonekana kama bahati au maajabu lakini matukio hayo aghalabu hupata msukumo wa mazingira.

Mwaka 2024 ulikuwa mwaka wenye matukio mchanganyiko katika michezo, hususani soka au mpira wa miguu. Kwa manufaa ya wasomaji wa safu hii, tutaongelea zaidi soka kama mchezo unaochezwa katika mikoa yote, wilaya, kata, shehia, vijiji, mitaa na vitongoji vyote vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpira wa miguu ni mchezo unaojumuhisha matabaka yote nchini.

2024 ni mwaka unaoingia kwenye historia ambao ndani yake kwa mara ya kwanza klabu mbili za kandanda zilifanikiwa, kwa pamoja ndani ya msimu mmoja, kucheza hatua ya makundi la Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF-CL). Pamoja na kuishia hatua iliyofuata ya robo fainali, kufika hatua hiyo kwa Yanga na Simba kulianza kuwafungua macho wanaofuatilia mpira wa Tanzania. Kwa kweli si jambo la kawaida kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika nchi moja kupeleka zaidi ya klabu moja kwenye ngazi ya robo fainali.

Mbali na michuano ya klabu, mwaka 2024 ulikuwa wa kihistoria kwa Tanzania kufuzu katika mashindano mbalimbali kwa timu za taifa. Timu hizo ni pamoja na Taifa Stars iliyofuzu CHAN na AFCON na huku ikiwa bado inawania kufuzu Kombe la Dunia 2026 ambalo mtoano bado unaendelea. Timu ya wanawake, Twiga Stars ilikuwa inawania kushiriki mashindano ya timu za taifa za wanawake WAFCON, na kufanikiwa kufuzu. Timu ya vijana chini ya miaka 17 inakwenda Afcon U-17. Timu ya vijana chini ya miaka 15 (U-15) inakwenda kwenye mashindano ya CAF ya shule za sekondari. Timu ya soka la ufukweni pia imefuzu mashindano ya Afrika.

NV 01

Mashindano ni mengi ambayo tunakwenda kushiriki. Siwezi kusema kuwa hatuna uzoefu wa kushiriki, hapana. Hata hivyo, hatuna uzoefu wa kushiriki na kushinda hasa kwa mshindano ya wakubwa. Pia hatuna uzoefu wa kushiriki kwa timu nyingi kiasi hiki.

Pamoja na kushiriki mashindano mengi, Tanzania ni mwandaaji mwenza wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) mwaka huu. Ni heshima lakini pia ni kazi kubwa kwelikweli ambayo Tanzania na mataifa ndugu ya Kenya na Uganda wanatakiwa kuifanya. Pamoja na kufanikisha mashindano hayo ya CHAN, nchi hizi zina jukumu la kuihakikishia dunia kwamba wana uwezo wa kuandaa mashindano makubwa kwani kwa pamoja watakuwa wenyeji wa mashi-ndano makubwa kabisa ya Mataifa ya Afrika yaani AFCON 2027.

NV 02

Kwa haraka unaweza kuona ni namna gani haya tunaweza kuyaita mafanikio makubwa. Hata hivyo, mafanikio haya yanakuja na wajibu mkubwa.

Yanakuja na wajibu ambao ukibebwa vizuri unaweza kuweka alama na kuwa mwanzo wa mambo mengine makubwa zaidi.Taifa lolote duniani lingeweza kujivunia kuwa katika mazingira haya.

Mashindano mengi yana maana ya mahitaji makubwa ya kifedha kwa serikali na shirikisho. Pamoja na kwamba kuna baadhi ya majukumu hubebwa na waandaaji kama CAF au FIFA lakini kuna mambo mengi kama kuandaa timu na kugharamia miundombinu ya michezo ambayo shirikisho husika na serikali yake wanalazimika kuingia mfukoni.Hili si suala dogo na bila shaka wahusika wamejiandaa vilivyo.

NV 03

Kama tulivyosema hapo awali, kushiriki ni jambo moja na kushiriki kwa mafanikio ni jambo jingine.

Kuandaa timu hizi zote ili ziweze kufanikiwa kunatakiwa kuwe kumeanza tayari. Maandalizi ya saa za jioni hayawezi kusaidia timu.

Kwa Taifa Stars inayocheza CHAN inaweza kufaidika kupitia mlango wa nyuma kwa wachezaji wake wanaocheza kwenye timu za taifa za Kilimanjaro na Zanzibar Heroes zitakazoshiriki mashindano ya timu za taifa ya Kombe la Mapinduzi. Hata hivyo, hilo tu halitoshi hasa unapokuwa mwenyeji wa mashindano.Timu mwenyeji kufanya vizuri ni kama asilimia 50 ya mafanikio ya mashindano.

NV 04

Mashabiki wengi hujaa viwanjani kadri timu zao zinavyofanya vizuri. Mashindano hayawezi kufana kama mashabiki hawajazi viwanja.

Ratiba hii ya mashindano mengi ya kimataifa inahitaji uratibu mahiri na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha tukio moja haliumizi tukio jingine.Mashindano ya ndani kama Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho yanaweza kuwa muhanga wa mashindano mengi ya mwaka 2025.

Tumesikia, hivi karibuni, bodi ya ligi ikitangaza kuahirishwa kwa Ligi Kuu ya NBC mpaka mwezi wa Machi 2025 kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi na yale ya CHAN.

NV 05

Kuahirisha huku kunaweza kuathiri ratiba ya ligi, Kombe la Shirikisho la CRDB na hata ushiriki wa klabu zetu katika mashindano ya Afrika. Athari ya matukio haya kwenye ligi inaweza kuwa na mwendelezo mpaka kugusa ligi ya msimu wa 2025/26.

Ushiriki wa timu za wanawake na za vijana unaweza usiwe na athari kubwa kwenye mipango ya Bodi ya Ligi (TPLB), lakini bado inaweza kuhitaji rasilimali fedha na rasilimali watu kutoka shirikisho hivyo pia uratibu wake unahitaji weledi wa hali ya juu.

Mwaka wa 2025 ni mwaka ambao umepokea fursa nyingi za kimkakati kutoka mwaka wa 2024.Ni namna gani fursa hizi zitachangamkiwa ni swali ambalo litatoa majibu ya mwelekeo wa soka letu kwa siku za usoni.


Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.