Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Morocco: AFCON hii tutawaonyesha, Msuva atia neno

Muktasari:

  • Katika michuano hiyo itakayoanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini Morocco, Taifa Stars imepangwa kundi C na nchi za Nigeria, Tunisia na Uganda.

WAKATI Watanzania wakiendelea kulipigia hesabu ndefu kundi la timu ya tifa ‘Taifa Stars’ katika michuano ya Afcon 2025, kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ametoa mtazamo wake wa namna watakavyokiandaa kikosi kwenda kushindana na sio kushiriki pekee.

Katika michuano hiyo itakayoanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini Morocco, Taifa Stars imepangwa kundi C na nchi za Nigeria, Tunisia na Uganda.

Morocco alisema hakuna kundi gumu kwenye droo hiyo aliyoishuhudia ikipangwa juzi Jumatatu nchini Morocco akiwa na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ sambamba na viongozi na maofisa wengine wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakiongozwa na rais Wallace Karia na makamu wake Athuman Nyamlani.

Morocco alisema Watanzania hawatakiwi kuogopa kwani Stars nayo inahitaji kuheshimiwa na mataifa mengine kwa kuwa imeshatoka kwenye unyonge wa miaka ya nyuma.

“Kwangu sijaona kundi rahisi likiwemo hili letu - yote ni magumu. Tanzania sio wanyonge nipo hapa Morocco na makocha mbalimbali ukijitambulisha unatoka Tanzania wanaheshimu sana na hata baada ya droo unaona washindani wetu wanatafakari kwa kina,” alisema Morocco na kuongeza:

“Tanzania imeshatoka kwenye enzi za unyonge tunatakiwa tujiamini kama Taifa kwamba tunaweza kufanya kikubwa. Miaka ya nyuma tulikuwa tunakuja kama wasindikizaji, fainali zilizopita tukafanikiwa kupata pointi kwenye makundi. Safari hii tunataka kuja kushindana kutafuta nafasi mbili za juu kwenda mbali.”

Kocha huyo alisema kwamba kundi hilo lina timu mchanganyiko ambapo wanarudi kuanza mikakati ya kina kuhakikisha kwamba Taifa linafikia malengo.

“Ukilitazama kundi letu kuna timu za Afrika Magharibi, Afrika Kaskazini na sisi Afrika Mashariki tukiwa na majirani zetu Uganda. Kitu muhimu hapa ni kuanza kujipanga. Sisi makocha tutakuwa na majukumu yetu kuwajua kiundani wapinzani wetu wote.

“Ukiacha hilo tutakuwa na vikao vya maandalizi tukiwa na viongozi wa TFF na Serikali. Kitu kikubwa hapa tunatakiwa kufanya maandalizi mazuri ya timu yetu kabla ya kwenda kushindana kwenye hizo fainali. Haya yote yakifanyika kwa kiwango kikubwa hakuna kinachoshindikana kwetu,” alisema kocha huyo.

Naye nyota wa Taifa Stars, Simon Msuva aliongeza kuwa, “hakuna unyonge tumepangwa na timu kubwa, lakini sisi kama wachezaji tunajua kabisa kuwa soka ni mchezo ambao mafanikio yake yapo katika maandalizi na juhudi.”

Msuva alisisitiza kuwa Tanzania ina wachezaji wenye uwezo na viwango vya kimataifa vinavyoweza kuleta matokeo mazuri katika fainali hizo.  “Tunahitaji kujiandaa vizuri na kuhakikisha kila mmoja anatoa kile kilicho bora ndani yake,” alisema Msuva.

“Kwa upande wetu hatuwezi kujali majina ya wapinzani wetu. Tunahitaji kujielekeza kwenye maandalizi na kuwa na umoja kama timu.”

Msuva ambaye ameshiriki fainali mbili za Afcon mwaka 2019 na 2023, alisema uzoefu wake pamoja na wachezaji wengine utasaidia katika kuhamasisha vijana.

“Tuna uzoefu wa kutosha, katika kila mechi tutajitahidi kupata matokeo bora. Mchezo wa soka ni vita ya mawazo, tunahitaji kuwa na imani,” alisema.

Stars inakwenda kushiriki Afcon 2025 kwa mara ya nne baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 (Nigeria), 2019 (Misri) na 2023 (Ivory Coast).

Katika Afcon ya 2019, ndiyo pekee ambayo Stars iliondoka bila ya pointi lakini 1980 ilipata pointi moja na 2023 pointi mbili ingawa mara zote iliishia hatua ya makundi.