Ninja: Championship ni nguvu, Ligi Kuu mbinu
Muktasari:
- Hapo awali hakuwahi kucheza Championship, lakini ilipotokea nafasi hiyo akaichukulia ni upande mwingine wa kujifunza katika maisha yake. Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti, Ninja anasema katika kazi ya mpira wa miguu kuna mambo mengi, hivyo wakati ikitokea mchezaji anapokuwa chini anachotakiwa ni kufanya bidii na siyo kukata tamaa.
KITU pekee asichokubaliana nacho beki wa kati anayecheza Transit Camp ya Ligi ya Championship, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ni kutokata tamaa, kwa kuwa kila kinachotokea katika maisha anakichukulia kuwa ni funzo.
Hapo awali hakuwahi kucheza Championship, lakini ilipotokea nafasi hiyo akaichukulia ni upande mwingine wa kujifunza katika maisha yake. Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti, Ninja anasema katika kazi ya mpira wa miguu kuna mambo mengi, hivyo wakati ikitokea mchezaji anapokuwa chini anachotakiwa ni kufanya bidii na siyo kukata tamaa.
“Mchezaji hakuna mtu wa kuitetea ndoto yake, isipokuwa yeye mwenyewe kupambana, ndiyo maana nilipoona nafasi ya Championship nikaona ni upande mwingine tena wa kujituma, nikiamini bado nina nafasi ya kufanya vizuri mbeleni,” anasema.
CHAMPIONSHIP
Anasema wakati anakwenda kujiunga na Transit Camp ya Championship, zilikuwepo timu za Ligi Kuu Bara, ila kuna mambo hayakwenda sawa, hivyo hakuna sababu ya kukaa nyumbani bila kazi.
Anakiri kwamba maisha ya mchezaji wa Ligi Kuu na Championship yanatofautiana kifursa na kiuchumi, ila kwa upande wake anapata funzo kubwa la jinsi ya kuyatazama maisha kwa upana wake.
“Stori ninazozisikia kutoka kwa wachezaji wengine wanaocheza katika ligi hii ni za maisha magumu, nashukuru ni tofauti na hapa Transit Camp viongozi wanajitahidi kuhakikisha wachezaji wanapata stahiki zao, nilichojifunza ni kukabiliana na mazingira ya kila aina katika maisha, leo unaweza ukawa juu kesho ukawa chini hilo ni kawaida katika mpira wa miguu,” anasema.
Kiufundi anasema Ligi Kuu Bara inatumia zaidi mbinu, akitofautisha na Championship ambako ni nguvu zaidi
“Kinachosaidia Ligi Kuu kila mechi inaonyeshwa inapunguza makosa huku Championship zinaonyeshwa baadhi, jambo linalosababisha makosa yanakuwa mengi zaidi,” anasema mchezaji huyo.
Ukiachana na hilo, anasema amekutana na wachezaji tofauti na wale ambao alikuwepo nao Ligi Kuu, anaona namna ambavyo wanapambana ili kupata nafasi ya kuonekana kwa ukubwa.
“Nimekutana na wachezaji wanaotamani kuwa kile nimewahi kuwa, hilo linanipa imani ya kujituma, haijalishi nacheza mara nyingi au la, jambo la msingi ni kuona mitazamo ya wengine dhidi yako,” anasema.
Anapoulizwa na mwandishi wa makala haya kama hakuna timu zinazomtakaji za Ligi Kuu kwa sasa, Ninja anasema: “Hilo ni mapema kulijibu kwa sasa, jambo la msingi ni kuhakikisha huduma yangu inakuwa muhimu kwa timu iliyoniajiri.”
KUCHEZA NJE
Ninja anaelezea kucheza nje kwake jinsi kulivyomsaidia kujifunza vitu vingi vinavyomsaidia katika kazi zake hata sasa.
“Nimekutana na watu tofauti katika harakati za mapambano, hivyo hali ya aina yoyote kwangu naichukulia kama fursa ya kujua vitu zaidi ambavyo sikuwa navyo awali,” anasema.
“Unapokutana na watu tofauti ni kufungua ukurasa mwingine wa mafunzo ya maisha, mfano Congo kukutana na wanajeshi wameshika bunduki katika daladala au mitaani kwao walikuwa wanaona ni jambo la kawaida kabisa, tofauti na hapa nchini.”
Kiuchumi anaeleza: “Nimefanya vitu vingi ambavyo siwezi kuviweka wazi, ila asilimia kubwa vimetokana na soka ikiwemo kumsaidia mama na ndugu zangu.”
KUKUTANA NA ZLATAN
Ninja anasema soka limemkutanisha na mastaa mbalimbali akiw emo Zlatan Ibrahimovic ambaye licha ya kuo nekana ni mbabe uwanjani na katika baadhi ya mahojiano yake, ila ni mtu poa na anayependa wengine wafanikiwe kwa juhudi binafsi.
“Nakumbuka ilikuwa asubuhi moja wakati nipo jikoni kuandaa chochote cha kifungua kinywa, nikakutana naye akiwa katika harakati hizo, tukasalimiana, akaniuliza natokea bara gani nikamjibu Afrika, akafurahi sana,” anasema na kuongeza:
“Miongoni mwa kauli ambazo sitazisahau kutoka kwake, aliniambia una muonekano wa kimpira, amini katika ndoto zako bila kujali wengine wanamtazamo gani, kwani hao hawawezi kuhisi uhalisia wa kile unachokiona mhusika, haujafika Marekani kwa bahati mbaya, upo kwa sababu ya mpira wa miguu, hivyo pambana na endelea mbele. “Siyo mtu anayependa kupoteza muda kwani hata kwa muda mchache niliyokuwa naye aliuthamini, maana palikuwa na watu wengi ambao walitamani hiyo nafasi, maana kabla ya kukutana naye asubuhi nilisikia stori zake kwamba Ibrahimovic yupo kambini amefika, hilo lilionyesha ukubwa wake, pia alinionyesha ucheshi wake ingawa ni kweli siyo mtu wa kumkabili kirahisi.”
Ninja mwenye urefu wa mita 1.88 alizaliwa Oktoba 21, 1998, Zanzibar, Tanzania, anasema bado ana deni la kufanya au huduma yake kuendelea kutumika katika mpira wa miguu. “Ukiachana na Ibrahimovic kunipa moyo wa kupambana, niliwahi kubahatika kujengwa na kaka yangu aliyekuwa nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alinikabidhi jezi yake wakati anastaafu, hayo yote yananifanya nisiwahi kukata tamaa hata siku moja,” anasema.
TIMU ALIZOCHEZA
Kwa mara ya kwanza alijiunga na Yanga Julai Mosi, 2017, kisha akapata dili la kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya MFK Vyskov 2019 iliyompeleka kucheza kwa mkopo LA Galaxy II ya Marekani, kisha akarejea tena Yanga mwaka 2020, akaenda Dodoma Jiji kwa mkopo Septemba 26, 2022, akarudi tena kwa Wanajangwani Desemba 28, 2022.
Alipo achana na Yanga alikwenda kucheza FC Lubumbashi Agosti 27, 2023, baada ya kuachana nao akasaini FC Lupopo Julai 25, 2025.