Mzigo wa AFCON 2025 upo Boxing Day
Muktasari:
- Shughuli kwanza itaanzania kwenye Kundi A, ambapo Comoro itakuwa na kazi ya kujiuliza ilifungwaje mchezo wake wa kwanza itakapojaribu kusaka ushindi wake wa kwanza kwenye AFCON 2025 kwa kuikabili Zambia uwanjani Stade Mohamed V.
MERRY Christmas. Na kesho, Alhamisi ni Boxing Day, ambapo huko kwenye mikikimikiki ya AFCON 2025, vigogo wanane wa soka watakuwa na kazi ya kufungua maboksi ya zawadi kwa mashabiki wao watakapoonyeshana ubabe kwenye mchakamchaka wa kusaka ubingwa wa Afrika nchini Morocco. Nani watafungua zawadi kwa kicheko? Na nani watafungua kwa kilio na kujiweka kwenye hatari ya kufungashiwa virago vyao vya kutupwa nje kwenye Afcon 2025?
Shughuli kwanza itaanzania kwenye Kundi A, ambapo Comoro itakuwa na kazi ya kujiuliza ilifungwaje mchezo wake wa kwanza itakapojaribu kusaka ushindi wake wa kwanza kwenye AFCON 2025 kwa kuikabili Zambia uwanjani Stade Mohamed V.
Katika mchezo wa kwanza, uliokuwa wa ufunguzi wa mashindano hayo ya AFCON 2025, Comoro ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa wenyeji Morocco na hivyo ndiyo wanaoburuza mkia kwenye kundi baada ya mechi hiyo moja. Zambia yenyewe, itasaka ushindi ili kukusanya pointi nne ambazo zitaiweka pazuri, baada ya mechi yao ya kwanza kutoka sare ya 1-1 na Mali, shukrani kwa bao la dakika za majeruhi la Patson Daka, aliyemchambua kwa kichwa kipa Djigui Diarra.
Vinara wa kundi hilo, Morocco, ambao pia ni wenyeji, wenyewe watakuwa na kibarua mbele ya Mali ya kipa wa Yanga, Djigui Diara. Ni mechi ngumu, ukizingatia Mali itajaribu kutafuta pointi ya kujiweka hai kwenye mashindano hayo, huku Simba wa Atlas wakitafuta ushindi ambao utawafanya kufuzu hatua inayofuata mapema kabisa wakiwa kwenye ardhi ya nyumbani.
Kipute hicho cha Morocco na Mali kitapigwa uwanjani Prince Moulay Abdellah. Nani atatoboa? Zawadi zitafunguliwaje?
Lakini, kimbembe cha AFCON 2026 kwenye Boxing Day hakitaishia kwenye mechi hizo za Kundi A pekee, bali mchakamchaka utakuwapo pia kwenye Kundi B, Angola wataonyeshana kazi na Zimbabwe ya Prince Dube mwenye bao moja hadi sasa kwenye Afcon 2025, wakati kasheshe jingine litakuwa baina ya Misri ya Mohamed Salah itakayoonyeshana kazi na Afrika Kusini ya Khuliso Mudau.
Angola na Zimbabwe zitapigana vikumbo Stade de Marrakech, huku msimamo kwenye kundi hilo ukisoma timu hizo zikiwa hazina pointi yoyote baada ya zote kupoteza kwenye mechi zao za kwanza kwa mabao 2-1, ambapo Angola ilipigwa na Afrika Kusini na Zimbabwe ilichapwa na Misri. Safari hii, nani ataibuka mbabe na kukataa unyonge?
Wababe wa kundi hilo, Misri na Afrika Kusini wenyewe wataulizana maswali magumu uwanjani Stade Adrar. Hii ni mechi ngumu, ukizingatia kila timu itahitaji ushindi ili kujihakikishia kuingia raundi inayofuata bila ya presha ya kusubiri mechi ya mwisho ya hatua ya makundi. Misri ilihitaji bao la dakika za majeruhi la Mo Salah kuichapa Zimbabwe, itakuwa na shughuli pevu mbele ya Afrika Kusini, ambayo pia ina uzoefu wa kutosha wa mashindano hayo ya Afcon. Patachimbika.
MECHI ZA BOXING DAY AFCON 2025
Angola v Zimbabwe (Saa 9:30 alasiri)
Misri v Afrika Kusini (Saa 12:00 jioni)
Zambia v Comoros (Saa 2:30 usiku)
Morocco v Mali (Saa 5:00 usiku)