Nini Diarra? Hawa walitisha kwa kudaka
MASHABIKI wa Yanga kwa sasa wanatembea kifua mbele. Sio kwa sababu chama lao limetinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuing'oa Rivers United ya Nigeria, la!
Ila ni kwa namna lango la timu hiyo kwa kwa misimu miwili mfululizo likiwa lipo salama tangu aliposajiliwa kipa Djigui Diarra kutoka Mali. Msimu uliopita ndiye aliyekuwa Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara akiiwezesha Yanga kubeba taji la Ligi Kuu Bara bila kupoteza na kunyakua pia Ngao ya Jamii na Kombe la ASFC, huku kwa msimu huu akiwa keshaipa Ngao ya Jamii na hadi sasa ameifanya kazi kubwa akiwa ndiye kipa kinara wa clean Sheet katika Ligi Kuu inayoelekea mwishoni.
Kabla ya ujio wa Diarra, Yanga iliwahi kuteseka kwenye milingoti mitatu licha ya kusajili makipa kadhaa kutoka nje ya nchi, akiwamo Yew Berko kutoka Ghana, Doyi Moke au Klaus Kindoki kutoka DR Congo ama Younde Rostand wa Cameroon au wale kutoka Serbia wa miaka ya 2000.
Hata upande wa watani wao, Simba wamewahi kuwa na makipa kutoka nje ya nchi kama Mackenzie Ramadhani kutoka Burundi, Daniel Agyei wa Ghana, Vincent Angban wa Ivory Coast mbali na kina Berko na Doyi Moke ambao nao walikipiga Msimbazi au Abel Dhaira kutoka Uganda.
Mbali na Simba na Yanga, lakini klabu ya Azam FC imekuwa inaongoza kwa miaka ya karibuni kusajili makipa kutoka nje ya nchi. Utabisha nini wakati ilishakuwa na Waserbia, Mrundi Vladimr Niyonkuru, Razack Abalora au walionao sasa, Ali Ahamada kutoka Comoro na Abdolaye Idrissukutoka Ghana.
Kadhalika klabu nyingine kadhaa zikiwamo Coastal Union, Namungo zimekuwa na makipa kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa wakichuana na makipa wazawa kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara.
Umiliki wa makipa kuanzia wawili wa kigeni ndani ya timu na kwenye msimu mmoja inaweza kuchukuliwa labda Tanzania ina uhaba au tatizo la wachezaji wa nafasi hiyo, kama ilivyo kwa nafasi ya ushambuliaji.
Ila ukweli ni kwamba Tanzania haijawahi kuwa na tatizo la makipa tangu nchi iwe uhuru mwaka 1961.
Kwa ufupi ni kwamba Tanzania kwa miaka nenda rudi ilikuwa ikitamba kwa kuwa na makipa bora ambao wakati mwingine ilikuwa ikiwapa wakati mgumu makocha wa klabu ama timu ya taifa, Taifa Stars kumpanga nani mbele ya wenzake.
Labda tu ni kwamba kwa miaka ya karibuni, tangu Juma Kaseja alipopunguza makali, kisha kustaafu akikiachia kijiti cha Tanzania One kwa Aishi Manula inaonekana hakuna uhakika wa makipa hodari wa kuaminika ila ukweli vipaji vya nafasi hiyo kwa miaka mingi haijawahi kuwa majanga.
Mwanaspoti inakuletea orodha ya baadhi ya makipa waliowahi kutamba nchini na ambao wanatajwa kama makipa bora wa muda wote waliowahi kuibuka nchini;
OMAR MAHADHI
Huyu ndiye anayatajwa kama kipa bora kuwahi kutokea Tanzania tangu uhuru kwa namna alivyokuwa na kipaji cha hali ya juu.
Bin Jabbir, aliyeanzia soka lake katika timu ya African Sports na Mkoa wa Tanga kabla ya kunyakuliwa na Simba mwaka 1975 na kuichezea Taifa Stars kwa mafanikio makubwa. Kwa waliomshuhudia kipa huyo wanadai, alikuwa na umbile la kawaida tu, lakini jinsi alivyokuwa mkali langoni, viliwafanya wenzake kusubiri mbele yake. Alitetemesha sio Tanzania tu, bali hadi barani Afrika alichuana na makipa waliokuwapo miaka hiyo.
Ndio maana haikushangaza katika Michezo ya Afrika (All Africa Games) mwaka 1973 iliyofanyika Nigeria, alipoteuliwa kwenye timu ya Kombaini ya Afrika. Mahadhi aliyetuliwa sambamba na straika aliyetamba miaka hiyo aliyekuwa Yanga, Maulid Dilunga kuunda kikosi hicho cha Afrika kilichofanya ziara mataifa mbalimbali duniani ikiwamo Mexico na nchi za Ulaya.
Mkali huyo alifariki duniani miaka ya 1980 na hadi leo jina lake linatajwa kutokana na umahiri wake na kama hujui tu alikuwa langoni wakati Simba wakiiitia aibu Yanga kwa mabao 6-0 Julai 19, 1977.
ATHUMAN MAMBOSASA
Kipa mwingine mahiri aliyewahi kutokea nchini. Kipa Mambosasa aliyefariki miaka ya 1990, alisifika kwa umahiri wake wa kulinda lango akisaidiwa na urefu wake. Cha kuvutia ni kwamba kipa huyu, pamoja na Mahadhi waliibuliwa na kocha Mjerumani Bemhard Carl Trautmann 'Bert Trautmann' na kudaka pambano ndani ya Simba, kiasi inaelezwa waliwapa kazi kubwa makocha kuamua nani wa kumpanga na kuwaachia kazi ya kuchagua wenyewe aanze nani kati yao. Huyu Trautmann ndiye aliyemuibua pia Juma Pondamali na nyota wengine miaka ya 1970. Mambosasa alikuwa kwenye kikosi cha Simba kilichofika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika 1974. Mambosasa pia alikuwa kwenye kikosi kilichoitoa nishai Mufurila Wanderers ya Zambia kwa kuifunga kwao 5-0 baada ya awali kushinda 4-0 ugenini jijini Dar es Salaam. Pia alikuwa kwenye kikosi cha Tanzania kilichoshiriki fainali za kwanza na mwisho za Kombe la Mataifa ya Afrika (afcon) 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.
Katika kikosi hicho Mambosasa aliambatana na makipa wengine Juma Pondamali 'Mensah' na Idd Pazi 'Father'.
Kabla ya kutua Simba kuidakia kwa mafanikio akiwa na Mahadhi, Mambosasa aliwahi kupitia Pan Africans kwa muda mfupi. Miaka inaenda na kupitia, lakini jina lake linaendelea kudumu akiwa mmoja ya makipa hodari kuwahi kutokea nchini.
JUMA PONDAMALI 'MENSAH'
Utasema nini juu ya kipa huyu wa zamani wa Yanga, Pan Africans, Pilsner na AFC Leopards ya Kenya, aliyekuwa ngumi mkononi. Yaani ukimzingua anakuzingua.
Achana na vituko vyake vilivyokuwa vikimfanya afungiwe kila mara kwa makosa ya kuwapiga waamuzi ama wachezaji wenzake, lakini Pondamali alikuwa fundi mahiri langoni.
Ndiye aliyedaka kwenye mechi muhimu dhidi ya Zambia mwaka 1979 ambayo iliivusha Tanzania kwenda Nigeria kwenye fainali za Afcon 1980, ambapo huko alikuwa gumzo na kuacha simulizi la aina yake kwa udakaji wake wa mbwembwe.
Alikuwa na uwezo wa kudaka mpira kwa mkono mmoja, kumrudishia mshambuliaji mpira na kuudaka tena mpira kwa mbwembwe za kipekee kiasi cha kukera.
Ndio kwa wanaozikumbuka fainali hizo za Afcon 1980 alipoenda na Taifa Stars na kupata nafasi ya kudaka mechi zote na katika michuano ya Kombe la Chalenji zilizofanyika Sudan wanakumbuka vitimbi vyake.
Tangu amestaafu soka karibu miaka 20 iliyopita, hajatokea kipa aliyekuwa na mbwembwe uwanjani na vituko visivyoisha kama Pondamali aliyepewa jina la utani la Mensah akifananishwa na aliyekuwa kipa mahiri ya Ghana, Robert Mensah, aliyechomwa na kuuwawa na mashabiki kwa kitu chenye nchi kali wengine wakisema kisu na wengine chupa iliyovunjwa mwaka 1971 mjini Kumasi nchini kwao.
Kwa waliomshuhudia Mensah mwenyewe aliyeiwahi kuidakia Asante Kotoko miaka ya 1960 na 1970 na kuona ufundi wa Pondamali, waliamua kumbatiza kipa huyo aliyekuwa na mbwembwe na vituko uwanjani jina hilo lililomkaa hadi leo akiwa ni kocha wa makipa na mwimbaji wa muziki wa kizazi kipya kama ilivyo kwa kipa mwingine wa zamani wa Mtibwa Sugar, Yanga na Stars, Manyika Peter.
IDD PAZI 'FATHER'
Simba inatajwa kuwa klabu pekee iliyokuwa na bahati ya kuwa na makipa hodari ambao wamebaki kuwa gumzo hata baada ya kuachana na soka ama kufariki dunia.
Idd Pazi 'Father' ni miongoni mwa makipa bora kabisa waliowahi kutokea nchini, ambapo licha ya kuidakia Simba, pia aliwahi kuzichezea Majimaji-Songea, Pilsner, Majimaji na Al Merreikh ya Sudan.
Alikuwa miongoni mwa makipa walioenda Afcon 1980, ametwaa mataji kadhaa akiwa na Simba na Taifa Stars, huku akiwa ndiye muasisi wa jina la Tanzania One alilopachikwa kwa umahiri wake wa kulinda lango enzi zake, akifananisha na Mahmoud Abbas wa Kenya aliyekuwa Kenya One.
Umakini wake langoni na kuwapanga makipa wake ulimtofautisha na wenzake, huku akiwa kipa wa kwanza kufunga bao kwenye mechi ya watani, akifanya hivyo mwaka 1985 kabla ya Juma Kaseja kuifikia rekodi hiyo mwaka 2012 Yanga ilipokufa 5-0.
Kwa sasa amepumzika masuala ya soka hasa baada ya kupata changamoto ya kiafya na kabla ya hapo alishawahi kuwa kocha wa makipa wa timu mbalimbali ikiwamo Simba klabu aliyoichezea kwa mafanikio makubwa sambamba na Taifa Stars.
MOHAMMED MWAMEJA
Utasema nini kwa kipa huyo wa aina yake aliyewahi kutamba na klabu za Coastal Union na Simba.
Alikuwa na umbile linalowatisha washambuliaji wa timu pinzani, kuna straika mmoja aliwahi kumhojiwa na kusema, eti Mwameja alipokuwa langoni alikuwa analiziba goli kiasi alikuwa akipata wakati mgumu kujua afungie upande upi kwa umbo alilokuwa nalo, kipa huyo maarufu nchini.
Ndiye aliyelirithi jina la Tanzania One na kukaa nalo kwa muda mrefu kuliko kipa yeyote, huku rekodi zake zikisisimua kwa kuweza kuifikisha Simba fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa hadi leo na timu yoyote. Alisajiliwa na Simba mwaka 1992 akitokea Coastal Union aliyeisaidia kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1988.
Mwameja alikuwa na uwezo mkubwa wa kudaka michomo mikali na kupanga mabeki wake na pia alikuwa na uwezo wa kuwaongoza wenzake uwanjani, pia alikuwa na mikwara iliyowafanya wachezaji wa timu pinzani kupata woga kwake.
Kwa sasa anajishughulisha na mambo ya biashara akiwa ameachana kabisa na soka, lakini jina lake linaendelea kukumbukwa kwa umahiri wake langoni enzi zake.
Mwameja anatajwa kama mmoja wa makipa waliotwaa mataji mengi (16) akiwa na Simba, akibeba Ligi Kuu Bara 1994, 1995 na 2001, Kombe la Nyerere (1995 na 2000), Ligi Kuu ya Muungano (1993, 1994, 1995, 2001 na 2002) Kombe la Tusker (2001 na 2002) na Kombe la Kagame (1992, 1995, 1996 na 2002).
Pia ametwaa taji la Kombe la Chalenji akiwa na Taifa Stars mwaka 1994, michuano ikifanyika Kenya, ikiwa ni baada ya miaka 20 kupita tangu Tanzania Bara ilipobeba taji la mwisho ya Chalenji 1974.
JUMA KASEJA
Kwa kizazi cha hivi karibuni huyu anatajwa ndiye kipa bora kwa uwezo wake mkubwa wa kulinda milingoti mitatu. Hakuwa na mwili mkubwa kama makipa wenzake waliotanguliwa kutajwa hapo juu, lakini umahiri wake langoni umemfanya Kaseja hadi sasa kutajwa kama mmoja ya makipa waliokuwa tishio na wagumu kufungika langoni.
Uwezo wake wa kudaka michomo, kupangua penalti na kupanga mabeki wake na hata wakati mwingine kupandisha mashambulizi yamemfanya kipa huyo kuendelea kuwa gumzo, akiwa ndiye aliyekuwa Tanzania One kabla ya kumpisha Manula.
Ndiye aliyekuwa kwenye kikosi cha Simba kilichoandika historia ya kuwavua ubingwa waliokuwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2003, Zamalek ya Misri kwa kudaka penalti mbili nchini Misri na kuivusha Simba kucheza makundi ikifuata nyayo za Yanga ilizoweka mwaka 1998.
Pia alihusika na kuipeleka Taifa Stars kwenye fainali za pili za CHAN 2020 kwa uwezo wake wa kudaka penalti na hivi karibuni alisaini mkataba wa kwenda kufanya kazi na mshikaji wake, Mecky Maxime, Kagera Sugar baada ya kupita timu kadhaa ikiwamo Mbeya City, Yanga, Simba na KMC aliyokuwa akiidakia msimu uliopita.
Kaseja ana vitu adimu kulinganisha na makipa wa zama hizi, jambo ambalo linamfanya kuendelea kutajwa kama kipa bora wa zama hizi, hasa ikizangatiwa kuwa kwa sasa Stars haina kipa namba moja wa kutumainiwa kama ilivyokuwa enzi zake, japo Manula kuonekana hana mpinzani.
Kipa huyo mstaafu naye ametwaa mataji mengi akiwa na Simba, Yanga na Taifa Stars ikiwamo mataji ya Ligi Kuu Bara 2003, 2004, 2007, 2009, 2010 na 2012, Kombe la Tusker (2003, 2005), Ngao ya Jamii (2003, 2005, 2011 na 2012) na Mapinduzi Cup (2008). Kwa Stars alitwaa nao Chalenji 2010.
MAKIPA WENGINE
Mbali na makipa hao waliotajwa hapo juu, lakini kuna wengine wakali walioacha alama kubwa kwenye soka la Tanzania kwa ustadi wao wa kudaka sambamba na vituko walivyowahi kufanya enzi wakicheza kiasi licha ya kustaafu au wengine kutangulia mbele ya haki bado wanakumbukwa.
Utabisha nini juu ya uwezo aliokuwa nao kina Hamis Kinye, Joseph Fungo, Peter Manyika, Moses Mkandawire, Kichochi Lemba, Mahamoud Nyalusi, Riffat Said, Steven Nemes, Joseph Katuba, Ali Bushir 'Benitez', John Bosco, Juma Mhina, Farouk Ramadhan, Madatta Lubigisa, Paul Rwechungula, Sahau Kambi, Kelvin Mhagama, Ivo Mapunda na Ally Mustafa 'Barthez'.
Makipa wengine wanaokumbukwa nchini ni Ismail Suma, Often Martin, Issa Manofu na ukirudi nyuma kuanzia miaka ya 1960 hadi 1980 kulikuwa na vichwa hatari vya kudaka mipira akiwamo Kitwana Manara 'Popat' aliyegeuka kuwa mshambuliaji tishio kama ilivyowahi kutokea kwa Said Mhando aliyeipandisha Mtibwa Sugar na baadae kuwa straika hatari nchini.
Pia kuna majina kama ya Abdul Hamid, Mbaraka Salum, Elias Michael 'Nyoka Mweusi', Muhidini Fadhil, Abdallah Bobea, John Semainda, Greyson Mwamwaja, Hassan Mlapakolo, Hemed Mussa, Dunia Adonis, Hamis Makene, Salim Waziri, Mbwana Makatta na wengine. Kwa hakika Tanzania kwa makipa, acha kabisa!