Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 63 ya kibabe michezoni

Uhuru Pict

Muktasari:

  • Kwa umri wa binadamu, miaka 63 ni mingi kiasi cha mtu kuitwa mzee, ikiwa na maana kama nchi imepiga hatua ndefu tangu Waingereza waliokuwa wakoloni wa mwisho kuitawala Tanganyika (sasa Tanzania Bara) walipoamua kuondoka nchini.

LEO ni Desemba 9. Hii ni siku muhimu kwa Watanzania hasa wa Tanzania Bara (zamani Tanganyika) ambao wanasherehekea Miaka 63 ya Uhuru tangu ilipojikomboa kutoa kwa Koloni la Kiingereza tarehe kama hiyo, lakini ni mwaka 1961 kisha kuwa Jamhuri mwaka mmoja tu uliofuata yaa 1962.

Kwa umri wa binadamu, miaka 63 ni mingi kiasi cha mtu kuitwa mzee, ikiwa na maana kama nchi imepiga hatua ndefu tangu Waingereza waliokuwa wakoloni wa mwisho kuitawala Tanganyika (sasa Tanzania Bara) walipoamua kuondoka nchini.

Yapo mengi ya kujivunia katika umri huo wa Miaka 63 hususani kwenye michezo hata kama kuna ndoto hazijafikiwa kama matarajio ya wengi, lakini kuna historia kubwa imeandikwa katika umri huo.

Kuanzia katika soka hadi michezo mingine kuna mambo ya kujivunia, ikiwamo kung’ara kwa baadhi ya nyota mbalimbali, huku timu za taifa zikiweka rekodi kadhaa kimataifa kuonyesha kuwa, Uhuru ulifungulia mambo mengi.

Kumbuka tu, Tanganyika iliungana na Zanzibar mnamo Aprili 26, 1964 na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya sasa inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.


TUANZIE HAPA

Haikuwa jambo jepesi kwa taifa changa kama Tanganyika wakati ule kushiriki kwenye michezo mikubwa ya Olimpiki.

Ilikuwa ni miaka miwili na miezi kadhaa tangu Tanganyika sasa Tanzania Bara kupata Uhuru, Desemba 9, 1961 na kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa kama taifa huru.

“Tulikuwa wageni katika kila kitu, kuna muda tulilazimika kutumia ishara ili kupata huduma,” aliwahi kukaririwa Daniel Thomas mmoja wa Watanganyika wa kwanza kushiriki Olimpiki mwaka 1964.

Michezo ya wakati huo ilifanyika Tokyo, Japan na Tanganyika iliwakilishwa na wanariadha wanne, wakiwamo Hassan Dyamwale na Paschal Mfyomi ambao wametangulia mbele za haki na Omary Abdallah inayesemekana yupo Falme za Kiarabu (UAE).

Thomas alisimulia safari ya Tanganyika katika Olimpiki hiyo ya kwanza baada tu ya Uhuru, enzi hizo pia alikuwa alikuwa ni mwalimu wa moja ya Shule za Msingi huko Musoma Vijijini anasema, ushiriki wa mashindano hayo ulibadilisha historia ya maisha yake.


REKODI MIAKA MINNE

Baada ya Uhuru, ilikamilika miaka minne kabla ya Tanzania kuweka rekodi ya kwanza ya medali ya kimataifa ambayo ililetwa nchini na mwanariadha Theresia Dismas.

Mwanariadha huyo wa mitupo, alishinda medali ya shaba ya kurusha mkuki katika Michezo ya Afrika (All Africa Games) ya 1965 iliyofanyika Congo Brazzaville.

Inaelezwa Theresia aliolewa baadaye na mwanariadha mwenzake raia wa Kenya na kuishi wote nchini Marekani, ingawa baadaye mumewe alifariki na yeye kurejea Kenya ambako anaishi na familia yake hadi sasa.


AKHWARI GUMZO

John Stephen Akhwari alikuwa katika timu ya Tanzania iliyoshiriki michezo ya pili ya Olimpiki ya 1968 huko Mexico, ikiwa ni Olimpiki yake ya kwanza, lakini mkongwe huyo aliandika historia ya dunia kwa kumaliza wa mwisho mbio ya marathoni (kilomita 42).

UH05

Katika mbio hizo, Akhwari aliumia na kufungwa bandeji mguuni, huku akivuja damu, mwanariadha huyo aliendelea na mbio pole pole huku akichechemea, wakati asilimia kubwa ya mashabiki wakiwa wameondoka uwanjani, ndipo yeye aliingia akiwa anachechemea.

“Nilipohojiwa niliwaeleza, taifa langu halikunituma kuanza bali kumaliza,” anasema Akhwari ambaye alitumia saa 3.25.27 akiachwa kwa zaidi ya saa moja na bingwa wa mbio hizo raia wa Ethiopia, Mamo Wolde aliyetumia saa 2.20.26.


NGUMI NAKO

Baada ya Uhuru, timu ya taifa ya ngumi ilisubiri kwa miaka tisa kuvuna medali ya kwanza ya kimataifa aliyoshinda, Titus Simba (sasa ni marehemu).

Simba alishinda medali hiyo kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya 1970.


REKODI YA DUNIA

Tanzania iliendelea kujidhihirisha michezo kwa kuvunja rekodi ya dunia katika mchezo wa riadha.

Ni rekodi ambayo Filbert Bayi anasema alimuahidi Mwalimu Nyerere kuivunja, alipomualika katika chakula cha jioni mjini Arusha na kweli alifanikiwa katika mbio za mita 1500 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola 1974 iliyofanyika New Zealand akitwaa medali ya dhahabu na kufanya vema kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwamo Michezo ya Olimpiki ya Moscow, Russia mwaka 1980 alipotwaa medali ya fedha ya Olimpiki kwenye mbio za mita 3000 kuruka viunzi na kukanyaga maji. Pia alishabeba medali za dhahabu katika michezo ya Afrika 1973 na 1978.

Kwenye michezo ya Olimpiki 1978, Suleiman Nyambui pia alitwaa medali ya fedha katika mbio za mita 5000, pia akishinda medali ya shaba katika Michezo ya Afrika 1978 iliyofanyikia Algeria.


REKODI ZAIDI

Moja ya mbio kubwa duniani ni zile za New York Marathon ambazo katika miaka 63 ya Uhuru, Tanzania ina historia ya kuwa bingwa mwaka 1989 aliyefanya kazi hiyo akiwa ni Juma Ikangaa akitumia saa 2.08.01 kabla ya kutwaa medali fedha mara mbili katika mbio nyingine kubwa za Boston Marathon 1988 na 1990.

Mbio nyingine ambazo Ikangaa alifanya vizuri ni zile za Fukuoka na Melbourne Marathon, Mashindano ya Afrika ya 1984, michezo ya Jumuiya ya Madola ya 1982.


WANAWAKE WATIKISA

Mwinga Mwanjala katika miaka 60 ya uhuru ana rekodi yake ya kuwa mwanamke wa kwanza kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki.

Mwanariadha bingwa wa taifa wa mbio za mita 800, Mwinga alishiriki Olimpiki ya 1980 na ana rekodi ya kufanya vizuri nchini kwenye mbio za mita 800 na 1500.

Pia kuna Zakia Mrisho, kati ya nyota wa riadha nchini waliotamba kimataifa. Zakia ambaye sasa ni kocha alitamba katika mbio ndefu za uwanjani za mita 3000 na 5000.

Mwaka 2005 alimaliza wa tatu kwenye mashindano ya dunia Monte Carlos, Monaco nchini Ufaransa ingawa pia amewahi kuwa kinara kwenye mashindano ya Diamond League ya 2004, 2005 na 2009. 

Kuna Failuna Abdi aliyeng’ara katika medani ya riadha ya kimataifa, mwanariadha huyu alikuwa mchezaji pekee aliyeiwakilisha nchi kwenye Olimpiki ya 2021 nchini Japan.


WENGINE HAWA HAPA

Alphonce Simbu

Katika miaka 60 ya Uhuru anaingia kwenye rekodi ya kutwaa medali ya shaba ya dunia kwenye mbio za marathoni, mwanariadha huyo ana rekodi ya kuingia kwenye tano bora ya Olimpiki ya Rio 2016 na mbio za London Marathon na dhahabu ya mbio ya Mumbai Marathon huku muda wake mkali ukiwa ni saa 2:09:10.


Samson Ramadhan

Ana rekodi yake tamu ya medali ya dhahabu ambayo ni ya mwisho kwa Tanzania kwenye michezo ya madola, Samson ambaye sasa ni mjeshi wa JWTZ alishinda medali hiyo kwenye michezo ya 2006 nchini Australia, huku Fabiano Joseph Naasi akishinda shaba kwenye mbio za mita 10,000.


Samwel Mwera

Amewahi kuitwa kwenye timu ya Afrika iliyoshiriki mashindano ya Afro Asian na hakurejea kapa, mwanariadha huyo bingwa wa taifa wa mbio za mita 800 alishinda medali ya shaba.

Mwera alipata nafasi hiyo baada ya kuwa bingwa wa mbio za mita 800 kwenye michezo ya Afrika ya 2003 uko Abuja, Nigeria akitumia dakika 1.46.13.


Fabiano Joseph Naasi

Ni miongoni mwa wanariadha wenye mijengo ya ghorofa ya maana pale Arusha, mwanariadha huyu kasi ya miguu yake iliwahi kubadili upepo wa maisha yake baada kushinda dola 100,000 kwenye moja ya mbio kubwa za pesa duniani mwanzoni mwa mwaka 2000.


Rashid Matumla

Ni miongoni mwa mabingwa wa ngumi za kulipwa nchini wa kihistoria, katika miaka 60 ya Uhuru, Matumla au Snake Man kama anavyopenda kujiita ameweka rekodi ya kuwa bingwa wa dunia wa WBU.

Matumla ambaye pia amewahi kuwa bingwa wa African Boxing Union (ABU) mwaka 1997 kwa sasa amestaafu anaishi nyumbani kwake Mbagala Kuu.


Francis Cheka

Alikuwa ni nembo nyingine ya Tanzania kwenye ngumi za kulipwa, baada ya zama za Matumla kupita, Francis Cheka ndiye alifuata na katika miaka 60 ya uhuru ana rekodi yake ya kuwa bingwa wa dunia wa WBF.

Cheka alivuliwa ubingwa huo baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, japo baada ya wiki kadhaa alipata msamaha na kupewa kifungo cha nje, hivi sasa Cheka amestaafu yuko nchini Msumbiji alikozaliwa mama’ake, Maria Rafael.


Hasheem Thabeet

Alitikisa vyombo vya habari akiwa ni Mtanzania ambaye alipata mafanikio kwenye mpira wa kikapu.

Nyota huyu wa kimataifa wa Tanzania wa kikapu katika miaka 60 ya uhuru ametengeneza rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi maarufu ya mpira wa kikapu duniani ya Marekani (NBA) mwaka 2009 na kati ya timu alizocheza ni ile ya Memphis Grizzlies, Houston Rockets, Oklahoma City Thunder na Portland Trail Blazers.


UH03

Hassan Mwakinyo

Ni bondia namba moja nchini, Mwakinyo aliandika rekodi ya kihistoria mwaka 2018 alipomchapa kwa TKO, Sam Eggington aliyekuwa nyumbani nchini Uingereza, pambano ambalo lilistua dunia kutokana na rekodi ya mabondia hao, Eggington akiwa namba nane wa dunia na Mwakinyo wa 179.

Pambano hilo lilimpandisha hadi nafasi ya 14 duniani, kabla ya kumchapa Eduardo Gonzalez wa Argentina kwenye pambano lililopigwa nchini Kenya na rais John Magufuli (sasa ni marehemu) kumualika Ikulu Dar es Salaam na kumpa zawadi ya kiwanja mjini Dodoma.


Michael Yombayomba

Hadi mauti yanamkuta mwaka 2015, rekodi ya Michael Yombayomba ilikuwa haijavunjwa kwenye timu ya taifa ya ngumi za ridhaa.

Yombayomba ni bondia pekee nchini kutwaa medali ya dhahabu ya kimataifa, ambayo alishinda mwaka 1998 kwenye Michezo ya Madola huko Kuala Lumpur, Malaysia.

Hata hivyo, bondia huyo hakupata nafasi ya kutetea medali yake kwenye michezo iliyofuatia ya 2002 ya nchini Uingereza.

Wengine walioandika rekodi katika miaka 63 ya uhuru ni bondia Habibu Kinyogoli na Haji Matumla na wanariadha Gidamis Shahanga na Zacharia Barie waliotwaa medali kwenye michezo ya Afrika na Madola, mbali na timu za kikapu, kuogelea na tenisi pamoja na timu ya soka la walemavu iliyocheza fainali za dunia.


SOKA NAKO MOTO

Ukiachana mafanikio kwenye michezo hiyo mingine, pia kwenye soka nako kuna alama kadhaa zimeachwa tangu nchi ipate Uhuru, kwani kama nchi ilijishughulisha na mchezo huo hata kabla ya Uhuru.

Klabu na wanamichezo mbalimbali wamekuwa na mchango mkubwa wa upatikanaji wa uhuru huo zikiwamo klabu za Simba na Yanga zilizoanzishwa zaidi ya miaka 88 iliyopita.

Historia inaonyesha Tanganyika iliasisi chama chake mwaka 1945 na kushiriki michuano mbalimbali hususani iliyohusisha nchini za Afrika Mashariki, inayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Michezo katika ukanda huo (CECAFA) lililoasisiwa mwaka 1926.

Tanganyika ilishiriki michuano ya Kombe la Gossage iliyochezwa kati ya mwaka 1926-1966, kisha ikabadilishwa na kuwa Kombe la Chalenji ikichezwa kati ya mwaka 1967-1971 na baadaye kuasisiwa tena kwa Kombe la Cecafa 1973 hadi sasa.

Rekodi zinaonyesha taji la kwanza la michuano hiyo, nchi ikiwa bado Tanganyika lilikuwa mwaka 1949, miaka minne tangu kuasisiwa kwa Chama cha Soka (sasa Shirikisho, TFF) kisha ikabeba tena 1950 na 1951, 1964, 1965, 1974, 1994 na 2010.

Upande wa Visiwani, Zanzibar ilitwaa mara moja tu taji hilo mwaka 1995.


UH01

MICHUANO YA AFRIKA

Mbali na kung’ara katika michuano ya CECAFA, Tanzania pia imefuzu fainali saba tofauti za Afrika, zikiwamo za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 1980 michuano ilipofanyika Nigeria, mwaka 2019 kule Misri, 2023 zilizofanyikia Ivory Coast na msimu ujao itacheza pia Morocco baada ya kukata tiketi huku 2027 itakuwa wenyeji sambamba na Kenya na Uganda.

Kadhalika imefuzu fainali za Afrika kwa Wachezaji wanaocheza kwenye ardhi za nchi zao (CHAN) 2009 iliyokuwa ya kwanza tangu ilipoasisiwa michuano hiyo na kisha kufanya hivyo tena 2020, japo michuano ilichezwa mwaka 2021 pale Cameroon na msimu ujao itashiriki kama wenyeji sambamba na Kenya na Uganda.


NYOTA WAWILI

Tanzania iliweka rekodi pia ya kutoa nyota wawili katika kikosi cha Afrika kupitia michuano ya All Africa Games ya mwaka 1973, iliyofanyika Nigeria kwa kipa Omary Mahadh Bin Jabir na Maulid Dilunga (wote sasa marehemu) kung’ara na Taifa Stars.

Wachezaji hao waliungana na wachezaji wenzao wa mataifa mbalimbali waliounda timu ya Afrika kufanya ziara katika nchi tofauti ikiwamo Mexico na kusababisha Maulid, kubatizwa jina la Mexico.

Pia Tanzania imefuzu fainali nne tofauti za vijana, ikiwamo ya Afcon U17 mwaka 2017 zilizofanyika Gabon, kisha ikawa wenyeji mwaka 2019 na 2021 ila fainali zilifutwa, huku kwa Afcon U20 tumeshiriki mara moja 2021 na tayari imefuzu kwa fainali za 2025. Kwa upande wa Cecafa imetwaa taji mara mbili 1971 na 2019.


UH04

NGAZI YA KLABU

Katika ngazi ya klabu Tanzania ina rekodi kadhaa za kujivunia, ikiwamo kubeba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) mara 13, Simba ikibeba mara sita ikiwa ndiye kinara katika michuano hiyo na Yanga ilitwaa mara tano na Azam yenyewe ikilibeba taji hilo mara mbili.

Licha ya kutowahi kubeba ubingwa wa Afrika licha ya kuanza kushiriki tangu mwaka 1969, lakini timu za Tanzania, Simba, Yanga na Namungo zimeweza kujitutumua na kufika hatua mbalimbali zinazozipa heshima kati ya timu za Tanzania.

Simba imefika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) mwaka 1974, kisha kufika fainali ya michuano ya Kombe la CAF 1993, taji lililotolewa na mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Mashood Abiola mwaka 1992 kabla ya michuano hiyo kuzikwa 2004 kwa kuunganishwa na ile ya Kombe la Washindi Afrika na kuwa Kombe la Shirikisho Afrika linalochezwa sasa.

Simba pia imefuzu makundi ya CAF mara sita 2003, 2018-2019, 2020-2021, 2022-2024, 2023-2024 na msimu huu, huku msimu wa 2019, 2020-2021, 2022-2023 na 20223-2024 ikifika hatua ya Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wakati msimu wa 2021-22 ilicheza makundi ya Kombe la Shirikisho na kufika robo fainali.

Yanga klabu asisi ya kucheza michuano ya Afrika nayo imewahi kufika mara kadhaa robo fainali ya michuano ya Kombe la Washindi, kucheza makundi mara sita, 1998, 2023-2024 ilipofika robo fainali katika Ligi ya Mabingwa ambapo kwa msimu huu imetinga pia makundi, huku 2016, 2018 na 2022-2023 ilifika makundi ya Kombe la Shirikisho. Na msimu wa 2022-2023, Yanga iliandika rekodi ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini lililoipa ubingwa USM Alger ya Algeria baada ya matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2.

Yanga ilifungwa nyumbani mabao 2-1 kisha kwenda kushinda 1-0 ugenini kwa bao la penalti la Djuma Shaaban ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha Namungo.

Timu nyingine za Tanzania zilizofika mbali katika michuano ya CAF ni Namungo iliyocheza makundi ya Kombe la Shirikisho, huku Malindi ya Zanzibar nayo ikiwahi kufika hatua za robo na nusu fainali miaka ya 1990 ya Kombe la Washindi.


UH02

SOKA LA WANAWAKE

Ndani ya miaka 60 ya Uhuru imeshuhudiwa pia soka la Wanawake likipata heshima kubwa ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na All Africa Games kwa miaka tofauti, huku ikitwaa mataji katika michuano ya CECAFA na ile ya COSAFA inayohusisha nchi za Kusini mwa Afrika inapoalikwa. Pia timu ya Vijana ya wanawake U17 ilishiriki fainali za Kombe la Dunia.

Kupitia timu za taifa za U17, U20, U23 na Twiga Stars, Tanzania inatembea kifua mbele katika soka la wanawake, huku ikiwa na Ligi Bora kabisa ya soka hilo iliyoasisiwa mwaka 2016 na aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi. Mwakani pia Twiga Stars itashiriki fainali za Afrika baada ya kukata tiketi hiyo.

Twiga imeshiriki fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) mara tatu na kuishia makundi 2011, 2015 na 2023. Pia imebeba taji la Cosafa 2021 na Cecafa 2016 na 2018 na kucheza makundi ya Wanawake Afcon 2010.

Kwa ngazi za klabu, Simba Queens imeshatwaa ubingwa wa Cecafa mara mbili na kucheza fainali za Afrika kama ilivyokuwa kwa JKT Queens iliyobeba taji la Cecafa mara moja na kucheza fainali za Afrika mara moja pia.