Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Messi alivyokaribia kutunyima chozi la Dembele

DEMBELE Pict

Muktasari:

  • Machozi hayo yalitokana na furaha ya kumwona mwanae Ousmane Dembele akiwa ameshika tuzo ya Ballon d’Or.

PARIS, UFARANSA: KATIKA ukumbi wa Theatre du Chatelet mwanamama mrembo Fatimata Dembele usiku wa juzi Jumatatu, Septemba 22, alikuwa akiyaogesha mashavu yake kwa machozi ya furaha.

Machozi hayo yalitokana na furaha ya kumwona mwanae Ousmane Dembele akiwa ameshika tuzo ya Ballon d’Or.

Ilikuwa ni kama anaota lakini ndiyo ukweli. Dembele ameshinda tuzo hiyo mbele ya mastaa wengine alioingia nao tatu bora Lamine Yamal na Vitinha.

Sio mama yake tu, hata Dembele mwenyewe pamoja na familia kwa jumla walikuwa wanatokwa na machozi kutokana na tukio hilo.

Machozi haya ya furaha kwa familia pengine tusingeyaona juzi kwenye usiku wa tuzo kutokana na kile ambacho Messi alikuwa akikifanya kwa Dembele.

Mwaka 2017, Hispania ilitikisika, Barcelona ilivunja rekodi ya usajili kwa kumsajili Dembele kutoka Borussia Dortmund kwa ada ya Euro 140 milioni.

DEMBE 01

Wakati huo Dembele alikuwa wa moto, ndiyo kwanza alikuwa akitimiza miaka 20, akiwa na Dortmund msimu wa 2016/17 alifunga mabao 10 akatoa asisti 20 katika mechi 49 za michuano yote.

Vigogo wote Ulaya walikuwa wakitamani kumpata. Lakini asingeweza kukataa kutua Barca kutokana na pesa ambazo ziliwekwa, pia ubora wa timu hiyo kwa muda huo.

Baada ya kutua katika viunga hivyo, mambo yalikuwa tofauti. Hali ya majeraha ilianza kuwa maisha yake, benchi likawa sehemu ya maisha yake.

Ilikuwa ajabu sana kwa mchezaji ambaye alitajwa kama kinda bora wa dunia katika msimu mmoja nyuma, iweje msimu uliofuatia awe anasugua benchi? Na majeraha kumwandama mara kwa mara.

Msimu huo Dembele alicheza mechi 24 ambazo nyingi aliingia akitokea benchi, mambo yaliendelea kuwa hivyo kwa panda shuka nyingi hadi Barcelona ilipoamua kumuuza kwa bei ya hasara ya Euro 50 milioni mwaka 2023 kwenda PSG.

Mambo ya nyuma ya pazia yanaeleza undani wa kufeli kwa Dembele Barcelona chanzo chake kikubwa hasa ilikuwa ni mtindo wa maisha ya Messi.

Kevin Prince Boateng, mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana ambaye aliwahi kucheza kwa mkopo wa miezi sita Barcelona, katika mahojiano yake na Rio Ferdinand aliweka wazi mtindo wa maisha wa Messi ulikuwa tofauti kabisa na wachezaji wengine bora aliowahi kuwashuhudia.

Boateng anasema hakuwahi kumwona Messi akiingia Gym kufanya mazoezi na mara chache alizoingia ilikuwa ni kwa ajili ya kufanyiwa masaji pamoja na kucheza mpira wa kikapu.

DEMBE 02

Anaeleza licha ya kutofanya mazoezi kwa asilimia mia, lilipokuja suala la kucheza uwanjani, alikuwa ni kama jini, hakuwa anachoka, muda wote alikuwa akikimbia na ukimsahau kidogo tu anakuadhibu.

Mtindo huo wa maisha anasema uliathiri vipaji vya wachezaji wengi wachanga waliokuwa wanachipukia Barcelona.

“Wakati ule kulikuwa na Ansu Fati na Dembele, ndio walikuwa wachezaji vijana pale, wengi walipotea kwa kufuata mtindo wa Messi, hawakuwa wanafanya mazoezi na wakakumbana na hali ya majeraha ya mara kwa mara.”

Mtindo huo wa maisha pengine ulitengenezwa kwa ajili ya Messi pekee na hiyo ilionyesha dhahiri kwani muda mwingi sana kilichokuwa kinawamaliza Dembele na Ansu ilikuwa ni majeraha. Hawa walikuwa ni wachezaji waliotarajiwa kufanya makubwa zaidi katika kikosi cha Barca lakini walipotea haraka kuliko isivyotarajiwa.

DEMBE 03

Dembele alikuwa mtu wa bata sana, kuchelewa mazoezini ilikuwa kawaida yake, kupigwa faini ilikuwa ndiyo utaratibu wake.

Aliinjoi maisha. Katika sherehe za juzi, alisema hata yeye alijikatia tamaa. Mama yake wakala wake bado waliendelea kuamini katika kipaji chake.

Haikuwa ajabu kuona Dembele akiondoka Barcelona, pengine ilikuwa lazima iwe hivyo ili kubadilisha akili yake. Inaelezwa mtindo wa maisha ya PSG pamoja na ule wa Dembele kwa sasa umebadilika sana. PSG baada ya kuwekeza sana kusajili mastaa ilipoamua kuachana na mpango huo wa kuwa na Messi, Neymar ilibadilisha pia mtindo wa maisha yao.

Kwa sasa wanafuatilia wachezaji wao wanalala saa ngapi, muda gani wanakula, wanakula nini, je mwili unakosa kitu gani muhimu jambo ambalo kwa zamani ilikuwa ni tofauti, mastaa wengi wakubwa kutokana na majina yao hawakuwa wanachungwa.

Vilevile watu wa karibu na Dembele wanasema aina ya mtindo wa maisha ya staa huyo kwa sasa umebadilika sana, aliacha kabisa kujiangalia kwenye kioo na kujiona Messi.

Mara kadhaa huwa wa kwanza kufika mazoezini, hufanya mazoezi yake binafsi kabla ya mazoezi ya timu.

Upande mwingine wa shilingi unasema, Dembele alibadilika baada ya kuoa. Mkewe Rima Edbouche alimsaidia kubadilika, kuanzia mtindo wa vyakula na muda wa kupumzika.

Mabadiliko hayo yanadaiwa kuchangia sana utimamu wa kimwili ambao yupo nao kwa sasa. Licha ya kwamba bado amekuwa akipata majeraha lakini kwa kiasi kikubwa siyo kama alivyokuwa Barcelona.

DEMBE 04

Msimu uliopita alicheza mechi 59, akafunga mabao 37 na kutoa asisti 14, na katika msimu huu hadi sasa ameshacheza mechi nane, amefunga mabao manne na kutoa asisti tatu.

Msimu uliopita pia alishinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa Ligue 1, mfungaji bora wa Ligue 1 na mchezaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Vilevile aliisaidia PSG kushinda taji la Ligi ya Mabingwa, Ligi Kuu Ufaransa, Coupe de France na French Super Cup.


KUHUSU BALLON D’OR

Mbali ya tuzo ya mchezaji bora aliyopata Dembele iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu, katika upande wa tuzo ya kipa bora Gianluig Donnarumma alichaguliwa kipa bora.

Donnarumma ambaye kwa sasa anaichezea Manchester City, ameshinda tuzo hiyo kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita na alisimama katika milingoti mitatu wakati PSG ikishinda mataji matatu msimu uliopita ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kufika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu.

Pia Kocha wa PSG, Luis Enrique alichaguliwa kocha bora kutokana na kiwango ambacho PSG ilikionyesha msimu uliopita ikiwa chini yake.

Staa wa Barcelona, Lamine Yamal alishinda tuzo ya mchezaji bora kijana kwa mara ya pili mfululizo baada ya kushinda pia mwaka jana.

Watu wengi walikuwa wakimshindanisha na Dembele wakiamini alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa mwaka kutokana na kiwango alichoonyesha akiwa na timu ya taifa ya Hispania mwaka jana ambapo aliisaidia kushinda taji la Euro, pia kiwango alichoonyesha akiwa na Barcelona.

Straika wa Arsenal, Viktor Gyokeres alishinda tuzo ya mfungaji bora baada ya kufunga mabao 54 katika mechi 52 za michuano yote akiwa na Sporting Lisbon msimu uliopita.

Tuzo hiyo inayoandaliwa Shirikisho la Soka Ufaransa na lile Ulaya (UEFA), inajumuisha kikombe cha Ballon d’or ambacho kinakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 3,500, ingawa hakitengenezwi kwa dhahabu moja kwa moja.

Hata hivyo, washindi huwa hawapewi pesa moja kwa moja, lakini faida ya kushinda Ballon d’or ni kubwa. Klabu mara nyingi hutoa bonasi na motisha kwa wachezaji wanaotajwa, na kampuni nyingi huingia mikataba ya ubalozi wa mamilioni ya pesa kwa wachezaji wanaoshinda tuzo hizo.