Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MTU WA MPIRA: Tumemsahau kabisa Himid Mao wetu

ACHANA na Mbwana Samatta. Mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya soka letu.

Samatta ameweka historia kubwa nchini. Tangu alipoondoka Simba mwaka 2011 mpaka leo hajarudi. Ni miaka 12 sasa. Ni muda mrefu sana.

Samatta aliondoka kwenda pale TP Mazembe wakati huo timu ikiwa na fedha ndefu za Moise Katumbi. Wachezaji wa Mazembe wakati ule walikuwa wakioga noti. Katumbi hakuwa anauza mchezaji kwenda popote.

Ni katika nyakati hizi Samatta alifanya mambo mengi ya msingi katika maisha yake kwa pesa za Katumbi.

Pale DR Congo alikuwa Mfalme. Mashabiki wote wa soka walimwabudu na kumkubali. Aliifanya Mazembe kuwa tishio zaidi.

Alitwaa ubingwa wa Afrika akiwa na Mazembe. Akawa mchezaji bora wa ndani Afrika akiwa na Mazembe. Aliishi katika dunia ya peke yake. Mwanadamu anahitaji nini zaidi? Hakuna.

Lakini mafanikio haya ndio yaliongeza njaa ya Samatta. Alitamani kwenda mbali zaidi ya Mazembe. Akauzwa kwenda pale KRC Genk ya Ubelgiji.

Akaanza maisha katika nyakati ngumu. Timu ilikuwa na wafalme wake. Hakupata nafasi kubwa sana katika kikosi cha kwanza katika msimu wake wa kwanza pale.

Ila kwa Samatta hii ilikuwa ni changamoto ya kawaida kwake. Alipokumbuka namna aliteseka na ufalme wa Tresor Mputu pale Mazembe wala hakuona shida.

Wakati ule Samatta anafika Lubumbashi Mputu alikuwa kama Mungu mtu. Aliabudiwa kila kona. Lakini ilimchukua Samatta miaka miwili tu kuhamishia ufalme kwake.

Ndivyo alivyoamini pale Genk. Alijua nyakati zake zaja. Na ndicho kilichotokea. Samatta aliwaongoza Genk kutwaa ubingwa pale Ubelgiji akiwa mfungaji bora wa timu.

Alipokuwa pale aligeuka Mfalme pia. Mashabiki walikuwa na nyimbo za kuisifu timu na kumsifu Samatta. Maisha yanahitaji nini tena? Hakuna .

Hata hivyo, kwa Samatta wala haikuwa jambo kubwa. Aliwaza mbali zaidi. Na ndiyo sababu baada ya mafanikio hayo akaondoka kwenda England.

Pamoja na maisha magumu pale Aston Villa, Samatta bado hakurudi nyuma. Akauzwa kwenda Uturuki na kisha akarejea pale Ubelgiji tena.

Ni wazi kuwa nyakati zake zinaelekea mwisho. Lakini nani anajali?

Samatta amefanya kile Watanzania wengi wameshindwa. Kucheza soka la kulipwa kwa miaka 12 nje ya Tanzania sio kila mtu anaweza. Ila kwa Mbwana wala haikuwahi kuwa tatizo.

Wachezaji wengi wamekwenda nje na kurudi wakati Samatta yuko palepale.

Shomari Kapombe alikwenda AS Cannes ya pale Ufaransa lakini baada ya muda mfupi akarejea. Thomas Ulimwengu alikwenda Sweden baada ya muda mfupi akapotea.

Rashid Chilunda na Farid Musa walikwenda pale Tennerife ya Hispania wakarejea. Shiza Kichuya alikwenda Misri akarejea.

Mifano ni mingi sana. Wachezaji wengi walikwenda nje maisha yakawashinda na kurejea mapema tu wakati Samatta yupo huko huko.

Ila katika wachezaji wote yupo kiungo mmoja fundi anaitwa Himid Mao Mkami.. Mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba na Mtibwa Sugar, Mao Mkami.

Huyu alikuwa mchezaji wa kutumainiwa pale Azam FC. Alikuwa kwenye kizazi cha dhahabu cha kina John Bocco na wengineo. Wakati wenzake wamechagua kwenda Simba na Yanga, Himid alikwenda Misri.

Alijiunga na Petrojet ya Misri mwaka 2018. Akacheza kwa msimu mmoja na timu yake ikashuka daraja. Ilikuwa bahati mbaya sana kwake.

Hebu fikiria unakwenda kucheza ugenini na msimu huo huo timu yako inashuka daraja? Kwa Himid wala haikuwa kikwazo.

Kutokana na kiwango bora akasajiliwa na Enppi SC. Akacheza pale kwa msimu mmoja kisha akatua Entag El Harby ya hapo hapo Misri.

Baadaye akasajiliwa na El Mahalla ya hapo hapo. Ni jambo la kuvutia sana.

Huu ni mwaka wa tano sasa Himid yuko pale Misri. Kwa sasa amekuwa Mfalme pale El Mahalla. Mashabiki sasa wanaimba na kusifu jina lake.

Wachezaji wengi walioondoka na Himid tayari wamerudi hapa nyumbani. Ni ujasiri wa hali ya juu alionao Himid.

Ni wachezaji wachache sana wanaweza kufanya kama yeye. Anastahili pongezi.