Prime
Ni muda sasa wa Taifa Stars kurejea Kwa Mkapa
WAKATI tunaelekea kuandaa fainali za mashindano ya ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), tulionekana kama hatukuwa na mkakati wa maandalizi ya timu na pia kuwaandaa mashabiki kuyapokea kwa mashamsham.
Juhudi kubwa zilifanyika mwishoni kushawishi wananchi wajitokeze kwa wingi kuangalia mechi hizo hasa wakati timu yetu ikicheza, tukiendelea na mtindo uleule wa kutumia wasemaji wa klabu za Simba na Yanga kuonyesha taifa kuungana kuwa kitu kimoja.
Wenyeji wenzetu wa Kenya na Uganda walifanikiwa kiasi fulani kujaza viwanja, hata pale timu zao zilipokuwa hazichezi fainali ikiwa ni ushuhuda mkubwa wa jinsi Kenya walivyohamasika.
Timu yetu ilienda kuweka kambi Misri takriban wiki mbili kabla ya mashindano kuanza, Shirikisho la Soka (TFF) likaandaa mashindano mafupi ambayo hayakuwa na mafanikio baada ya baadhi ya waalikwa kugoma kushiriki.
Msimu wa soka ulichelewa kuisha na hivyo wachezaji kuwa na muda mfupi wa kupumzika kabla ya kuingia kambini na timu kutotambulika vizuri kwa mashabiki kutokana na baadhi ya wachezaji kubadilikabadilika.
Moja ya mikakati ilitakiwa kuwa ya timu yetu kucheza mechi za kirafiki kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku idara ya habari ikifanya kazi kubwa ya kuhamasisha mashabiki kujitokeza kwa wingi.
Kulikuwa pia na haja kwa idara hiyo ya mawasiliano kuandaa siku maalumu kwa ajili ya vyombo vya habari kushuhudia mazoezi ya wazi na baadaye kufanya mahojiano na wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa ajili ya kuijua vizuri timu na kuondoa tetesi zozote kuhusu kikosi hicho.
Hayo hayakufanyika na haikuwa ajabu mashabiki kusita kujitokeza viwanjani, ukizingatia kuwa mashindano hayo hayana mvuto unaotokana na wachezaji nyota wanaocheza kwenye ligi kubwa duniani, kama zilivyo fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).
Tunaelekea fainali za Afcon zitakazofanyika Morocco mwakani, huku vichwani tukiwa na akili za kuwa tena wenyeji wa Afcon za mwaka 2027 zitakazoandaliwa kwa pamoja nan chi tatu za Afrika Mashariki.
Pengine TFF wana mkakati wao wa jinsi ya kuandaa timu na mashabiki, lakini haitakuwa vibaya tukichangia mawazo ya nini kifanyike.
Timu ya taifa itacheza mechi ya kirafiki ya tarehe ya Fifa siku ya Ijumaa wakati itakapokuwa mgeni wa Kuwait nchini Misri. Ni mechi nzuri, hasa kutokana na jinsi nchi kutoka Arabuni zinavyozidi kukua kisoka, mechi dhidi ya Iran ikiwa ushuhuda baada ya ushindi wa mabao 2-0.
Timu italazimika kucheza mechi moja baada ya viongozi wa klabu zinazoshiriki mashindano ya klabu Afrika kuomba wachezaji wao warudi mapema kwa ajili ya maandalizi ya mechi hizo.
Kuna haja kubwa kwa TFF kurudisha akili kwenye Uwanaja wa Mkapa ambao pia utatumika kwa mechi za Afcon za mwaka 2027.
Kila wakati timu inapocheza nje inapoteza mvuto na katika siku za karibuni imebidi serikali iingilie kati kwa kununua tiketi na kuruhusu mashabiki kuingia bure, jambo ambalo linashusha thamani ya timu.
Timu inapocheza nje dhidi ya timu za kawaida na hasa inapopoteza, inapunguza mvuto kwa mashabiki na hivyo ni muhimu kurudi Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya mechi za kirafiki ili kurudisha hamasa iliyokuwepo kwa mashabiki miaka michache iliyopita.
Ni jambo la kujiuliza inakuwaje timu iliyofuzu mara tatu kucheza Afcon bado haiwezi kujaza Uwanja wa Mkapa wakati timu ambayo haikuwahi kufuzu ilikuwa inajaza uwanja?
Ni lazima kuna mvuto unakosekana na ambao ni lazima urejeshwe kwa mbinu na mikakati tofauti.
Wakati ule wapinzani wa Tanzania walikuwa kama Ivory Coast, Senegal, Misri, Morocco, Algeria na zaidi tukawahi kucheza mechi za kirafiki na mataifa kama Afrika Kusini, Cameroon na Pakistan, mechi ambazo huhitaji nguvu nyingi kuhamasisha mashabiki wajae uwanjani.
Lakini tangu Shirikisho la Soka Afrika (CAF) libadili mfumo wa kufuzu kucheza fainali za Afcon na CHAN, hatupati wapinzani wakubwa kama hao. Badala yake tunakutana na timu kama Niger, Cape Verde, Guinea au za kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo bado hazijakuwa na nyota wanaonekana kila mwishoni mwa wiki katika ligi kubwa duniani.
Kwa hiyo, kunahitajika kwanza kurudi kwa Mkapa kucheza mechi za kirafiki, jambo ambalo linaweza kufanikishwa na sekretarieti kama itafanya kazi kubwa ya kusaka mechi dhidi ya ‘wakubwa’ badala ya kusubiri hizi za nchi za Uarabuni.
Kuche-za nyumbani pia kunasaidia kupunguza uchovu wa safari kwa wachezaji. Fikiria wachezaji wa Simba, Yanga, Singida Black Stars na Azam wataathirikaje na mechi hiyo dhidi ya Kuwait.
Wamecheza mechi mwishoni mwa wiki, waliokuwa nje ya Dar es salaam wamelazimika kusafiri kurudi Dar. Siku moja baadaye watasafiri tena kwenda Misri na baadaye kurudi tena Dar kabla ya kwenda kwenye mechi zao nje ya nchi.
Ni uchovu ambao utaathiri klabu zao ama timu ya taifa.
TFF inatakiwa irejeshe burudani ya Watanzania nyumbani wakati huu tunaojiandaa kuandaa fainali za AFCON za mwaka 2027. Na Uwanja wa Mkapa ndio mahali sahihi pa kurejesha mapenzi ya Watanzania kwa timu yao badala ya kusubiri ushawishi wa Ally Kamwe na Ahmed Ally.