Prime
Mtihani mgumu unaomkabili Barker Simba
KIBARUA alichonacho Kocha Steve Barker cha kuirejesha Simba kwenye ufalme wake nchini na kuendelea kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa sio mchezo, kinawakilisha kipimo halisi cha uwezo wa kocha katika mazingira magumu.
Kutoka Stellenbosch ya Afrika Kusini ambayo haikuwa na presha kubwa ya ushindani hadi klabu yenye matarajio makubwa kama Simba yenye ukame wa misimu minne bila ubingwa wa ligi, Barker amejikuta katika kibarua kizito cha kusimamia timu iliyokosa mwelekeo mzuri kiuchezaji na matokeo chini ya Dimitar Pantev ambaye alimalizana na miamba hiyo wiki chache zilizopita.
Kuingia wakati msimu umeanza katika klabu inayopigania mataji ya ndani na heshima ya kimataifa kunamhitaji kocha mwenye uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka, kusimamia kuvimba kichwa ‘egos’ kwa baadhi ya wachezaji na kurejesha mfumo wa ushindani ndani ya muda mfupi.
Licha ya kwamba, Simba ilikosa baadhi ya wachezaji wake katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar haikuonekana kucheza kwa njaa ya kutafuta matokeo kitu ambacho pia kilionekana katika michuano ya Mapinduzi visiwani Zanzibar.
MICHUANO YA MAPINDUZI
Michuano ya Mapinduzi ilikuwa hatua ya kwanza kwa Barker kuanza kutathmini Simba kwa undani. Ingawa michuano hii haiko kwenye kiwango cha Ligi Kuu au Ligi ya Mabingwa Afrika, bado ni sehemu kwa kocha kujaribu mbinu, uchezaji wa wachezaji na kuona ni nani anayeweza kushirikiana vizuri na nani anaye hitaji msaada wa ziada.
Hata hivyo, kilichoonekana katika michuano hiyo kilikuwa ni picha halisi ya changamoto, Simba ilionekana kucheza bila mwelekeo maalum na mara nyingi wachezaji walionekana kuzunguka kutoka upande mmoja wa uwanja hadi mwingine bila kusababisha hatari kwa mabeki timu pinzani.
Safu ya kiungo ya Simba, ambayo mara nyingi imekuwa kiini cha kuendesha mashambulizi, ilionekana haina ubunifu wa kutosha, huku washambuliaji wakikosa msaada wa kutosha wa kuunda nafasi.
Kitu kama hicho kilitokea katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa kocha huyo wakati Simba ikitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, angalau katika dakika 45 za kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili walionekana kupoteza mwelekeo kiasi cha Mtibwa kurejea mchezoni.
NJAA YA USHINDI
Changamoto kubwa kwa Barker ni jinsi ya kuhamasisha wachezaji ambao wamepoteza hamasa ya kushindana. Simba ya sasa haionekani kuwa na ile njaa ya kutafuta matokeo ambayo ilitambulisha timu hii miaka michache iliyopita. Mechi za Mapinduzi zilionyesha kuwa wachezaji walicheza kama ni lazima tu, badala ya kuonyesha shauku ya ushindi.
Hali hii ilitokana na mchanganyiko wa matokeo mabaya, presha ya mashabiki, na mara nyingi kuingia kwa mabadiliko ya kocha bila mpangilio. Barker anatakiwa kuanza kazi ya kurekebisha hali hii, kuhakikisha kila mchezaji anaamini kuwa bado kuna nafasi ya kufanya vizuri na ushindi ni jambo linalowezekana.
Bila kuweka msingi huu, mbinu yoyote ya kiufundi inaweza kuwa sawa na kazi bure.
SAFARI YA MPITO
Simba ilianza kampeni ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu katika hatua ya makundi chini ya Dimitar Pantev lakini matokeo mabaya yalimhukumu mapema. Kipigo cha nyumbani cha bao 1-0 dhidi ya Petro de Luanda kilikuwa pigo kubwa, ikizingatiwa Simba mara nyingi imekuwa imara nyumbani.
Kipigo hiki kilifuatiwa na kipigo kingine ugenini, ambapo Stade Malien waliwashinda Bamako kwa mabao 2-1. Matokeo haya mawili yalisababisha wasiwasi mkubwa ndani ya uongozi na mashabiki na hatimaye kufanya uongozi wa klabu kumalizana naye.
Hapo ndipo Barker alipoingia. Kuingia kocha mpya katikati ya msimu ni changamoto kubwa zaidi kuliko kuanza mapema, kwani timu tayari imekuwa na muundo maalum wa kiufundi. Barker anakabiliana na hali na ni lazima achambue haraka, afahamu nguvu na udhaifu wa kila mchezaji na kubadilisha mtindo wa uchezaji kwa haraka ili kupata matokeo yanayohitajika.
MSIMAMO WA KUNDI D
Hadi sasa, Simba inaburuza mkia katika kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo.
Kundi hilo linaongozwa na Petro de Luanda yenye pointi nne, sawa na Stade Malien ya Mali, huku Esperance Tunis ikiwa nafasi ya tatu kwa sababu ya sare mbili mfululizo.
Hali hii inafanya mechi dhidi ya Esperance kuwa kama fainali. Simba haina nafasi ya kufanya makosa na kila mchezaji na kocha wanapaswa kufanya zaidi ili kuweka hai matumaini yao.
Hii ni presha ya aina tofauti, kwa sababu wachezaji wanajua ushindi dhidi ya Esperance unaweza kuwa sehemu ya kuanza kurekebisha historia yao ya matokeo mabaya, wakati kushindwa kunaweza kukoleza moto hali iliyopo.
SAFARI YA TUNISIA
Simba imeenda Tunisia kwa ajili ya mechi dhidi ya Esperance Tunis, itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi, ingawa wenyeji hawapo katika kiwango cha juu msimu huu, bado ni timu yenye wachezaji wenye uzoefu mkubwa na ubora wa kiufundi.
Barker anatakiwa kuandaa Simba ipasavyo kuhakikisha timu inacheza kwa nidhamu ya hali ya juu, inashirikiana vizuri kati ya safu ya ulinzi na viungo na kuunda nafasi kwa washambuliaji.
Mbinu za kiufundi pekee haziwezi kutosha lazima pia kuwe na motisha kwa wachezaji ambao nao wanapaswa kuamini kuwa wanaweza kushinda, hata wakicheza ugenini dhidi ya timu yenye historia ya kutwaa mataji manne ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika miaka ya 1994, 2011, 2018 na 2019.
CHANGAMOTO ZA UCHEZAJI
Barker anatakiwa kufanya mabadiliko kadhaa kwanza, kuchagua safu ya wachezaji wenye uwezo wa kukabiliana na presha ya mechi kubwa.
Pili, kuanzisha mfumo wa uchezaji unaojumuisha ushirikiano kati ya kiungo na washambuliaji. Simba mara nyingi imekuwa na tatizo la washambuliaji kutumia vizuri nafasi. Barker anatakiwa pia kuwa na mpango wa B au C pale inapohitajika.
Mbinu hizi hazitoshi bila kuhamasisha morali ya timu. Kocha lazima awe aongeze morali ya ushindani kwa wachezaji, kuhakikisha kila mchezaji ana nia ya kupigana hadi dakika ya mwisho na hakuna mchezaji anayecheza kwa sababu tu ya ratiba, bali kwa sababu ana ndoto ya kushinda.
HAKUNA NAMNA
Simba inahitaji kurejesha utambulisho wake wa awali, timu inayoshindana, yenye nidhamu, yenye nguvu na yenye akili za kushinda. Barker, ingawa ana changamoto kubwa, anayo nafasi ya kuunda timu ambayo itacheza kwa heshima ya nembo, ikiwa na nguvu ya kuunda mashambulizi na ushirikiano mzuri kati ya safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji.
Hii itahitaji muda, uvumilivu na kazi kubwa ya uongozi katika kusapoti maono yake kimbinu na timu.
Wachezaji wanapaswa kuamini kupitia kocha mpya na mashabiki wanapaswa kuonyesha mshikamano ili kusaidia kurejesha morali ya timu.
SAFARI NDEFU
Kwa ujumla, Barker ana kibarua kizito cha kuirudisha Simba kwenye reli. Kuanzia Mapinduzi hadi sasa, dalili zinaonyesha timu inayopitia kipindi cha mpito kigumu. Mechi dhidi ya Esperance Tunis si tu mtihani wa kuonyesha vile hawapo mbali na hilo.
Iwapo Simba itaonyesha njaa ya ushindi, nidhamu na mshikamano, hata kama matokeo hayatakuwa vile wanataka, kutakuwa na ishara za matumaini.
Hata hivyo, kama hali ya kupoteza umakini, morali ya timu itaendelea kuwa chini basi safari ya Barker itakuwa ndefu, ngumu na yenye miiba.