Mitindo ya nywele ya mastaa inabamba kitaa
Muktasari:
- Kuna wanaobadilisha unyoaji kila baada ya muda mfupi kiasi kwamba mashabiki wanaweza kuanza kuzungumza kuhusu nywele zao kuliko hata mabao waliyofunga.
KAMA unadhani wachezaji wana kazi ya kukimbiza mpira tu uwanjani, basi kuna kitu unakikosa. Kabla hata hawajavaa jezi na kuingia uwanjani, baadhi yao huwa tayari wameacha alama nyingine nje ya uwanja kutokana na nywele zao.
Kuna wanaobadilisha unyoaji kila baada ya muda mfupi kiasi kwamba mashabiki wanaweza kuanza kuzungumza kuhusu nywele zao kuliko hata mabao waliyofunga.
Katika miaka miwili iliyopita, mastaa mbalimbali wa soka duniani wamekuwa wakitokea uwanjani na mitindo ya nywele inayovutia macho.
Wengine wameamua kuweka mistari, wengine wameacha nywele nyingi juu, wengine wamezipunguza kabisa, huku wengine wakithubutu hata kubadilisha rangi.
Jambo la kuvutia zaidi ni mitindo hiyo haibaki kwa wachezaji pekee. Mashabiki na vijana wengi wamekuwa wakienda kwa vinyozi wakiwa na picha za mastaa wao na kusema, “Nataka kama hii.”
1. RAFU DREDI (MOHAWK YA VINICIUS JUNIOR)
Vinicius Junior ni miongoni mwa wachezaji ambao wamewahi kuonekana na mitindo mbalimbali inayosisimua. Mtindo wa mohawk unaacha nywele nyingi zaidi katikati ya kichwa halafu zinakuwa kama zimejisokota flani hivi kama hazijachanwa.
Mtindo huu unaweza kuukuta kwa wachezaji wengi wa Bongo, lakini si hivyo tu hata boda boda amenyoa mtindo huo, jambo ambalo linaonyesha nguvu iliyoko kwenye mitindo ya mastaa hao ambao wanatambulika dunia nzima.
2. AFRO (LOW TAPER YA JUDE BELLINGHAM)
Jude Bellingham amekuwa mmoja wa wachezaji wanaopenda mwonekano wa nywele fupi lakini wenye mpangilio. Low taper hupunguza nywele taratibu pembeni na nyuma, bila kuzifanya ziishe kabisa.
Huku mtaani wanauita Afro, unaweza kukutana na vijana wengi wamenyoa hivyo kwa sababu unapendwa sana na rika hilo kutokana na mvuto wake hasa kwa wale wenye nywele nyingi.
3. KAMA MBAPPE(BUZZ CUT)
Kuna wakati mchezaji anaamua kuachana na mambo mengi na kwenda moja kwa moja kwenye nywele fupi. Hapo ndipo buzz cut inapokuja na Mbappe akiwa miongoni mwa mastaa ambao hawataki mambo mengi kichwani.
Huu mtindo huu unapendwa sana na watu wa makamu ambao ukiwaangalia tu unajua huyu anajielewa, kama ni ofisini basi anaweza kuwa bosi au kiongozi wanaamini kwamba ni mtindo wa heshima.
4. KIDUKU (MULLET YA NEYMAR)
Neymar amekuwa maarufu pia kwa kubadilisha sura yake mara kwa mara, na mullet ni moja ya mitindo iliyowahi kumtambulisha.
Mambo ya wale masharobaro ndio haya mtindo huu mtaani wanauita kiduku unaacha nywele katikati ya kichwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho ukiwa umenyoa pembeni, na wapo ambao wanaziwekea dawa ili zilainike kabisa, wale wa mitindo hapa wanaelewa zaidi (vijana wa 2000).
5. WEI ZA PEMBENI (FADE)
Mistari iliyonyolewa pembeni mwa kichwa imekuwa sehemu kubwa ya mitindo ya wachezaji. Unaweza kuwa umenyoa tu kawaida, lakini ukaongeza mstari mmoja, miwili au michoro midogo pembeni.
Mara nyingi wanaonyoa hivi ni kama hawapendi mambo mengi ila wanatambulisha namna wanavyofagilia mitindo.
6. KISAHANI(CURLY FADE)
Huu ni mtindo ambao unawakuta mastaa wanaacha nywele nyingi kidogo hapa kati wakinyoa maeneo yote kwa usawa na kuacha zingine kwa juu kidogo.
7. VIRASTA NA RANGI(FROSTED TIPS)
Lammine Yammal na mastaa wengine wamekuwa wakibadilisha hata rangi ya ncha za nywele. Frosted tips ni mtindo ambao ncha za nywele hupakwa rangi nyepesi (BLEECH) huku sehemu nyingine ikiendelea kuwa na rangi yake ya kawaida.
Mastaa wengi wamewahi kunyoa mtindo huu ambao mara nyingi utaona wameweka nywele za kati rangi, ila huu wa kuweka kwenye ncha ni mtindo ambao umetamba miaka ya hivi karibuni.
8. UPARA
Wapo mastaa ambao hawataki kabisa kuwa na mambo mengi kichwani wala hapendelei kuonyesha haiba yake ya mitindo kupitia nywele, mfano Zinedine Zidane,Fabio Cannavaro na wengine.
Lakini huu sio mtindo unaotumiwa sana na mastaa wa soka wa sasahivi, hivyo unafifia sana na hata vijana mtaani hawapendelei kunyoa upara na wale watu wa makamo ambao nywele zimeanza kuwakimbia siku hizi baadhi yao wanavaa mawigi au kupaka mafuta maalum ya kuotesha nywele, hivyo ni ngumu kuona mastaa wameonyoa upara matokeo yake hata mtaani watu hawatumii mtindo huo.