MZEE WA UPUPU: Kwa kauli hizi za Wanasiasa ipo kazi
NILIWAHI kuandika hapa kwenye gazeti la Juni 2020 kwenye makala iliyokuwa na kichwa cha habari cha HEKIMA YA KARIA NA KIBRI CHA NDOLANGA.
Nilikuwa najadili matukio ya wanasiasa wa Tanzania wanaojiona wako huru kusema chochote kuhusu mpira na viongozi wake.
Wanasiasa hao ambao mara nyingi ni waheshimiwa wabunge na wengine ni waheshimiwa mawaziri wamekuwa na jicho zuri sana la kuona upungufu wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na uendeshaji wa mpira kuliko hata majukumu yao muhimu.
Siku hiyo nilijadili kauli ya Waziri wa Michezo wa wakati huo, Dk Harrison Mwakyembe ya Julai 7, 2019, pale alipojitishwa jukumu lisilo lake la kumhakikishia ‘ugali’ kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, halafu siku iliyofuata wenye majukumu yao wakamtimua.
Dk Mwakyembe akapaniki na kuwataka viongozi wa TFF kwenda ofisini kwake mara moja kwa maelezo zaidi. Viongozi hao hawakwenda. Siyo kwa kumdharau, bali yeye mwenyewe kujidharaulisha.
Siku hiyo viongozi wa TFF walikuwa na ahadi ya kukutana na ujumbe mzito wa UEFA ambao ulikuwa na baraka zote za serikali kupitia wizara ya Dkt. Mwakyembe chini ya Baraza la Michezo (BMT).
Lakini TFF ya masikini ya Mungu Karia, ilia kimya kama hakijatokea kitu.
Dk Mwakyembe akagundua kwamba alikurupuka, akachutama kiungwana. Dk Mwakyembe ni mmoja wa wanasiasa wengi ambao hudhani mpira ni sehemu ya mipaka yao ya kiutawala hivyo wako huru kusema chochote.
Wakina Tarimba Abbas Tarimba ni mfano wa wabunge hao, lakini kubwa zaidi ni hili la Hussein Bashe.
Baada ya kusoma alichoandika kwenye mtandao wa kijamii, nikahisi lakini akaunti yake amefanyiwa udukuzi au simu alikuwa nayo mtoto.
Bashe ninayemfahamu ambaye ameshakuwa bosi wangu kwenye vyombo vya habari, ana busara kubwa zaidi ya aliyoionesha kwenye kile alichokiandika baada ya mchezo wa Simba na Yanga.
Wakati Bashe na wanasiasa wenzake wakiitumia vyema haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni, nimejikuta namkumbuka mzee wangu Alhaji Muhidin Ndolanga na vita zake dhidi ya wabunge kama hawa, enzi zake.
Kuelekea uchaguzi wa FAT wa 1996 Ndolanga akijiandaa kutetea nafasi yake kama Mwenyekiti, serikali ilimkata jina. Wakati huo waziri wa michezo alikuwa Profesa Kapuya.
Ndolanga hakumuogopa waziri, akasimama na kumwambia, ‘huna mamlaka ya kunitoa...nitagombea na nitashinda’.
Akapeleka malalamiko FIFA, nao wakatishia kuifungia Tanzania. Jina la Ndolanga likarudishwa, na akagombea na kushinda kwa kishindo.
Kuelekea uchaguzi wa 2005, kukawa na mgogoro mkubwa zaidi kuwahi kutokea. Ndolanga akawa kwenye ugomvi na katibu mkuu Michael Wambura.
Mkutano mkuu wa FAT ukawasimamisha wote, na nafasi zao kuchukuliwa na kamati ya muda chini ya Yahya Mhata (mwenyekiti wa Mtwara) na Mwina Kaduguda (katibu mkuu wa FRAT).
FIFA wakamtuma mwakilishi wao, Dk Joseph Misfud kujua tatizo, akatoa ripoti iliyounga mkono Ndolanga kutolewa. Ukaitishwa mkutano mkuu wa FAT wa kuipa kamati ya muda mamlaka ya kuendelea na majukumu na kuitisha uchaguzi.
Lakini cha kushangaza, mkutano huo ukapiga kura kuwarudisha Ndolanga na Wambura. Venance Mwamoto, mbunge wa Iringa, akasema Ndolanga anafaidika na mfumo mbaya wa wa FAT ambao una wajumbe 63 tu, ni rahisi kuwahonga, ndiyo maana anashinda mara zote.
Ndolanga akajibu kwamba idadi ya wapiga kura siyo tatizo kwa sababu hata wao wabunge wanahonga majimboni kwao licha ya kuwa na wapiga kura wengi.
Emmanuel Muga, mmoja wa waandishi nguli wa wakati huo, alikuwa akiziripoti habari hizi kila siku. Kwa sasa Muga ni mwanasheria...ameachana na uandishi.
Ndo nawaza hapa, angekuwa Alhaji Ndolanga, hawa wabunge wa sass wasingeachwa watambe kama wanavyotamba. Lazima kingeumana!