Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MTU WA MPIRA: Hata Simba wangemuuza Mayele timu kubwa

KUMEKUWA na kelele nyingi mitandaoni juu ya kuondoka kwa mkali wa mabao pale Yanga, Fiston Mayele. Na rasmi ametambulishwa katika kikosi cha Pyramid FC ya Misri. Wala sijashtuka maana nilitarajia hili mapema.

Mayele amekuwa katika kiwango bora kwa miaka yake miwili pale Yanga. Msimu uliopita alifunga mabao 16 kwenye Ligi Kuu Bara pekee. Achilia mbali mabao aliyofunga kwenye mashindano mengine.

Msimu huo alimaliza kama mfungaji bora namba mbili nyuma ya George Mpole aliyekuwa na mabao 17. Alikua katika kiwango bora sana.

Msimu uliopita 2022/23 akawa mfungaji bora kwa mabao 17 sawa na Saido Ntibazonkiza wa Simba. Huu ulikuwa msimu bora zaidi kwake. Alivuka idadi ya mabao aliyofunga katika msimu wa kwanza.

Kwenye mechi za CAF huko ndio biashara yake ilikaa vizuri zaidi. Alifunga mabao saba kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na kuwa mfungaji bora. Inavutia sana.

Kabla ya hapo alikua amefunga mabao kama hayo kwenye mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na Al Hilal ya Sudan na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika.

Nani amesahau lile bao bora aliloifunga Al Hilal hapo kwa Mkapa wakati Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1? Ni ngumu kusahau.

Mayele alifunga bao la umbali mrefu kwenye mchezo huo mgumu. Aliwaamsha Wananchi kwa shangwe kubwa.

Mbali na mabao aliyofunga, Mayele alicheza kwa kiwango bora sana katika michezo ya CAF. Aliwafanya mabeki wa timu pinzani kile alichojisikia. Inafurahisha sana. Huyu ni fundi wa mpira haswa.

Kwa msimu wa kwanza kwenye Ligi ya Tanzania aliingia kwenye kikosi bora. Aliteuliwa pia katika orodha ya wachezaji watatu waliokuwa wakiwania tuzo ya mchezaji bora wa msimu. Bahati mbaya ilikwenda kwa Yannick Bangala.

Msimu uliopita akashinda tuzo hiyo. Wachambuzi na mashabiki wote wa soka nchini walikubali kuwa Mayele alistahili tuzo hiyo. Alikuwa katika kiwango bora sana.

Ni katika msimu huu ambapo Mayele aliitwa Timu ya Taifa ya DRC. Akapata nafasi ya kucheza na kufunga moja ya mabao mazuri sana.

Ni jambo gumu kwa mchezaji kutoka Ligi ya Tanzania kuitwa Timu ya Taifa ya DR Congo lakini Mayele amepata nafasi hiyo mara kadhaa. Ameitwa na akacheza tena kufunga bao. Ni historia kubwa sana kwa ligi yetu.

Huwa inatokea mara chache. DR Congo ina utajiri mkubwa sana wa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa Ulaya na maeneo mengi duniani. Ila Mayele alipenya katikati yao.

Ni wazi kuwa alikuwa katika kiwango bora zaidi cha maisha yake ya soka. Watanzania wameona. Wakongo wameona. Afrika imeona.

Katika nyakati kama hizi ilikuwa wazi kuwa ni ngumu kumzuia Mayele asiuzwe kwenda timu nyingine kubwa zaidi ya Yanga.

Ndio biashara ya soka ilivyo. Ni jambo gumu kwa timu ndogo kukaa na mchezaji mkubwa kwa muda mrefu. Timu zenye fedha siku zote hutegemea kununua wachezaji mahiri kutoka timu za kawaida.

Sisemi kwamba Yanga ni timu ndogo sana. Hapana. Ila kwa Afrika zipo timu nyingi kubwa na zenye msuli wa fedha zaidi yao. Timu kutoka Afrika Kusini, Angola na Kaskazini mwa Afrika zina fedha nyingi.

Timu hizi hutumia fedha zao kununua wachezaji wa timu za madaraja ya kati. Unafikiri leo Mamelodi Sundowns, Kaizer Chiefs, Al Ahly, Pyramids, Zamalek, ama Wydad Casablanca zikimtaka mchezaji wa Yanga wanaweza kukataa?

Ni ngumu sana. Ni ngumu kama vile mchezaji wa Dodoma Jiji kuzigomea Simba na Yanga. Hapa kinachoongea ni fedha.

Pia, wachezaji wakishafanya vizuri sehemu fulani wakiona fursa ya kuondoka huwa wanalazimisha jambo lao lifanikiwe. Ndio sababu tunasikia Mayele ndiye amelazimisha kuondoka katika dirisha hili.

Mayele kama walivyo wachezaji wengi wanaamini kuwa muda wa kuondoka ni pale unapokuwa katika kilele cha ubora wako. Wako sahihi.

Mayele ameshakuwa Mfungaji Bora na Mchezaji Bora wa ligi yetu. Amekuwa Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa Yanga. Haoni sababu ya ziada ya kuendelea kusalia akiwa hapo.

Anaamini ni muda sahihi kwake kupata timu kubwa zaidi ya Yanga. Yupo sahihi kabisa.

Ni kama ilivyokuwa kwa Luis Miquissone na Clatous Chama kwa wakati ule. Walipofanya vizuri na Simba kwa wakati ule waliamini wanastahili kwenda sehemu kubwa zaidi.

Miquissone akaenda kwa mabingwa wa Afrika, Al Ahly na Chama akaenda RS Berkane. Simba ikavuna mabilioni ya fedha kwa mauzo yao.

Sisemi kama Mayele atafanikiwa ama atafeli huko anakokwenda ila ni wakati sahihi kwake kupata timu kubwa zaidi ya Yanga. Na yeye ameliona hilo.

Ndivyo ambavyo huwa tunawaambia wachezaji wetu kila siku. Unapokuwa katika kilele cha ubora wako ndio muda sahihi wa kuondoka kwenda kupata changamoto mpya nje.

Bahati mbaya wengi huwa hawasikilizi hilo. Wanaamini zaidi katika Simba na Yanga. Kwao ndio mafanikio makubwa zaidi. Ila kwa wachezaji wenye ndoto kubwa kama Mayele wanapamana kufika mbali zaidi. Na ndiyo sababu anaondoka Yanga.

Ukweli ulioko wazi ni kuwa anaacha pengo kubwa pale Yanga. Wana mtihani mzito wa kuziba nafasi yake. Ni ngumu kupata straika aina ya Mayele sokoni. Mchezaji mwenye kasi, utulivu na mpira, uwezo wa kupiga chenga na kufunga. Ni ngumu kama kuvunja nazi kwa mkono.

Yule Kennedy Musonda ni mfungaji mzuri. Lakini kwa uwezo ameachwa mbali sana na Mayele. Hapa sasa ndio kwenye mtihani mkubwa kwa Yanga.