MSIMU: Kuna Pacome halafu Mpanzu si mchezo
Muktasari:
- Akitokea timu ya U-20 na kupandishwa moja kwa moja kwenye timu ya wakubwa msimu wa 2023-24, Msimu ameendelea kuonyesha nidhamu, juhudi na uwezo mkubwa katikati ya uwanja.
MIONGONI mwa viungo wanaofanya vizuri kwenye kikosi cha Coastal Union ni pamoja na Bakari Msimu ambaye ni msimu wake wa tatu kuitumikia timu hiyo akipandishwa kutoka kikosi cha vijana.
Akitokea timu ya U-20 na kupandishwa moja kwa moja kwenye timu ya wakubwa msimu wa 2023-24, Msimu ameendelea kuonyesha nidhamu, juhudi na uwezo mkubwa katikati ya uwanja.
Alianza kama mchezaji wa akiba, lakini kutokana na bidii na maelekezo kutoka kwa makocha, aliweza kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza mwishoni mwa msimu huo.
Baada ya kupandishwa msimu wa 2024-25 akakabidhiwa kitambaa cha unahodha na kuiongoza Coastal kubali Ligi Kuu akifunga mabao manne na kutoa asisti tatu.
Nahodha huyo anasema haikuwa rahisi kwake kufikia hatua hiyo, lakini anajivunia kujifunza mambo mengi chini ya makocha mbalimbali waliompa nafasi ya kukua kisoka.
Kuanzia kwa kocha Mkenya David Ouma aliyeipeleka Coastal kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka 2022, Juma Mwambusi, Joseph Lazaro, Ali Mohammed Ameir na sasa Mohamed Muya bado ameendelea kupata nafasi.
“Sio jambo rahisi kupata nafasi ya kuanza kwa timu kama Coastal kwa sababu ni timu kubwa na yenye historia kubwa kwenye soka la Tanzania, naamini juhudi zangu zimefanya makocha hao wote kuniamini na kunipa nafasi,” anasema Msimu.
Mwanaspoti lilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano kujua safari yake kisoka, changamoto alizokutana nazo na ndoto zake.
MBILI HATAZISAHAU
Nahodha huyo anaeleza mechi mbili ambazo hatazisahau ni pamoja na ile ya waliyocheza dhidi ya Yanga Arusha na kupoteza kwa bao 1-0, ilihali waliamini watapatan ushindi kulingana na mbinu za kocha alizowapatia.
“Mechi ilikuwa ngumu sana tulijitahidi kukaba na kuzuia, lakini ndio hivyo Yanga nayo ilikuwa inahitaji kushinda kwa hiyo kila dakika lango letu lilishambuliwa hatukuwa na hata dakika ya kupumua,” anasema Msimu.
Anaongeza mechi nyingine ambayo hataisahau ni dhidi ya Dodoma Jiji ambayo alicheza dakika 70 ikiwa mechi yake ya kwanza tangu alipopandishwa akitokea timu ya vijana.
“Nakumbuka aliyetakiwa kuanza alipata shida ghafla kwa hiyo tulikuwa vijana kama watatu tunafanya mazoezi na timu ya wakubwa nikachaguliwa kuanza mechi hiyo, kiukweli nilikuwa na wasiwasi kidogo, lakini kuna kaka zangu walionitangulia walinipa moyo na kuniambia naweza na kweli nikaonyesha uwezo wangu.
“Kwa hiyo tangu siku ile nilikuwa nimeaminiwa kidogo siku nyingine nikawa nacheza, siku nyingine nikwa sipo kabisakikosini na nyingine nilikuwa nakaa benchini tu. Nikawa najituma mazoezini hadi nikapewa nafasi moja kwa moja ya kuanza.”
SAFARI YAKE
Anasema tangu akiwa mdogo alikuwa akicheza mpira mitaani lakini kwenye soka la ushindani Coastal Union ndio timu ya kwanza kumtambulisha.
Anaongeza kuwa kiwango alichoonyesha kwenye michuano ya vijana kilimfanya kuonekana na benchi la ufundi la timu kubwa lililompa nafasi ya kupandishwa rasmi msimu wa 2023-24.
“Coastal ndio timu ya kwanza kucheza kwa hiyo hapa ndipo nimejifunza soka la ushindani kuanzia timu ya vijana U-17 na U-20 hadi nikapandishwa timu ya wakubwa.”
TAIFA STARS
Miongoni mwa matamanio makubwa ya winga huyo ni kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars kwa mafanikio makubwa akiamini ana uwezo wa kucheza muda ukifika.
“Timu ya taifa ni kwa wachezaji wote mimi bado kijana mdogo na naamini muda wangu ukifika nitacheza na nitaonyesha kiwango kizuri ili niweze kuisaidia timu yangu na mimi pia kwa sababu ni sehemu ya kujiuza,” anasema Msimu ambaye mwaka jana alikuwa sehemu ya nyota wa Ngorongoro Heroes walionyakua ubingwa wa CECAFA U-20 dhidi ya Kenya.
PACOME, MPANZU
Nahodha huyo anasema anajifunza vitu vingi kwa nyota wa Yanga, Pacome Zouzoua na Elie Mpanzu wa Simba kwa aina yao ya upambanaji inayoweza kubadilisha matokeo ndani ya dakika chache.
“Pacome ni mchezaji mzuri ambaye nafikiri asilimia kubwa ya wachezaji wanamtazama na kujifunza vingi, binafsi nacheza nafasi moja naye winga hivyo huwa namuangalia anapocheza muda mwingine nachukua ujuzi wake,” anasema Msimu
“Mpanzu amekuja Tanzania akacheza nusu msimu lakini kila mmoja aliona ubora wake akaisaidia Simba kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa hiyo ni wachezaji wazuri ninaowatazama sana na kuiga vitu wanavyofanya.”
Msimu anamtaja nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta kuwa moja ya wachezaji wa Kitanzania wanaoliwakilisha vyema taifa hili kwa kuweka rekodi mbalimbali Ulaya. “Tangu tukiwa wadogo wengi tumemtazama kama mchezaji anayetuhamasisha sana kwa aina yake ya upambanaji. Kila anapokwenda anaacha rekodi hilo ni jambo kubwa,” anasema nahodha huyo na kuongeza:
“Mimi natamani nifikie mafanikio yake au zaidi kwa sababu hata hapa malengo yangu baada ya kuizoea Ligi Kuu basi nitoke nje kucheza au Simba na Yanga kwa sababu ni sehemu ya kujiuza kutokana na ukubwa wao Afrika.”
FEI TOTO, CHASAMBI
Anasema mbali na Samatta wachezaji wa Kitanzania anaowakubali wanaofanya vizuri Ligi Kuu ni Ladack Chasambi wa Simba na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC.
“Nimewataja hao kwa sababu ni wachezaji wenye vipaji vikubwa, Fei akiwapo uwanjani basi lile eneo la kiungo analitawala sitashangaa kumuona akiendelea kuchukua nafasi Azam kwa sababu ni mchezaji anayekupa vitu vingi,”
“Ingawa Chasambi hapati nafasi Simba lakini nimekuwa nikimtazama na tumewahi kukutana hasa kwenye mashi-ndano ya vijana, ni mchezaji mzurii pia akipata nafasi ataonyesha uwezo wake.”
Nje ya soka, mchezaji huyo anasema anapenda kufanya ibada.
“Mimi napenda kufanya mazoezi sana nikiwa nyumbani kufanya ibada na kupumzika sana sijui kwa sababu ni mambo ya soka lakini niko hivyo sio mtu wa bata,” anasema na kuongeza:
“Napenda kuwekeza kwenye mambo ya biashara hilo ni moja ya malengo yangu makuu, kwa hiyo nikiendelea kucheza naweza kufungua biashara yoyote ile halali.”