Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MR LIVERPOOL: Hii Liverpool inahitaji kufanyiwa kisomo aisee

SIJUI kama mmiliki wa klabu ya soka ya Liverpool ya England, John W. Henry au Kocha Mkuu, Jurgen Klopp, wamewahi kusikia utaratibu wa kile sisi watu wa Pwani hupenda kuita kisomo. Majogoo hao wa Anfield wanahitaji huduma hiyo.

Kile kinachoipata klabu hiyo kwa sasa, ndani na nje ya uwanja ni kitu ambacho sijawahi kusikia kimetokea kwa klabu yoyote ile hapa Tanzania au nje ya nchi. Nami si kijana mdogo kwani nimeanza kufuatilia soka kabla Marcus Rashford wa Manchester United hajazaliwa.

Hebu fikiria kidogo.

Ili Liverpool icheze kwenye ubora wake, inamtegemea mlinzi wake Virgil van Dijk afanye mambo yake. Mholanzi huyo huifanya timu isogee mbele kidogo kwa sababu anajua anaweza kukimbizana na washambuliaji wenye kasi.

Yeye pia ni mzuri wa mipira ya juu na hivyo wale watakaotaka kupitia mbinu ya mipira ya juu hukutana na mtu ambaye mipira hiyo kwake ni kama chai ya asubuhi tu.

Kubwa zaidi, Virgil ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi ndefu. Maana yake ni kwamba wakati ambapo Liverpool inashambuliwa, hasa kwenye mechi kubwa, huwa pia ndiyo wakati hatari zaidi kwa wanaoshambulia. Hii ni kwa sababu, pasi moja tu ya umbali wa mita 40 hubadili kushambuliwa kuwa nafasi ya kufunga.

Ni mlinzi ambaye hapati shida kupeleka mpira anapotaka uende. Katika klabu ambayo ina washambuliaji wenye kasi kama Sadio Mane na Mo Salah, hii ni silaha muhimu katika timu.

Huyu ndiye kiongozi wa safu ya ulinzi ya Liverpool. Katika timu pia, uwepo wake ni muhimu kwa sababu anapokuwepo, timu nzima hutulia. Sasa unajua nini kimetokea mwaka huu? Mlinzi huyo ameumia na klabu haitarajii kama atacheza tena msimu huu.

Anapokuwa hayupo, mlinzi ambaye wanakaribiana naye kwa mengi na pacha wake kwenye safu ya ulinzi ni Joe Gomez. Huyu ni mlinzi kijana ambaye kiwango chake kimepanda sana kwa kucheza na Van Dijk mfululizo.

Wiki mbili tu baada ya kuumia kwa Van Dijk, Gomez naye akaumia. Na hakuumia kwa wiki mbili au tatu. Hapana, majeraha yake ni ya muda mrefu kiasi cha kutotarajiwa kucheza tena kwenye ….eenhe msimu huu wote.

Unajua nani ni kiraka wakati Gomez na Virgil wanapokuwa hawachezi? Ni raia mmoja wa Cameroon aitwaye Joel Matip. Sasa ngoja nikwambie nini kimemkuta naye. Kapata majeraha na hatarajiwi tena kucheza msimu huu.

Kichekesho ni kimoja. Baada ya kuona walinzi wake wanaumia mara kwa mara, Klopp akaamua kumsajili Ben Davies kutoka Preston. Katika siku yake ya nne mazoezini, naye akaumia kidogo.

Lakini upepo huu mbaya haujaishia hapo tu. Wakati watu hao wakiumia, Liverpool haikuwa ikicheza vizuri sana lakini ilikuwa ikipata ushindi wa hapa na pale. Mchezaji aliyekuwa akiikoa timu kwa kufunga mabao muhimu alikuwa akiitwa Diogo Jota.

Wakati akiwa kwenye fomu na akifunika mapengo ya kina Salah, Mane na Bobby Firmino waliokuwa chini ya kiwango, Jota akaumia katika mechi dhidi ya Midjtyland ya Denmark. Majeruhi hayo yamemuweka nje kwa walau miezi mitatu sasa.

Klopp akaona namna pekee ya kuziba pengo la akina Gomez ni kumrudisha Fabibho kwenye safu ya ulinzi. Baada ya kufanya kazi nzuri kwenye eneo hilo, raia huyo wa Brazil naye aliumia na sasa yuko kwa madaktari akitibiwa.

Akabaki nahodha na kiungo muhimu zaidi wa Liverpool. Yeye naye akarudishwa kwenye ngome ili aiongoze timu kutokea nyuma kwa sababu ya uzoefu wake. Wiki hii naye kaumia na inasemwa atakuwa nje kwa muda wa takribani wiki 12. Hiyo ni sawa na miezi mitatu.

Wataalamu wanaofahamu kuhusu tatizo lake la misuli ya paja wanasema huenda asicheze tena msimu huu. Huyu ni mchezaji ambaye uzoefu na uwepo wake kwenye timu ni muhimu kwa sababu ndiye hasa kiongozi wa wachezaji wote.

Halafu yanatokea mambo mengine nje ya uwanja. Mwezi uliopita, Klopp alifiwa na mama yake, Elisabeth, na kwa sababu ya matatizo ya ugonjwa wa Corona, ameshindwa kusafiri kwenda kumzika mzazi wake huyo.

Labda watu hawajui nini maana ya msiba huu. Kwa waliowahi kusoma kitabu kuhusu historia ya maisha ya Klopp kilichoandikwa na mwandishi wa Kijerumani, Raphael Honigstein, kiitwacho Bring the Noise, watafahamu kuwa kocha huyu alikuwa na uhusiano wa kipekee na mama yake. Yeye ndiye mtoto pekee wa kiume katika familia yenye mabinti wengine wawili; Isolde na Stefanie.

Kwa watu wazima, na kwa wale wanaofahamu historia ya eneo la Swabi (Black Forest) kule alikozaliwa Klopp, wataelewa mapenzi ya mama kwa mtoto pekee wa kiume na tena wa mwisho.

Na juzi Liverpool imepata taarifa za msiba wa baba mzazi wa mlinda mlango wake namba moja, Alisson Becker. Huyu ndiye mchezaji ambaye usajili wake uliibadili Liverpool kutoka kuwa washindani wa Man City hadi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Ulaya na Dunia kwa ujumla.

Sijawahi kuona kitu kama hiki. Liverpool inahitaji kisomo wallahi.


Imeandikwa na Ezekiel Kamwaga