Musonda katikati ya mtego
KLABU ya Yanga imemsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Kennedy Musonda kutoka Power Dynamos.
Musonda amesajili kupitia dirisha dogo, ili kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa pia inatetea taji lake.
Ujio wa Musonda unaangaliwa kama utaongeza chachu kwa Yanga katika eneo la mbele ikizingatiwa inakabiliwa na michuano ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023.
Yanga ilitinga hatua hiyo ya makundi baada ya kuing’oa Club Africain ya Tunisia kwenye mechi za play-off mara ilipong’olewa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Musonda ametua Yanga akiwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Zambia, akifunga mabao 11, ikionyesha namna gani vijana wa Nasreddine Nabi wamepata jembe kwelikweli.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuthibitisha ubora wake kwenye kikosi hicho na Ligi Kuu Bara, kwani misimu kadhaa ya nyuma walisajiliwa nyota kadhaa waliokuwa vinara wa mabao walikotoka, lakini wakachemsha vibaya.
Hapa chini ni orodha ya baadhi ya wakali wa kutupia nyavuni ambao walisajiliwa katika klabu mbalimbali nchini ikiwamo Yanga na kuchemsha mapema, kitu ambacho ni kama mtego kwa Musonda katika kuhakikisha hapiti njia walizopita wenzake na kutimka kinyonge.
Dan Sserunkuma-Simba
Huyu mwamba alisajiliwa na Simba msimu wa 2014-2015, kupitia dirisha dogo akitokea Gor Mahia ya Kenya ambako alikuwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Kenya. Licha ya usajili wake kujaa mbwembwe nyingi akimchomoa aliyekuwa kinara wa mabao wa msimu wa 2013-2014, Amissi Tambwe kikosini, lakini mambo yalimwendea kombo.
Wakati anatua Simba, Sserunkuma alitoka kubeba tuzo ya misimu miwili mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya akiwa na Gor Mahia 2012-2013 akifunga mabao 17 na 2013-2014 akifunga mabao 16, huku akinyakua pia Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka 2013.
Nyota huyo kutoka Uganda, alichemsha mbaya na kuondoka Simba akiwa ameifungia timu hiyo mabao matatu tu kwa muda wote aliocheza, huku akionekana kituko zaidi kwa kushindwa kuonyesha makali uwanjani.
Cha ajabu alipoondoka Simba na kurudi Uganda, alinyakua Tuzo ya Mfungaji Bora msimu wa 2017-2018 akitupia mipira 17 kambani akiwa anaichezea Vipers, timu aliyotoka kocha mkuu wa sasa wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Laudit Mavugo- Simba
Nyota huyo wa Burundi alitua Msimbazi dirisha kubwa la mwaka 2016-2017, akitoka kuwa kinara wa mabao kwa misimu miwili mfululizo nchini kwao.
Siyo kinara wa mabao tu, lakini mara zote alizochukua Tuzo za Ufungaji Bora Burundi, jamaa alifunga mabao 32 msimu wa kwanza na ule wa pili alifunga 30 ikiwa na maana katika misimu miwili mfululizo jamaa alitupia mabao 62, kuonyesha alivyokuwa mkali na mashabiki wa Simba waliamini angewasha moto kisawasawa na kuibeba timu hiyo.
Hata hivyo, kilichotokea Mavugo aling’ara kwenye Tamasha la Simba Day aliingia kipindi cha pili na kuisaidia Simba kushinda mabao 4-1 dhidi ya AFC Leopards ya Kenya na baada ya hapo alionekana mchezaji wa kawaida sana tofauti na matarajio ya wengi ukiacha mechi chache ikiwamo ile ya kufunga bao la kusawazisha katika Kariakoo Derby kisha Shiza Kichuya kupiga bao la pili na kuipa Simba ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga iliyotangulia kwa bao la penalti la Simon Msuva, aliyekuja kuibuka Mfungaji Bora wa msimu huo.
Mavugo alishindwa kuonyesha makali na kulazimika kurudi Burundi kabla ya kuibukia Napsa Stars ya Zambia ambapo alinyakua Tuzo ya Mfungaji Bora katika hatua ya Nane Bora msimu wa 2019 kwa kufunga mabao 10.
Juma Balinya-Yanga
Huyu mwamba alisajiliwa kimafia sana na Yanga msimu wa 2019-2020 akitokea Polisi Uganda akiwa ndiye kinara wa Ligi Kuu a Uganda.
Balinya alitua Yanga na kutambulishwa kwenye Mkutano Mkuu wa Yanga wa Kubwa Kuliko akiwa ametoka kufunga mabao 19 katika Ligi ya Uganda.
Mashabiki waliamini ule moto aliokuwa nao Polisi Uganda ungehamia Jangwani, lakini kilichotokea jamaa aliondoka kinyonge kwa kushindwa kuibeba Yanga, akifunga mabao yasiyozidi matano na baadaye kuibukia Gor Mahia, akipishana na Yikpe Gnamien.
Balinya alishindwa kuonyesha makali yake na wapo walioamini soka lake lilidumazwa na mfumo wa Kocha Mwinyi Zahera ambaye kipindi hicho ndiye aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, ila cha ajabu baada ya kwenda Kenya aling’ara kabla ya kurudi Uganda kukipiga KCCA na sasa akiichezea Polisi.
Mozinzi-Azam FC
Mkali huyo wa mabao kutoka DR Congo alivivuruga vigogo wa Simba na Yanga kwa muda mrefu na kuisaka saini yake bila mafanikio kutokana na dau kubwa lililowekwa na klabu yake ya Maniema.
Hata hivyo Azam ilimbeba 2020-2021 katika dirisha dogo la msimu huo na wengi wakaamini atafanya mambo makubwa kikosi cha matajiri hao wa Bongo.
Mozinzi alishindwa kwenda na kasi ya timu hiyo na Ligi Kuu Bara na mwishowe kutemwa akiwa ameifungia timu hiyo mabao mawili tu. Ndio hujakosea mabao mawili tena katika mechi za kufungia msimu kisha akapewa mkono wa kwaheri na sasa anakipiga DC Motema Pembe ya DR Congo aking’ara.
Yahaya Mohammed- Azam
Mshambuliaji huyo wa kati kutoka Ghana, alisajiliwa na Azam msimu wa 2017-2018 kutoka Aduana Stars akiwa anatisha kwa kutupia mipira nyavuni.
Mashabiki na hata mabosi wa Azam waliamini wamepata mrithi sahihi wa Kipre Tchetche, mmoja kati ya washambuliaji wa kigeni waliowika kwa muda mrefu nchini wakikipiga katika timu hiyo.
Alisajiliwa sambamba na ndugu yake ambaye alikuwa ni beki wa kati, Yakubu Mohammed, hata hivyo tofauti na matarajio ya wengi, Yahaya alichemsha vibaya.
Licha ya kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, jamaa alishindwa kuibeba Azam kwani aliishia kumaliza msimu akifunga bao moja tu.
Yahaya aliamua kurejea chama lake la zamani la Aduana na kurejesha makali yake, japo sio kwa kiwango kile cha awali kilichowavutia Azam kumbeba jumla.
Chris Mugalu- Simba
Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo aliyekuwa akicheza soka la kulipwa Zambia alitisha na kuifanya Simba kuvunja benki kumsajili misimu mitatu iliyopita.
Akitokea klabu ya Lusaka Dynamos iliyomsajili kutoka FC Saint Eloi Lupopo, Mugalu alitarajiwa kufanya makubwa ndani ya Simba.
Hata hivyo, ni msimu wa kwanza tu aliokaribia kuwa Mfungaji Bora kama sio bao la penalti la nahodha wake, John Bocco siku ya mechi ya kufungia msimu dhidi ya Namungo kumnyima tuzo na kwenda kwa Bocco aliyemaliza na mabao 16 dhidi ya 15 na Mkongomani huyo.
Msimu uliopita ulikuwa mbaya sana kwa Mugalu, kwani alimaliza bila bao kabla ya kutemwa na kuibukia Al Quwa Al Jaw ya Ligi Kuu nchini Iraq. Nini kitakachotokea kwa Musonda?
Ni suala la kusubiri kuona ataimudu ligi kama alivyoimudu Mayele ambaye kwa misimu miwili amekuwa akifunga mabao na kuwapa raha mashabiki wa Yanga.