Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MEDDIE KAGERE; Simulizi yake ya kusisimua akimtaja Doumbia, Shalulile

Muktasari:

  • Viwanja vya Amahoro na Kigali Pele, ambavyo kwa siku zilizopita vilikuwa kitovu cha maelfu ya mashabiki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki na Kati, vilionekana kurejea katika maisha yake ya kawaida.

KULIKUWA na utulivu ndani ya Jiji la Kigali baada ya siku kadhaa za shamrashamra za mashabiki na presha ya mechi za Kombe la CECAFA Kagame 2026, hatimaye mashindano yalikuwa yamesimama kufuatia kukamilika kwa hatua ya makundi. Hiyo ilikuwa kati ya Agosti 2 na 3, 2026.

Viwanja vya Amahoro na Kigali Pele, ambavyo kwa siku zilizopita vilikuwa kitovu cha maelfu ya mashabiki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki na Kati, vilionekana kurejea katika maisha yake ya kawaida.

Hata waandishi wa habari, makocha na wachezaji walikuwa wamepata nafasi ya kuvuta pumzi kabla ya kuanza kwa hatua ya nusu fainali kisha mechi ya mshindi wa tatu na baadae fainali. Kwangu, siku hiyo haikuwa ya kupumzika, nilikuwa na ratiba ya kukutana kwenye Uwanja wa Kigali Pele na mtu ambaye jina lake bado linaishi mioyoni mwa mashabiki wengi wa Simba. Huyu si mwingine bali ni Meddie Kagere.

Tofauti na siku za mechi, hakukuwa na harakati yoyote, Kagere hakuwa na jukumu la kwenda uwanjani kama ambavyo ilikuwa siku nyingine kwa sababu siku hiyo hakukuwa na mchezo wa CECAFA Kagame.

Kwa kipindi chote cha mashindano, alikuwa mmoja wa wachambuzi wa televisheni zinazorusha michuano hiyo, lakini siku ya mapumziko kama hii alikuwa huru kabisa. Huo ukawa wakati mzuri wa kuketi naye kwa mazungumzo marefu yaliyochukua zaidi ya saa tatu.

Alifika kwa utulivu, akiwa amevaa koti, tisheti ndani na jeans, mavazi yaliyomfanya afanane zaidi na mtu aliyekuwa ametoka kukutana na marafiki kuliko mmoja wa washambuliaji waliotikisa viwanja vya Afrika Mashariki kwa zaidi ya muongo mmoja.

Tabasamu lake halikuwa jipya kwangu, lakini kilichonivutia zaidi ni namna alivyokuwa mwepesi wa mazungumzo. Hakukuwa na dalili za mtu anayesumbuliwa na ukweli kwamba kwa sasa hana timu. Badala yake, alionekana kama mtu aliyeridhika na alichokifanya ndani ya soka huku akiamini ukurasa wake bado haujafungwa.

Mara kwa mara simu yake ilikuwa ikiita, watu wakimsalimia au kumtakia siku njema, ishara kwamba licha ya kutokuwa tena uwanjani kila wiki, heshima yake ndani ya soka la Rwanda na Afrika Mashariki bado ipo palepale.

SIKU ANAVYOIANZA

Licha ya kufanya makubwa katika soka la Afrika Mashariki na Kati, Kagere bado anaishi maisha ya nidhamu ambayo yalimjenga tangu akiwa mchezaji anayesaka nafasi.

“Nikimka kwanza huwa naswali kwa sababu najua nikiswali tu ndiyo kama nimeanzisha safari ya siku nzima, ni kama dawa yangu ya kunilinda siku nzima na mabaya yote yanayotokea," anasema Kagere huku akiongeza;

"Baada ya kuswali, sasa huwa nafanya mazoezi, hapo ni saa 12 asubuhi, huwa ni kila siku kabla ya kuendelea na ratiba nyingine, hayo ndio maisha nimekuwa nikiishi."

Kagere anaamini mchezaji mkubwa hajengwi kwa kipaji pekee, bali pia na namna anavyoishi nje ya uwanja. Ndiyo sababu hata akiwa hana klabu kwa sasa bado anajitunza, akiamini nafasi inaweza kutokea muda wowote.

“Siwezi kukaa bila kufanya mazoezi. Hayo ndiyo maisha yangu. Nimezoea tangu zamani, kwa hiyo hata ukiwa huna timu lazima ujitunze kwa sababu hujui kesho itakuwaje," anasema.

MK14, PACMAN, SNIPER HADI TERMINATOR

Katika soka, baadhi ya wachezaji hubaki na jina lao halisi lakini wengine hupewa majina yanayoeleza tabia yao ndani ya uwanja, Kagere ni miongoni mwao.

Safari yake ya soka imeambatana na majina mengi ambayo kila moja lina simulizi yake. Mashabiki wa Tanzania wanamfahamu zaidi kama MK14 na Terminator, lakini hilo si jina pekee alilowahi kuitwa.

Katika maeneo mbalimbali aliyopita, alibeba majina tofauti kutokana na namna alivyocheza na kile ambacho watu walikiona ndani ya uwanja.

“Majina yanatokana na sehemu, wengine walikuwa wananiita kutokana na nguvu nilizokuwa nazo, kasi na namna nilivyokuwa nafanya kazi uwanjani,” anasema Kagere.

Anaeleza kuwa, baadhi walimuita Sniper kutokana na uwezo wake wa kulenga lango, akimaanisha mchezaji ambaye akipata nafasi mara nyingi hakuachi. Pia alipewa jina la Six Cylinder kutokana na kasi yake uwanjani huku Kenya akiwa na jina ambalo mashabiki walimzoea zaidi.

“Kenya wanazoea kuniita Pacman. Rwanda kuna majina mengine, lakini Tanzania ndiyo Terminator na MK14 yanajulikana zaidi," anasema mshambuliaji huyo.

Lakini jina lililobeba uzito mkubwa zaidi lilikuwa Terminator. Kagere anakumbuka siku ambayo mtangazaji wa Azam Tv, Baraka Mpenja, alipoanza kulitumia jina hilo.

“Siku ya kwanza mtu akikuita jina kama hilo unalipokea vizuri kwa sababu si kwa ubaya maana yake wanaona kitu kizuri kwako. Ukipewa jina kama hilo ni kwa sababu kuna kitu wameona," anasema.

Kwa Kagere, majina hayo hayakuwa mzigo bali yalikuwa ishara ya upendo wa mashabiki, anaamini kama mchezaji anapewa jina zuri, ni kwa sababu ameacha kitu kinachowafanya watu wajisikie fahari.

KIDOGO ASAINI YANGA

Kabla hajawa mfalme wa mabao ndani ya Simba, Meddie Kagere alipitia njia ndefu iliyokuwa na maamuzi magumu. Moja ya ndoto zake ilikuwa kucheza Tanzania, lakini safari hiyo haikuja kirahisi kama wengi wanavyoweza kufikiria.

Kagere anasimulia kuwa kabla ya kutua Simba, alikuwa na nafasi ya kucheza Tanzania mapema zaidi, lakini mambo yalibadilika baada ya kupata ofa ya kwenda Afrika Kusini.

“Nilikuwa nimefika Tanzania na kuzungumza na Yanga, nakumbuka kila kitu kilikuwa kimekaa vizuri, lakini baadaye nikapata ofa ya Bidvest Afrika Kusini," anasema.

Wakati huo akiwa bado kijana aliyekuwa anatafuta kujenga maisha yake, aliona nafasi ya Afrika Kusini kama hatua kubwa zaidi kwenye safari yake. Alimweleza mtu aliyekuwa akimsaidia Tanzania kuhusu uamuzi huo na akaelewa.

“Nilimwambia ukweli, kwamba Tanzania na Afrika Kusini kuna tofauti kubwa, nataka kwenda kujenga maisha yangu. Akaniambia sawa cha muhimu ni wewe ujenge maisha yako na familia yako," anasema

Safari yake ilimpeleka Afrika Kusini, baadaye Tunisia, ambako alisaini na klabu kubwa ya Espérance Sportive de Tunis, kabla ya kupitia mataifa mengine na baadaye kurudi Afrika Mashariki. Lakini wakati fulani Kagere alifikia hatua ya kufikiria kuacha soka kabisa baada ya kuona tofauti kubwa kati ya maisha ya soka Ulaya na Afrika.

“Nilifika wakati nikasema bora niache mpira nifanye biashara nyingine, niliona maisha ya Ulaya na Afrika yana tofauti kubwa," anasema.

Hata hivyo, mpira ulikuwa bado unamuhitaji kufuatia kupata tena nafasi kucheza soka la kulipwa Kenya ambako ndipo alianza kujijenga upya na baadaye kuandika historia ambayo ilimfikisha hadi Simba.

WAKATI NILIPOTAKA KUACHA SOKA

Baada ya safari ya kucheza Afrika Kusini, Tunisia, Lebanon na Ulaya, Kagere alifikia hatua ambayo hakufikiria tena kuendelea na soka.

Kwake, tofauti ya mazingira ya mpira kati ya Ulaya na Afrika ilimfanya aanze kujiuliza kama bado alikuwa kwenye njia sahihi.

Kagere anasema baada ya kutoka Ulaya, aliona maisha ya mpira hayakuwa rahisi kama alivyokuwa akifikiria. Alikuwa kijana aliyekuwa na ndoto kubwa, lakini changamoto za maisha zilimfanya aanze kufikiria njia nyingine nje ya soka.

“Nilivyokwenda Ulaya niliona maisha yale na maisha ya Afrika yana tofauti kubwa, nikasema mimi sitaki tena mambo ya kuteseka, bora niachane na mpira nifanye biashara zangu nyingine tofauti," anasema.

Wakati huo tayari alikuwa ameanza kufikiria maisha baada ya soka. Alitaka kuingia kwenye eneo lingine la maisha na hata alikuwa na mpango wa kusoma zaidi ili kujenga maisha nje ya uwanja.

“Nilikuwa nafikiria nisome engineering, niingie kwenye kazi nyingine, niliona labda muda wangu wa mpira umefika mwisho,” anasema mshambuliaji huyo.

Pamoja na hayo, Gor Mahia ambayo awali iliwahi kumfuata ilirudi tena mezani. Wakati wa kwanza Kagere alikataa kwa sababu bado alikuwa na mawazo ya kuendelea Ulaya.

Baada ya mazungumzo na rafiki yake, Francis Kahata aliamua kucheza tena soka kwa muda mfupi.

“Nilimwambia rafiki yangu mimi nimeachana na mpira, lakini akaniambia njoo tu mwaka mmoja ujaribu, nikasema sawa, ngoja nifanye mwaka mmoja tu, " anasema.

Uamuzi huo ambao ulionekana kama wa muda mfupi ndiyo uliokuja kubadili kabisa historia yake. Kagere hakujua kwamba kurudi Kenya kungekuwa mwanzo wa safari mpya ambayo baadaye ingemfikisha kwenye kilele cha soka la Afrika Mashariki.

TERMINATOR ALIPOZALIWA UPYA

Alipofika Gor Mahia, Kagere hakutaka kukimbilia uwanjani, licha ya kuwa na uzoefu mkubwa, alijua mwili wake ulihitaji maandalizi baada ya kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu. Alikuwa anafanya mazoezi binafsi kabla hajajiunga na timu, lakini alifahamu kuna tofauti kubwa kati ya kuwa fiti kimwili na kuwa tayari kucheza mechi za ushindani.

“Nilikuwa nafanya gym, nakimbia na kufanya mazoezi yangu binafsi, kimwili nilikuwa fiti, lakini sikuwa na utimami wa kuchezea mpira," anasema.

Kagere alimweleza kocha kuwa bado hajawa tayari kucheza mechi za kirafiki na kocha huyo alielewa hali yake. Hakutaka kulazimisha kwa sababu alijua thamani ya kumsubiri mchezaji mwenye uzoefu.

“Nilisema mimi sipo tayari kucheza mechi, kocha akanielewa akasema sawa, tunakutegemea kwenye ligi," anasema.

Hata hivyo, mashabiki wa Gor Mahia walianza kuwa na maswali, walikuwa wanataka kumuona mchezaji aliyekuwa ametoka Ulaya akionyesha kile alichokuwa nacho.

Kagere hakukubali kuingia kwenye presha ya mashabiki, aliamini mechi yake ya kwanza ndiyo ingeweza kuamua namna ambavyo angepokelewa.

“Mechi yako ya kwanza ndiyo funguo yako, ukienda ukaharibu mlango huo unaweza ukafungwa, lakini ukienda ukafungua vizuri unaingia salama," anasema.

Hatimaye siku ya kwanza ya ligi ilifika. Kagere alianza benchi kwa sababu aliamini bado hakutakiwa kukimbilia kuonyesha watu uwezo wake kabla hajawa tayari.

Lakini baada ya timu kupata wakati mgumu, kocha alimuita, dakika 20 alizopewa zilitosha kubadilisha kila kitu.

Aliingia uwanjani, akatoa pasi ya bao na kusaidia timu kupata ushindi ndipo mashabiki waliokuwa na mashaka wakaanza kuona kwamba yule mchezaji aliyesemekana hana uwezo bado alikuwa na kitu kikubwa.

“Nilipoingia nilikuwa na ile hali ya kujiamini sana ndani ya dakika 20 tu tukapata ushindi, ndipo watu wakaanza kusema huyu ana kitu," anasema.

MUME WA KISUMU

Baada ya kuanza vizuri Gor Mahia, Kagere alibadilika kutoka mchezaji aliyekuwa anaulizwa uwezo wake hadi kuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa wanaogopwa zaidi Kenya. Msimu wake wa kwanza ulikuwa wa mafanikio makubwa. Alimaliza akiwa miongoni mwa wafungaji bora, akitwaa tuzo mbalimbali na kuanza kujenga heshima yake ndani ya soka la Kenya.

“Nilijikuta niko kwa wale wafungaji bora, msimu ukaisha niko MVP, watu wakaanza kuniona kama niko na uwezo," anasema.

Lakini kabla ya hapo, kulikuwa na kipindi ambacho Gor Mahia ilimkosa baada ya kuamua kuondoka. Kagere alikaa nje kwa miezi kadhaa kabla ya kurejea tena baada ya timu kuona pengo lake.

Aliporudi, mashabiki walimkaribisha kwa namna ya kipekee. Walimpa jina la “mume wa Kisumu” kwa sababu eneo hilo lilikuwa moja ya sehemu ambazo alikuwa akifunga mara kwa mara.

“Kisumu ilikuwa sehemu yangu, nilifika pale mechi zote nilikuwa nafunga ndio maana mashabiki wakasema baba amerudi nyumbani," anasema.

Ushindani wa Gor Mahia na FC Leopards pia ulimfanya awe mchezaji wa kipekee kwa mashabiki. Kila alipokutana na wapinzani hao, alionekana kuwa na uwezo wa kuwatesa. Lakini nyuma ya mafanikio hayo kulikuwa na jambo kubwa ambalo Kagere alijifunza umuhimu wa kuwa na subira na kuheshimu maamuzi ya makocha.

Safari yake Kenya ndiyo iliyompa tiketi ya kwenda hatua kubwa zaidi. Kutoka Gor Mahia, jina lake lilianza kuvuma hadi Tanzania, ambako Simba ilikuwa inatafuta mshambuliaji mwenye uwezo wa kuleta tofauti.

SIMBA ILIVYOMPATA

Baada ya kutengeneza jina kubwa akiwa Gor Mahia, Kagere alifika kwenye hatua ambayo alihitaji changamoto mpya. Miaka mitatu Kenya ilikuwa imemjenga, lakini moyoni alikuwa akitamani kubadilisha mazingira na kujaribu sehemu nyingine.

Wakati huo alikuwa amemaliza msimu akiwa mchezaji bora na mmoja wa wachezaji waliokuwa wakizungumza sana katika soka la Kenya.

Mashindano ya SportPesa Cup yakawa moja ya matukio yaliyomuweka kwenye macho ya klabu mbalimbali.

Katika mashindano hayo ndipo alipokutana na timu za Tanzania, ikiwamo Simba. Kagere anasema aliona namna ambavyo Simba ilikuwa kwenye nafasi nzuri zaidi wakati huo, hasa kutokana na ushiriki wake kwenye mashindano ya Afrika.

“Nilichagua Simba kwa sababu wakati huo ilikuwa inatoka kucheza Ligi ya Mabingwa, niliona vitu nilivyokuwa navihitaji vilikuwa Simba," anasema.

Uamuzi wa kuja Simba haukuwa wa kawaida kwake kwa sababu kulikuwa na timu nyingine zilizokuwa zikimfuatilia ambazo ni Yanga, Singida United na Azam. Lakini kwake, jambo kubwa lilikuwa kutafuta sehemu ambayo ingempa nafasi ya kucheza kiwango cha juu zaidi.

“Mimi nilikuwa naangalia timu ambayo itanisaidia kukua na kucheza mashindano makubwa ndiyo maana nikaona Simba inanifaa zaidi," anasema.

Hata hivyo, kabla ya kutua Msimbazi, kulikuwa na siri kubwa ambayo hakutaka watu wengi waijue. Kagere alijua kama taarifa za mazungumzo yake na Simba zingetoka mapema, mambo yangekuwa magumu upande wa Gor Mahia.

“Nilijua nikisema nimezungumza na Simba mambo yanaweza kubadilika, nilikuwa bado namalizia majukumu yangu Kenya, ndiyo maana nilitaka kila kitu kikamilike kwanza," anasema.

Hatimaye siku ilifika. Kagere akasaini Simba na hapo ndipo ukurasa mpya wa maisha yake ulipoanza ukurasa ambao baadaye ulimfanya kuwa mmoja wa washambuliaji waliopendwa zaidi katika historia ya klabu hiyo.

PRESHA YA MASHABIKI NA JINA LA TERMINATOR

Mchezaji anapotua kwenye klabu kubwa kama Simba, mara nyingi hukutana na jambo moja kubwa matarajio ya mashabiki, Kagere alifika Msimbazi akiwa na rekodi kubwa kutoka Kenya, lakini alijua kwamba jina pekee halitoshi.

Alielewa kuwa mashabiki walitaka kuona matokeo ndani ya uwanja. Wakati huo Simba tayari ilikuwa na washambuliaji hatari kwa wakati huo, Emmanuel Okwi na John Bocco hivyo swali kubwa lilikuwa, Kagere atapata wapi nafasi?

“Nilijua nimekuja kwenye timu kubwa yenye washambuliaji wazuri, mimi sikuja kusema mimi ndiye mwenye timu, nilikuja kufanya kazi, kocha ndiye ataamua nani acheze," anasema.

Kagere anasema alipokea maneno mengi kabla hata hajaanza kucheza. Wengine walikuwa na mashaka kama angeweza kuhimili presha ya Simba. Lakini kwake, hiyo haikuwa mara ya kwanza kukutana na mashaka, alikuwa ameshapitia hali kama hiyo Gor Mahia, ambako awali watu hawakuamini kama angeweza kusaidia timu.

“Watu wanaweza kusema huyu hawezi, huyu atacheza wapi, lakini mwisho wa siku kazi yako uwanjani ndiyo inayojibu," anasema.

Alipofika kambini, kocha Patrick Aussems aliamua kutumia utaratibu wa kawaida kwa mchezaji mpya. Kagere alianza taratibu, akipewa dakika chache kwenye mechi za kirafiki ili kuzoea mfumo wa timu na wachezaji wenzake. Mara nyingi alikuwa akiingia dakika za mwisho.

“Nilikuwa naingia dakika 10, dakika 15 za mwisho kwa sababu makocha wengi wanapenda kuanza na kikosi walichokikuta, halafu wale wengine wanaingia taratibu kuzoea mfumo,” anasema.

Alipoanza kucheza, alianza kuonyesha kwa nini Simba ilimfuata. Mabao yakaanza kuja na mashabiki waliokuwa na maswali wakaanza kumpongeza. Hapo ndipo jina la Terminator likaanza kupata umaarufu mkubwa zaidi Tanzania. Halikuwa tena jina la mashabiki wa maeneo mengine, bali likawa utambulisho wake ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Akawa mfungaji bora ndani mara mbili mfululizo msimu wa 2018-2019 akiwa na mabao 23 na 2019-2020 akiwa na mabao 22.

Kagere alijua kuwa ili kuishi Simba hakuhitaji kuzungumza sana, bali alihitaji kufanya kazi. Na hilo ndilo alilolifanya kuacha miguu yake izungumze.

HUKU KAGERE NA BOCCO, KULE OKWI

Msimu wa 2018-2019 ulipoanza, nafasi ilimjia Kagere baada ya John Bocco kupata majeraha. Ghafla mchezaji aliyekuwa akisubiri nje akajikuta akipewa nafasi ya kuonyesha thamani yake.

Mechi ya Ngao ya Jamii ikawa mwanzo wa safari yake rasmi. Kagere alianza na kuonyesha kwa nini Simba ilikuwa imemsajili.

Baada ya hapo alicheza mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Prisons, ambako alipata nafasi nzuri na kuitumia ipasavyo.

Anakumbuka namna Bocco alivyomsaidia kabla hata hajafunga bao lake la kwanza.

“Bocco aliniambia mikimbio yako hii ukicheza na mimi utafunga magoli mengi,” anasimulia Kagere na kuongeza.

“Nilipata nafasi moja, nikapiga shuti likaingia, kitu cha kwanza nilisema Mungu nimefungua mlango mzuri,” anasema.

Bao hilo lilikuwa mwanzo wa safari yake ya kutengeneza historia baadaye alianza kufunga mfululizo na kuwa mmoja wa washambuliai hatari.

Lakini siri kubwa ya mafanikio yake haikuwa tu uwezo wa kufunga. Ilikuwa ni namna ambavyo Simba ilikuwa na washambuliaji waliotofautiana.

Kwa Kagere, yeye alikuwa mshambuliaji wa kuingia kwenye nafasi na kumalizia.

“Staili yangu mimi ni kuomba kwenye nafasi, mbele ya goli niwe sehemu sahihi. Mimi ni box striker,” anasema.

Kwa upande mwingine, Bocco alikuwa mshambuliaji mwenye uwezo wa kushikilia mpira, kupambana na mabeki na kuhusisha wenzake kwenye mchezo.

“Bocco anaweza kulinda sana mpira, anaweza kuchezesha wengine. Mimi sio staili yangu hiyo, mimi nataka nafasi na kumaliza,” anaongeza.

Huo utofauti ndiyo uliowafanya wafanye kazi pamoja badala ya kugombania nafasi.

Siri ya Kagere, Bocco na Okwi kuwa hatari

Mara nyingi washambuliaji wanaocheza nafasi moja huwa na ushindani mkubwa. Wengine huanza kuona mwenzake kama tishio kwa nafasi yake.

Lakini ndani ya Simba ya kipindi hicho, hali ilikuwa tofauti.

Kagere anasema walikuwa na kitu kimoja kikubwa walikuwa wanaelewa kwamba mafanikio ya timu yalikuwa muhimu kuliko mafanikio ya mtu mmoja. “Kiukweli sisi tulikuwa wachezaji wenye uzoefu, tulikuwa tunajua tunahitaji nini kama timu, sio wewe unahitaji nini,” anasema.

Kwao, haikuwa muhimu nani angefunga bao, muhimu ilikuwa Simba ishinde.

“Mimi nifunge lakini timu ifungwe haina maana lakini tukifanikiwa timu inapata ushindi, kila mtu anaonekana amesaidia,” anaongeza.

Kagere anakumbuka walikaa chini kama washambuliaji na kufanya mazungumzo yao binafsi. Waliona kwamba kama kila mmoja angejaribu kuwa shujaa pekee yake, timu ingeumia. Ndani ya kundi hilo, Kagere anamtaja John Bocco kama mtu aliyekuwa na sifa za uongozi.

“Bocco ni mtu mwenye kutafuta wengine wafanikiwe, akiona kitu kibaya atakuambia. Huyo ndiyo kiongozi,” anasema.

Kwa Kagere, huo ndiyo ulikuwa msingi wa Simba iliyokuwa ikitawala Tanzania na kufanya vizuri Afrika. Haikuwa tu kuhusu vipaji, bali ilikuwa kuhusu wachezaji waliokuwa tayari kusaidiana.

MFUMO MPYA ULIVYOBADILI MAISHA YA WASHAMBULIAJI

Kwa nini Kagere anaona namba tisa imekuwa ngumu kufunga? Katika miaka ya hivi karibuni, soka limebadilika.

Mfumo wa timu nyingi umebadilika kutoka kutegemea mshambuliaji wa mwisho pekee hadi kutumia washambuliaji wanaoshuka chini, wanaotengeneza nafasi na kusaidia ujenzi wa mashambulizi.

Kwa Kagere, hilo limechangia kupungua kwa idadi kubwa ya mabao kutoka kwa washambuliaji wa kati.

“Siku hizi mifumo imebadilika. Wengi wanatumia viungo zaidi, mshambuliaji anakuwa kama sehemu ya mfumo tu,” anasema.

Anatoa mfano hata kwa timu kubwa duniani ambako washambuliaji wa kawaida wa namba tisa wamekuwa wachache.

“Ukiangalia hata Kombe la Dunia, unakuta Mbappe anatafuta mabao lakini mtu kama Messi ambaye ni kiungo mshambuliaji naye anaingia kwenye orodha ya wafungaji,” anasema.

Kwa Kagere, mshambuliaji wa aina ya zamani anayesubiri ndani ya boksi na kufunga kwa wingi sasa amekuwa adimu.

“Huyo namba tisa kabisa siku hizi ni ngumu kumpata,” anasema lakini bado anaamini kitu kimoja hakijabadilika mshambuliaji lazima awe na ujasiri.

UJUMBE WA TERMINATOR

Baada ya uzoefu wa zaidi ya muongo mmoja kwenye soka la ushindani, Kagere anaamini changamoto kubwa kwa washambuliaji wengi vijana ni kukosa kujiamini.

Kwake, hakuna mshambuliaji anayefanikiwa bila kupitia kipindi cha kukosa mabao.

“Kitu cha kwanza lazima ujiamini kama unaweza na usipojaribu huwezi kufanikiwa,” anasema.

Anaeleza kwamba hata washambuliaji wakubwa duniani hukosa nafasi tofauti ni kwamba hawaruhusu kosa moja liwanyang’anye ujasiri.

“Kubali ukosee, leo umekosa, kesho jaribu tena, mwisho wa siku utafanikiwa,” anasema.

Kwa Kagere, bao ndilo linatoa ladha ya mpira. “Bila goli watasema hatuna mshambuliaji. Bila goli mchezo unakuwa mbaya,” anasema.

Ndiyo maana anaona mshambuliaji ana jukumu kubwa zaidi kuliko wengine kwa sababu dakika 90 zinaweza kuamuliwa na sekunde moja ya utulivu mbele ya lango.

SIKU ALIYOAGWA KWA HESHIMA

Baada ya miaka kadhaa ya mafanikio ndani ya Simba, ilifika siku ambayo Kagere alilazimika kuagana na klabu ambayo ilikuwa imempa nafasi ya kuandika historia kubwa katika soka la Tanzania.

Lakini tofauti na wachezaji wengi ambao huondoka kimya kimya baada ya kumaliza safari yao, Kagere alipata heshima ya aina yake. Aliitwa kwenye tukio maalum la Simba Day, siku ambayo mashabiki wa klabu hiyo walipata nafasi ya kumuaga rasmi.

Kwa Kagere, haikuwa siku ya huzuni, bali ilikuwa siku ya kuthibitisha kwamba uhusiano wake na Simba ulikuwa umevuka mipaka ya mkataba wa kazi.

“Nilivyoitwa Simba Day nilifurahi sana kwa sababu kama kuna kitu nilichokizoea ni kucheza kwenye uwanja uliojaa mashabiki. Ile sauti yao inanipa nguvu na kunipa morali,” anasema.

Lakini kilichomgusa zaidi ni namna ambavyo klabu ilivyompa nafasi ya kuondoka kwa heshima.

Anasema simu aliyopokea kutoka kwa viongozi wa Simba wakati wakija Rwanda kwa ajili ya michuano ya Kagame ilimfanya ajione bado anathaminiwa.

“Waliponipigia wakaniambia tupo nyumbani leo tunakuhitaji. Nikasema sawa, nitakuja. Lakini sikujua kama walitaka mimi ndiyo niwapokee wachezaji,” anasema.

Kwa Kagere, ilikuwa ishara kubwa kwamba hata baada ya kuondoka bado jina lake lilikuwa na nafasi ndani ya familia ya Simba.

“Walionyesha heshima na upendo. Kwangu mimi ni kitu kikubwa sana. Walinifanya nijisikie bado upo moyoni mwetu, bado tunakufikiria,” anasema.

Kwake, kitendo hicho kilikuwa zaidi ya zawadi. Kilikuwa ujumbe kwamba miaka aliyotumia Msimbazi haikupotea.

HAKUONDOKA KWA UGOMVI

Katika maisha ya soka, kuondoka kwa mchezaji kwenye klabu kubwa mara nyingi huambatana na maneno mengi.

Wengine huondoka kwa migogoro, wengine huacha uhusiano ukiwa umeharibika. Lakini Kagere anasisitiza kwamba safari yake na Simba ilimalizika kwa heshima.

“Sehemu ukitoka vizuri ni rahisi kurudi. Kuna wengine wakitoka mambo yanakuwa tofauti kwa sababu hakuna ule muunganiko tena,” anasema.

Kwa upande wake, anaamini miaka aliyokaa Simba ilijenga uhusiano mkubwa kati yake na mashabiki.

Alikuwa sehemu ya kizazi kilichoipa Simba mafanikio makubwa ndani na nje ya Tanzania.

Alikuwa sehemu ya timu iliyofika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ambayo iliongeza heshima ya klabu hiyo kimataifa.

SIMBA YA SASA INAHITAJI MUDA

Baada ya kuondoka kwake, Kagere ameendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Simba. Anaamini changamoto kubwa ambayo klabu hiyo imekuwa nayo katika miaka ya karibuni ni kubadilisha misingi mara kwa mara.

Kwa mujibu wake, timu iliyokuwa na mafanikio wakati wake ilijengwa kwa muda mrefu, wachezaji walielewana, walijua tabia za wenzao na mfumo wa kocha ulikuwa tayari umeingia ndani ya kikosi.

Anasema kujenga timu mpya kila msimu kunahitaji uvumilivu kwa sababu wachezaji na makocha wanahitaji muda kuzoeana.

“Wakati mwingine ukibadilisha timu yote unakuwa kama unaanza upya. Kocha anakuja na mfumo wake, wachezaji wanakuja na mawazo yao, hivyo inahitaji muda ili kila kitu kikae sawa,” anasema.

Kagere anatoa mfano wa kipindi chake Simba ambacho walifika hatua kubwa Afrika. Anasema wakati huo hawakuwa wamejenga mafanikio kwa siku moja, bali walikuwa wamekaa pamoja na kuelewana.

“Tulikuwa na timu ambayo ilikuwa imekaa muda. Kila mtu alijua mwenzake anataka nini. Ukiwa na timu kama hiyo hata ukiongeza mchezaji mmoja au wawili ni rahisi kuingia kwenye mfumo,” anasema.

Kwa sasa anaamini Simba bado ina ubora wa kufanya vizuri, lakini inahitaji kuipa nafasi timu iliyopo kujengwa.

“Wakipata muda wa kuzoeana wanaweza kufanya vizuri kwa sababu ubora upo,” anasema.

KUHUSU IBRAHIM DOUMBIA

Katika kikosi cha sasa cha Simba, mmoja wa wachezaji waliomvutia Kagere ni mshambuliaji mpya Ibrahim Doumbia.

Mshambuliaji huyo alipata nafasi kubwa kwenye mechi ya mwisho ya Kombe la CECAFA Kagame dhidi ya Singida Black Stars, ambako alifunga bao lake la kwanza akiwa na jezi ya Simba.

Kwa Kagere, bao hilo linaweza kuwa mwanzo mzuri kwa sababu kwa mshambuliaji kuanza kwa kufunga kunaongeza hali ya kujiamini.

“Kitu cha kwanza anaweza kufunga kwa kichwa, ana kasi na ana uwezo. Kitu muhimu kwake ni kupata muda,” anasema.

Anaamini mshambuliaji anahitaji kuaminiwa na kupewa nafasi ili aweze kuonyesha ubora wake.

“Kuna tofauti kubwa kati ya mshambuliaji anayefunga na yule anayekosa. Ukifunga unapata kujiamini, lakini ukikosa sana unaweza kuanza kuogopa hata kuomba mpira,” anasema.

Kwa Kagere, Doumbia ana vitu muhimu vinavyohitajika kwa mshambuliaji wa kisasa. Ana urefu, uwezo wa kucheza mipira ya juu na anaweza kushambulia nafasi. “Ni suala la muda tu. Akipata mazingira mazuri anaweza kusaidia Simba,” anasema.

SHALULILE NA CHANGAMOTO YA KUISHI TANZANIA

Wakati Simba ikiendelea kujenga kikosi chake, mpinzani wake mkubwa Yanga nayo imeendelea kufanya usajili mkubwa.

Moja ya majina makubwa yaliyoingia Tanzania ni mshambuliaji Peter Shalulile, aliyekuwa akicheza Afrika Kusini.

Kagere anamfahamu vizuri mshambuliaji huyo na anakiri kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao.

Anasema Shalulile ameonyesha kiwango kikubwa akiwa na Mamelodi Sundowns, lakini changamoto kubwa kwake itakuwa kuzoea mazingira mapya.

“Mchezaji anaweza kuwa mzuri sehemu fulani, lakini akienda sehemu nyingine lazima aangalie suala la adaptation,” anasema.

Kwa Kagere, si kila mchezaji anayefanya vizuri nje anaweza kuja moja kwa moja na kuendelea kufanya vizuri bila kupitia kipindi cha kuzoea.

“Ligi ni tofauti, maisha ni tofauti, timu ni tofauti. Lazima aingie kwenye mfumo wa Yanga na Tanzania kwa ujumla,” anasema.

Hata hivyo, anaamini ubora wa Shalulile hauwezi kupuuzwa.

“Ni mshambuliaji mzuri, ana uwezo mbele ya lango. Kikubwa ni muda wa kuzoea,” anasema.

UBINGWA WA CAF KWA SIMBA, YANGA

Kwa miaka ya karibuni, soka la Tanzania limeanza kupanda hatua baada ya Simba na Yanga kwa vipindi tofauti kila mmoja kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa Kagere, mafanikio hayo si bahati, bali ni matokeo ya uwekezaji na ushindani uliopo ndani ya ligi.

Anasema ligi ya Tanzania sasa imekuwa na ushindani mkubwa kutokana na uwepo wa timu zenye uwezo kama Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars.

“Ligi kila siku inabadilika, upinzani ukiwa mkubwa unasaidia timu zote kukua,” anasema.

Anaamini ushindani kati ya Simba na Yanga umeongeza kiwango cha soka la nchi.

“Simba ilipofika hatua kubwa Afrika, Yanga nayo ikaona kwa nini isiwe sisi. Wakawekeza nao wakafika fainali. Huo ndiyo ushindani unaosaidia,” anasema.

Kwa mtazamo wake, Tanzania ipo kwenye njia sahihi kuelekea kushindana zaidi Afrika.

“Ukifika robo fainali leo, kesho unafikiria nusu fainali, ukifika nusu fainali unafikiria fainali. Ndiyo namna timu zinavyokua,” anasema huku akidai hawezi kushangaa siku moja klabu hizo zikitwaa ubingwa wa michuano hiyo ya CAF.

KUTOKA SIMBA HADI MAISHA YA SASA

Baada ya miaka ya mafanikio akiwa Simba, Kagere ambaye pia aliichezea Namungo, anabaki na kumbukumbu kubwa ya safari yake ndani ya klabu hiyo. Alitoka kuwa mchezaji aliyekuwa na maswali mengi hadi kuwa mmoja wa washambuliaji waliopendwa na kuheshimiwa.

Lakini kwa sasa, akiwa hana timu, Kagere anaangalia maisha kwa mtazamo mpana zaidi. Kwake, soka ni safari yenye hatua tofauti na kila kipindi kina ujumbe wake.

“Mpira bado ninao moyoni, siwezi kusema nimefunga mlango kwa sababu bado ninaupenda kwa sasa nimejikita zaidi kwenye biashara zangu, " anasema.

Mbali na biashara ambazo anafanya, Kagere anasomea ukocha kama ilivyo kwa Haruna Niyonzima pia akisoma na masomo ya uskauti ili kujiandaa na maisha baada ya kutundika daruga.