MTU WA MPIRA: Ajibu amepiga hatua moja mbele, kumi nyuma

IBRAHIM Ajibu. Kipaji kikubwa cha soka katika zama hizi. Fundi haswa. Ukimtazama anakufanya uone soka ni kazi rahisi sana.
Wakati anachipukia pale Simba watu walimtabiria makubwa. Alitazamiwa kufika mbali kama vile Mbwana Samatta na wengineo. Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti sana.
Siku zote tumekuwa tukikubaliana juu ya ukubwa wa kipaji cha Ajibu. Bahati mbaya ameshindwa kuwa mchezaji mkubwa.
Majuzi Coastal Union ya Tanga imemtangaza kuwa nyota wao mpya. Inashangaza sana. Ajibu ni mchezaji wa kucheza Coastal Union leo? Hapana. Kuna kitu hakipo sawa.
Wakati Samatta akiendelea kuzurura kwenye timu za Ulaya, Ajibu amezidi kupiga hatua 100 nyuma. Sina maana kuwa Coastal Union ni timu ndogo, hapana na wala sina nia ya kuishusha hadhi. Ila Ajibu hakupaswa kuwa huko leo hii.
Nakumbuka aliyewahi kuwa Kocha wa Simba, Dylan Kerr aliniambia kama enzi zake angekuwa na kipaji kama cha Ajibu, angeweza kucheza Manchester United.
Ila akasema Ajibu hataweza kufika huko kwasababu haweki juhudi katika kipaji chake. Hili ndiyo limekuwa tatizo kubwa la Ajibu siku zote. Anaamini kuwa anajua sana, hivyo hana haja ya kuweka juhudi kubwa.
Si mpenzi wa mazoezi. Ni mchezaji anayeishi maisha kama ya Bongo Fleva. Anafanya mazoezi kidogo, anatumia muda mwingi zaidi kupumzika.
Pamoja na ukubwa wa kipaji chake, Ajibu amewahi kuwa kwenye kilele cha ubora wake kwa misimu miwili tu. Alipohama kutoka Simba kwenda Yanga.
Aliitendea haki miaka yake miwili pale Yanga. Akaongoza kwa kupiga pasi za mabao kwenye ligi. Alifunga mabao muhimu pale Yanga.
Ni wakati huu ambao TP Mazembe ikiwa kwenye kilele cha ubora wake ilitaka kumsajili, lakini akachagua kurejea Simba. Ikawa mwisho wake.
Hakuweza kurejea tena katika ubora wake pale Simba. Na tatizo lilikuwa lilelile. Hajitumi uwanjani wala mazoezini. Kocha gani anapenda mchezaji mvivu? Hakuna.
Kuna wachezaji wengi nchini ambao Ajibu amewazidi kipaji lakini wamefanikiwa kuliko yeye. Mfano mzuri ni huyu Mzamiru Yassin. Si mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana, lakini anajituma sana.
Mzamiru anacheza kwa juhudi kubwa mazoezi. Akifika kwenye mechi anajituma zaidi. Ndiyo sababu kwa miaka saba sasa makocha wote wanaofika pale Simba wamekuwa wakimtumia kama chaguo la kwanza.
Mwingine ni Himid Mao. Hana kipaji kikubwa kama cha Ajibu. Hata hivyo, amekuwa akijituma sana mazoezini na kwenye mechi. Anaifanya kazi yake vyema sana. Ndiyo sababu sijastaajabu kuona anazidi kubadilisha timu pale Misri kila msimu.
Anachoambiwa afanye uwanjani ndicho ambacho anakifanya. Yuko fiti kucheza kwa dakika zote bila kuchoka. Kwanini? Ni kwasababu anajituma sana kwenye uwanja wa mazoezi.
Mfano mwingine ni huyu Saimon Msuva. Hana kipaji kikubwa sana kama cha Ajibu, lakini amefanikiwa sana. Ametamba pale Morocco na kule Saudi Arabia.
Msuva siku zote amekuwa ni mtu wa kufanya mazoezi sana. Hata kama timu haina ratiba ya mazoezi, utamkuta akifanya ya peke yake. Ajibu hawezi kufanya hivi.
Ndiyo sababu Simba iliamua kuachana naye. Nikaishangaa Azam FC ilipomsajili wakati ule. Iliamini kwenye kipaji chake, lakini kwenye uwanja wa mazoezi akawaangusha. Muda mwingi hakuwa kambini na wachezaji wenzake. Unawezaje kumbadilisha mchezaji wa hivi? Ni ngumu sana. Ndicho ambacho pia kimeikuta Singida Fountain Gate ambao imemuacha tu baada ya nusu msimu.
Ingefanya nini zaidi? Ni kweli ni mchezaji mzuri lakini hajitumi kama wenzake. Ikampa mkono wa kwaheri.
Kwa Coastal Union nayo im eamini pia kwenye kipaji cha Ajibu. Lakini kama hatabadilika sioni akiongeza kitu kikubwa kwenye timu yao.
Mchezaji yeyote mzuri anatakiwa kuwa na juhudi kubwa za mazoezi pia. Hawa kina Leonel Messi, Cristiano Ronaldo na wengineo licha ya vipaji vyao wanafanya sana mazoezi. Wanapambana katika kila mchezo.
Vipi kwa mchezaji wa Kitanzania ambaye ana kipaji ila hafanyi mazoezi ya kutosha? Hawezi kufika popote. Ndivyo ambavyo tumekipoteza kipaji cha Ajibu mapema sana. Acha tumuone Ajibu chini ya Kocha Mwinyi Zahera atatamba tena uwanjani?