Miaka mitano ya kibabe ya Sportpesa Tanzania

Miaka mitano ya kibabe ya Sportpesa Tanzania

KAMA utani vile. Kampuni ya Michezo na Burudani ya Sportpesa, leo inaadhimisha miaka mitano tangu kuanza shughuli zake za michezo ya kubashiri nchini Tanzania.

SportPesa iliingia na kuanza shughuli zake nchini Mei mwaka 2017 na kutoka hapo imefanya mambo makubwa ya kihistoria yanayoifanya itembee kifua mbele.

Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SportPesa na Mtanzania pekee mwanahisa, Tarimba Abbas akizungumza kwenye ofisi za kampuni hiyo zilizopo Oysterbay, anasema wanajivunia kutimiza miaka mitano ya kufanya shughuli zao nchini kwa mafanikio makubwa.

“Kampuni hii ya Sportpesa ilianza rasmi shughuli zake Mei, 2017 ikiwa na ofisi yake Oysterbay, Dar es Salaam,” anasema na kuongeza;

“Tangu kuanza kwa kushughuli zake za michezo ya ubashiri na kubahatisha kampuni ya Sportpesa ndani ya miaka 5 imefanikiwa kuwa namba 1 kati ya kampuni zaidi ya 20 zinazojihusisha na shughuli za ubashiri nchini Tanzania.

“Kampuni yetu ilianza na uwekezaji mkubwa wa kimtaji ikiwekeza zaidi ya Bilioni 35 kuanzia wakati ule mpaka wakati huu ambapo tunaadhimisha miaka mitano ndani ya ardhi ya Tanzania.”


UZOEFU

Akizungumzia uzoefu wake katika tasnia ya michezo ya bahati nasibu, Tarimba anasema amehudumu serikalini kwa zaidi ya miongo miwili na nusu ambapo alifanikiwa kupata uzoefu wa kutosha kumudu kuongoza kwa mafanikio taasisi ya Bahati Nasibu Tanzania, Bodi ya michezo ya Kubahatisha na sasa Sportpesa Tanzania.

“Mwaka 2002 niliasisi utafiti uliopelekea kuvunjwa kwa Shirika la Bahati Nasibu Ya Taifa na kuanzishwa kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha. Mimi niliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa taasisi hiyo ambayo ipo hadi sasa ikiratibu na kusimamia sheria, kanuni na matakwa ya kiuwekezaji katika sekta ya michezo ya kubahatisha,” anasema Tarimba na kuongeza;

“Katika miaka yangu yote ya kufanya kazi serikalini nimebahatika kuhudhuria makongamano na mafunzo mbali mbali ambao umenipa msingi na kunijenga kuwa na uzoefu mkubwa ambao umezinufaisha hata nchi Jirani kama Kenya, Uganda, Msumbiji, Ghana, Ethiopia na Malawi.”

“Hii ilipelekea mimi baada ya muda mrefu wa kuitumikia serikali, ilipofika muda wa kustaafu nilifikiria namna ya kujiunga na kampuni binafsi ambayo ina mipango na weledi kama niliokuwa nayo mimi. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mimi kujiunga na Sportpesa na kuwa mmoja wa washirika wa kibiashara kama mwanahisa pekee ndani ya kampuni.

“Moja ya jambo ambalo tunajivunia kwa uhakika kabisa ni namna tulivyoweza kukua kwa kiwango cha kuongoza soko kwa asilimia 30. Toka tumeanza tumekuwa tukikuwa katika maeneo mengi moja wapo ni aina za huduma na viwango vya zawadi tunavyotoa, ikienda sambamba na ujumla wa kodi tunazolipa.

“Kwa ufupi kwa miaka hii mitano tu, jumla ya kiwango cha fedha za zawadi kwa wachezaji wetu tumetoa Bilioni 434.4, hii ikienda sambamba na kiwango kikubwa kabisa cha zawadi ya washindi wawili wa Jackpot ambao waligawana Milioni 400 na ushehe ambapo mwajiriwa wa Magereza na Muajiriwa wa Jeshi walishinda kila mmoja.

Tarimba anaongeza kwa kusema; “Pia kuna kodi iliyotokana na zawadi za washindi ambapo jumla yake ni Sh 63.3 Bilioni zimelipwa serikalini, kiasi cha kodi Sh 34 Bilioni kimelipwa kwenye matumizi mengine ya kawaida na shughuli za operesheni za kibiashara za kampuni.”


UDHAMINI

“Kwa upande wa kurudisha kwa jamii tumewekeza kiasi kikubwa sana kwenye udhamini ambapo tulianza na Simba na Yanga baadae tukaenda kwa Singida United na Namungo. Pia katika muktadha huo tuliweza kuwaleta Everton na Sevilla kwa nyakati mbili tofauti, pamoja na wachezaji kadhaa waliowika wa ligi kuu ya Uingereza kama Sol Campbel na viongozi wa timu kama Southampton, Hull City, Arsenal, Everton na watendaji wa ligi ya La Liga ambao kwa pamoja walifanya kliniki kwa wachezaji na viongozi wa kitanzania.”

Anafafanua kuwa; wakati wa maandalizi ya kuwaleta Everton iligundulika eneo la kuchezea na la kubadilishia nguo katika uwanja wa Mkapa hayakuwa katika viwango na ubora unaostahili hivyo ililazimu kuleta wataalamu wa nyasi wa kimataifa toka nje pamoja na waliofanyia maboresho vyumba vya kubadilishia nguo.

“Ilitulazimu kudhamini maboresho na matengenezo ya uwanja wa Mkapa ambao zamani ulikuwa unaitwa uwanja mkuu wa taifa. Tulifanya ukarabati wa eneo la kuchezea katika awamu moja wakati wa kuileta Everton ambapo tulifanya ukarabati wa muda mfupi na baada ya hapo tulidhamini usimamizi na maboresho ya nyasi za uwanja kwa miaka miwili tukileta wataalamu waliobobea katika shughuli hizo toka Ireland na Italia.”

Tarimba anaendelea kusema katika hatua kubwa za udhamini walizozifanya ni Pamoja na kuanzisha mashindano ya Kombe la Sportpesa ama (Sportpesa Cup) lililofanyika mara mbili Tanzania na mara moja nchini Kenya.

“Kwa sasa mashindano haya yalisimama kwa muda kutokana na athari za ugonjwa wa uviko 19, lakini mipango bado ipo jikoni tukifanya tathmini ya namna ya kuyarudisha katika siku za usoni pale ambapo mazingira yatakuwa rafiki.”


CHANGAMOTO

Anasema angependelea kuwe na ubunifu zaidi wa mfumo wa kodi ambao utachochea wachezaji wangi zaidi ili faida iongezeke si tu kwa wao kama kampuni bali hata kwa Serikali

“Hapa natolea mfano wa kodi ambayo ilikuwa inakatwa toka kwa wachezaji na kwa kampuni ambayo ilikuwa asilimia 20 kutoka Julai hadi Desemba 2020. Baada ya kutolewa asilimia 5 ya kodi hiyo kumepatikana faida ya mapato Sh 14 Bilioni kwa kipindi cha miezi sita yaani Julai hadi Desemba 2021 ambayo ni asilimia 37 zaidi ya 2020,” anasema Tarimba na kuongeza; “Kwa mwaka wa fedha Julai 2021 hadi Juni 2022 serikali ilipanga kukusanya Sh 150 Bilioni na hadi sasa umebaki mwezi mmoja wameshakusanya asilimia 90 ya mapato waliyotarajia.”

Anaitaja changamoto nyingine ni kwamba, anaona serikali inabidi iweke mizania sawa wakati wa kutunga sheria zinazohusiana na michezo ya kubahatisha ili wadau wakuu nao wapewe nafasi inayostahiki katika kusikilizwa kabla sheria hazijapitishwa ama kutungwa.

“Hapa naamini pana changamoto ya uelewa wa mazingira halisi ya biashara hii ambapo ni ngumu kwa mtu ambaye hana taaluma ama uzoefu kama wa kwangu wa kuingia kwa undani kutunga sheria na kanuni zitakazowezesha mazingira mazuri ya kukuza aina hii ya biashara.”

Tarimba amegusia pia uwepo wa utitiri wa vyombo ama taasisi za udhibiti zimekuwa nyingi zote zikilenga kupata mapato kwenye eneo moja. Hii inapelekea kampuni kutumia fedha nyingi katika shughuli ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na uzalishaji wa mapato.


MIPANGO YAO

Tarimba anamalizia kwa kuanika mipango ya Sportpesa kwa miaka mitano ijayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mafanikio waliyoyapata ndani ya miaka hii mitano yanadumisha na kuyaboresha.

Pili lengo kuu ni la kuendelea kuongoza sekta hii ya michezo ya kubahatisha kwa kusalia kwenye nafasi ya kwanza kama ilivyosasa.

Jambo la tatu ambalo analiona Sportpesa itafanikiwa nalo ni pamoja na azma ya kuongeza mapato hadi kufikia zaidi ya asilimia 40 au 50 ya ukubwa wa soko. Nne kuongeza ajira kwani kadri wigo wa wachezaji na mtaji utakavyokuwa ndivyo huduma nyinginezo zitakavyohitaji watendaji wa kuzisimamia na kuzitekeleza.

Tano kuongeza thamani ya zawadi ambapo alitolea mfano wa Jackpot yetu ya sasa ambayo ipo zaidi ya Sh 1 Bilioni, itakapopata mshindi basi wataongeza Jackpot nyingine kubwa ambayo itavutia zaidi. Ikumbukwe Jackpot inayochezwa sasa hivi inaanzia Sh 200 Milioni 200 na pia inachezwa kwa mechi 13 tu.