Prime
Muda wa kuwaudhi wazungu na Afcon yetu umefika sasa
NIMEMSIKIA Cesc Fabregas ‘akilia’ kuhusu winga wake wa kimataifa wa Senegal, Assane Diao. Hataki aende katika michuano ya Afcon kwa sababu anadai alikuwa na majeraha ya muda mrefu na ndio kwanza ametoka kupona. Fabregas ni kocha wa Como ya Italia.
Afadhali Cesc ameweka wazi, lakini Wazungu wengine huwa wananuna kisirisiri. Huu ndio muda ambao nyongo huwa zinatibuka. Muda ambao nyota wao muhimu wanakwenda zao Afcon katika michuano ya mataifa ya Afrika.
Labda ndio maana Sir Alex Ferguson alikuwa hawataki wachezaji wa Afrika. Kuna wachezaji wachache kweli kweli wa Afrika ambao waliwahi kupita Manchester United wakati Sir Alex akiwa kocha. Mmojawapo ni Eric Djemba Djemba. Hatujui kama ilikuwa bahati mbaya au vinginevyo, lakini United ya Sir Alex ilikuwa haiathiriki na michuano hii ya Waafrika.
Wachezaji wa Afrika huwa wanaharibu ‘timing’ ya wazungu na timu zao. Kwanza kabisa wengi wanakuwa muhimu katika vikosi vya wazungu. Wakiwa wanacheza wenyewe kwa wenyewe katika vikosi vya timu za taifa unawaona kama wachezaji wa kawaida. Wakienda kuchanganyika na wazungu wanakuwa watu hatari.
Hapa ndio kuna watu huwa wanasema baadhi ya wachezaji wa Afrika huwa hawajitumi wanaporudi kucheza katika timu zao za Afrika, lakini wanajituma zaidi wakicheza kwa wazungu. Kuna ukweli lakini wakati mwingine sio kweli. Wakicheza na wazungu huwa wanacheza na watu wenye akili zaidi na makali yao yanaonekana zaidi.
Didier Drogba wa Chelsea alikuwa hatari zaidi kuliko Didier Drogba wa timu ya taifa ya Ivory Coast. Huo ndio ukweli. Lakini kitu kingine kilichokuwa wazi ni kwamba hata walipokutana Drogba, Yaya Toure, Kolo Toure, Solomon Kalou na mastaa wengine wa Ivory Coast katika kikosi cha timu yao ya taifa hawakuonekana kuwa hatari sana kama walivyokuwa wanacheza katika timu za wazungu.
Wazungu akili zinawavurugika zaidi kwa sababu michuano hii inakuja kila baada ya miaka miwili na inakuja katika kipindi ambacho Ligi zimeanza kuchanganya kweli kweli. Kuna ambao wanawania ubingwa, kuna wanaowania Top Four na kuna wale wanaotaka kujikwamua kutoka chini ya msimamo wa ligi. Vichwa vinawauma.
Kuna wachache ambao wanatabasamu kama Arsenal. Mikel Arteta sijui kwa bahati mbaya au makusudi, lakini kwa sasa hana mchezaji hata mmoja kutoka Afrika. Hawezi kudhurika. Enzi za Arsene Wenger alikuwa amewajaza wengi kutoka Afrika. Kina Kolo Toure na Nwankwo Kanu.
Wafikirie ndugu zangu kama Manchester United. Wakati huu wakiwa taabani wanajitafuta ghafla Amad na Bryan Mbeumo wanaondoka kwenda Morocco. Wakiwa na Amad na Mbeumo tu bado hali ni tete, vipi wakiondoka?
Rafiki zangu Sunderland ambao wamekuwa na msimu mzuri pale England hadi sasa watapoteza zaidi ya wachezaji sita kwa ajili ya michuano hii. Sidhani kama wataendelea na makali yao wanayoonesha kwa sasa.
Wazungu hawayapendi mashindano haya. Huwa hawajitokezi na kusema wazi kwamba sababu wataonekana wabaguzi kama ambavyo tulimuona Jamie Carragher kuwa ni mbaguzi baada ya kudai kwamba Mo Salah hawezi kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Dunia kwa kushinda michuano ya Afcon.
Hata hivyo, wengi ni hisia zao za kweli kwamba hawayapendi mashindano haya. Yanaharibu ‘timing’ zao. Kuanzia kwa mabosi wa timu, mabenchi ya ufundi na mashabiki huwa hawapendi mashindano haya. Yanapora vipaji vyao vya Afrika katika wakati muhimu.
Kwa upande wa wachezaji ukweli ni kwamba kuna kundi kubwa la mastaa huwa linarudi kucheza katika michuano hii wakiwa shingo upande. Wanahofia tu kuonekana sio wazalendo. Wanaamini kwamba mkate wao halisi unapatikana katika mpira wa Ulaya au Uarabuni na sio katika timu za taifa.
Kitu kigumu zaidi kwao kwa sasa ni ukweli kwamba hawawezi kukataa kujiunga katika vikosi vyao au kuleta ukorofi wowote kwa sababu kuna baadhi yao ambao wanatarajia kushiriki michuano ya Kombe la Dunia baadaye mwakani katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
Ukijiondoa kizembe kwa sasa unaweza kuanzisha bifu na Shirikisho lako la soka au benchi lako la ufundi ukajikuta nje ya kikosi cha timu ya taifa kinachoshiriki Kombe la Dunia 2026. Hapo ndipo kuna mtego kwa baadhi ya mastaa. Ni ndoto ya kila mwanasoka duniani kucheza Kombe la Dunia.
Kwa mtazamo wangu binafsi sioni sababu za msingi za michuano hii kutofanyika Juni pindi ligi mbalimbali zinapomalizika. Huwa inatokea mara chache kwa michuano hii kuingiliana na Kombe la Dunia na hapo ndipo unapoweza kupanga ikafanyika Januari.
Kwa hali ilivyo nadhani pia michuano yenyewe inapoteza mvuto kwa sababu watu wanakuwa wanazifuatilia kwa karibu ligi mbalimbali ambako timu zao pendwa zinacheza. Tunapoteza pia mashabiki kutoka nje ya bara la Afrika.
Ni ngumu kufuatilia pambano la Tanzania na Uganda linapochezwa muda sawa na pambano la Liverpool na Arsenal. Huu ni ukweli ambao mabosi wa CAF wamekuwa wakiufumbia macho kwa muda mrefu. Ni mara moja tu michuano hii ilichezwa Juni na dunia ikafuatilia kwa karibu.
Michuano kama ya Euro au Copa Amerika huwa inafuatiliwa kwa karibu sio tu kwa sababu inakusanya mastaa wakubwa, lakini huwa inachezwa Juni wakati ligi mbalimbali zinapokuwa zimesimama. Kama Afcon ingeingia katika utaratibu huu maisha yangekuwa rahisi zaidi. Sijui kwanini CAF wanakomaa michuano hii ichezwe wakati ligi mbalimbali zinaendelea.