Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MIANDAD: Mwamba wa kriketi Pakistan aliyetunzwa makumbusho ulaya

Muktasari:

  • Rekodi ya Miandad ilikuwa ya alama 163 alizopiga Pakistan ilipocheza na New Zealand Oktoba 9, 1976. Siku hiyo alikuwa na umri wa miaka 19 na siku 119. Rekodi hiyo ilivunjwa na Lhuan-dre Pretorius wa Afrika Kusini Juni 29, mwaka huu katika mchezo uliofanyika Bulawayo, Zimbabwe kwa kupiga alama 153. Alikuwa na miaka 19 na siku 93.

MIONGONI mwa mambo yaliyosubiriwa na mashabiki wa kriketi litokee kwa nusu karne hatimaye lilipatikana Juni 24, mwaka huu. Nalo ni kuvunjwa kwa rekodi iliyodumu miaka 49 ya mchezaji mahiri wa Pakistan, Javed Miandad kuwa mdogo zaidi katika mashindano ya kimataifa ya kriketi kupata alama zaidi ya 150 katika mchezo mmoja.

Rekodi ya Miandad ilikuwa ya alama 163 alizopiga Pakistan ilipocheza na New Zealand Oktoba 9, 1976. Siku hiyo alikuwa na umri wa miaka 19 na siku 119. Rekodi hiyo ilivunjwa na Lhuan-dre Pretorius wa Afrika Kusini Juni 29, mwaka huu katika mchezo uliofanyika Bulawayo, Zimbabwe kwa kupiga alama 153. Alikuwa na miaka 19 na siku 93.

Kuvunjwa kwa rekodi ya Miandad kulitawala kurasa na vipindi vya habari za michezo duniani zikiambatana na maelezo ya namna Miandad alivyotawala kriketi wakati wa ujana wake. Nyota huyo siku hizi hatoki viwanjani kuangalia vijana wakicheza na kila mwaka hutembelea nchi ambazo Wapakistani walikokwenda kufanya kazi na kuhimiza waanzishe timu za kriketi ili kiwe chombo kitachowakutanisha wakati wa furaha na huzuni. Mapema mwezi uliopita alikuwa Saudi Arabia alikopokewa kwa shangwe na raia wa Pakistan waliopo huko.

Kwa miaka mingi nilifuatia habari za Miandad kama vijana wa sasa wanavyopenda kandanda wanavyojua habari za kina Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Mo Salah, Saido Mane na wengineo. Miaka kama 40 iliyopita nikiwa Ghana kama mwandishi wa habari wa Daily News na Sunday News niliingia katika duka la rafiki yangu, Ramesh Patel, lililopo Accra kununua bidhaa.

Nilimkuta Patel aliyeoa binti wa kabila la Fanti nchini humo amefunga kitambaa cheusi mkononi na kabla sijampa pole nilitaka kujua nani amefariki dunia, lakini jibu lake lilinishangaza. Aliniambia alikuwa katika msiba kwa sababu timu ya India ilichapwa na Pakistan jana yake.

Patel hakuwalaumu wachezaji wa India, bali alimlaumu kijana aliyepeleka maafa India na ndio maana alifunga kitambaa cheusi kuashiria msiba uliomkuta. Kijana aliyemuumiza na mpaka leo anasifika kama mtu aliyeijengea heshima Pakistan katika kriketi na kuwa mmoja wa wachezaji mahiri wa miaka iliyopita ni Javed Miandad.

Mchezaji huyo ameacha kumbukumbu nzuri ambazo hazisahauliki kama mimi - ambavyo sitamshau yule mfanyabiashara aliyefunga kitambaa cheusi kutokana na Miandad kumnyima raha. Huyo ni mchezaji aliyeanza kutesa akiwa na umri mdogo kupiga mipira inayozunguka kwa kujiamini na kwa kipindi kirefu alikuwa nahodha aliyehimili dhoruba na kuivusha Pakistan katika michezo migumu.

Mwaka 1992, akiwa na miaka 35 alionekana amechoka na mashabiki wa kriketi wa Pakitan walitaka apumzishwe kwa mashindano ya Kombe la Dunia. Gazeti moja la Pakistan ambalo baadaye lilimuomba radhi liliandika: "Miandad amechoka na anafaa kwa michezo ya wazee tu na watu wenye ulemavu na si vijana kama ilivyo katika mashindano ya Kombe la Dunia."

Miandad alipotakiwa kuzungumzia kauli ile alisema uzee huanzia kaburini na kwa mshangao wa wengi alicheza katika mashindano hayo kama alivyokuwa kijana wa miaka 20. Huku akishangiliwa na vijana waliokuwa hawaamini alivyocheza, Miandad alifyatua mikwaju iliyomvusha hadi kwenye mpaka wa uwanja na kupata pointi nne na kuipaisha juu mipira mingine  na kujipatia pointi sita.

Mchezo wake katika mashindano hayo hasa walipokutana na India ndio ulioiwezesha Pakistan kubeba kombe ambalo Miandad alisema lilikuwa zawadi kwa wazee wa Pakistan. Hapo ndipo magazeti ya India, Pakistan, Bangladesh, New Zealand, Uingereza na Austratlia yalipochapisha makala ndefu zilizoeleza kuwa Javed Miendad amezaliwa upya. 

Lazima nikiri mimi pia nilishangazwa na namna Miandad ambaye alikuwa na umri mkubwa kuliko wachezaji wote katika mashindano yale alivyocheza. Hata hivyo, nilibaki kujisemea hata katika michezo mingine kama soka hutokea wachezaji wenye umri mkubwa wakafanya maajabu.

Licha ya kuwa mtu ambaye alikuwa na hasira, Javed Miandad aliyezaliwa Karachi Juni 12, 1957 alikuwa mpiga mikwaju na nahodha mahiri wa Pakistan. Alichomoza mara ya kwanza Oktoba 9, 1976 akiwa na miaka 19 pale alipokung'uta mikwaju 163 Pakistan ilipocheza na New Zealand ambayo ilikuwa na wachezaji mashuhuri wenye uzoefu wa kuwatega wapinzani.

Alifanikiwa kuwa mchezaji wa pili wa Pakistan kukung'uta mikwaju zaidi ya 100 katika michezo ya kimataifa baada ya Khalid Ibadulla aliyefikisha 166 Pakistan ilipocheza na Australia 1964. Aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kufikisha mara mbili mikimbio zaidi ya 100 katika shindano moja.

Wakati ule hii ilikuwa na rekodi iliyofikiwa na mchezaji mmoja tu - George Headley wa West Indies aliyekung'uta mikimbio 223 walipocheza na Uingereza Aprili, 1930. Miandad aliweka rekodi nyingi katika michezo ya siku moja na ni mchezaji wa kwanza wa Pakistan kupata alama 100 aliposhuka uwanjani mara ya kwanza kucheza na India. Hii ilikuwa Oktoba, 1978 nchi hizo zilipokutana katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Miandand alichezea timu za Pakistan na Uingereza. Miongoni mwazo ni Habib Bank Limited, Sind na Karachi za Pakistan pamoja na Sussex na Glamorgan za Uingereza. Kwa wastani ufungaji wake haukuwa wa chini ya alama 50, lakini pia mwepesi kudaka mipira ya juu na chini. Baadhi ya nyakati alikuwa methali ya 'nyani anaporukia tunda liliowiva' na mipira aliyorusha iliwasumbua wapinzani wake.

Mpaka sasa Miandad ni mchezaji pekee duniani kushiriki mashindano sita ya Kombe la Dunia la Kriketi kuanzia 1975 hadi 1996. Mchezo wake wa mwisho wa kimataifa ulikuwa Desemba 16, 1997 Pakistan ilipocheza na Zimbabwe, na alipostaafu wengi walihisi ilikuwa mapema kwa vile alikuwa bado anacheza vizuri.

Baada ya kustaafu alitangaza na kuchambua michezo ya kimataifa alipokuwa India kwa muda na alisema India ni taifa lake la pili kwa vile baba yake aliishi huko hadi alipohama na mamilioni ya watu waliokwenda kuanzisha taifa la Pakistan  1947 India ilipogawanyika pande mbili - India na Pakistan.

Alipoulizwa kuhusu Bangladesh ambayo nayo ilitokana na Pakistan kugawanyika alisema: "Pakistan ndio baba na mama, India ni mjomba na shangazi na Bangladesh ni mjukuu." Miandad ameandika vitabu vya kriketi na kueleza kwa kirefu  alivyojitayarisha kwa michezo ya kimatifa.

Mara nyingi amekuwa katika migogoro kwa kauli zake za mafumbo yenye matusi yaliyojificha. Siku moja aliwaudhi wachezaji mahiri aliposema tatizo la baadhi yao ni kudhani mchezo huo ni sawa na kukuna nazi au kupaka hina. Mkasa mwingine ni siku ilipofika zamu yake kuingia uwanjani kucheza baada ya mwenzake mmoja kushindwa kuvilinda vijiti visiangushwe. Alipotafutwa alikutwa anasali na ilibidi asubiriwe kwa dakika tatu. Mwamuzi alipomlaumu kwa kufanya hivyo alimwambia: "Wapi imeandikwa katika sheria za kriketi wachezaji kutakiwa kuabudu mchezo na kumuweka Mungu pembeni."

Miandad pia anakumbukwa kwa kijembe alichompiga aliyekuwa Rais wa Pakistan, Zia Ul-Haq alipokasirika Pakistan  ilipofungwa na India. Alimwambia anaelewa machungu aliyokuwa nayo, lakini siyo sahihi na kumtaka Rais ahame Ikulu na kujiunga na timu ya taifa ili kulinda heshima ya Pakistan inapocheza na India.

Rais Zia alikasirika, lakini alishauriwa asimtie gerezani kwa sababu angefanya hivyo Pakistan ingekumbwa na balaa kutokana na mapenzi makubwa waliyokuwa nayo wananchi kwa Miandad. Jina la Miandad limeingizwa katika Ukumbi wa wanamichezo maarufu wa kriketi nchini Uingereza. Mwishoni mwa 2008 aliombwa kuifundisha timu ya Pakistan, lakini alikataa kwa maelezo ya kutaka kupumzika.