Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matano ya Simba, Yanga kuipa uzito Kagame

KAGAME Pict

Muktasari:

  • Miaka kadhaa iliyopita, kushiriki michuano ya Kagame ilikuwa heshima kwa klabu za ukanda wa CECAFA. Ilikuwa ni michuano iliyokuwa ikikusanya mabingwa na vigogo wa eneo hili huku ushindani wake ukiwapa wachezaji nafasi ya kujiandaa kwa msimu mpya na wakati huohuo kuwapa mashabiki burudani ya kiwango cha juu.

BAADA ya Ijumaa iliyopita kupigwa fainali ya Kombe la CECAFA Kagame kati ya Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sports ya Rwanda, swali kubwa linaloendelea kusalia vichwani mwa wengi ni nini kifanyike ili mashindano hayo yarudishe hadhi yake na kuanza kuvutia tena klabu kubwa za Afrika Mashariki na Kati kama Simba na Yanga?

Miaka kadhaa iliyopita, kushiriki michuano ya Kagame ilikuwa heshima kwa klabu za ukanda wa CECAFA. Ilikuwa ni michuano iliyokuwa ikikusanya mabingwa na vigogo wa eneo hili huku ushindani wake ukiwapa wachezaji nafasi ya kujiandaa kwa msimu mpya na wakati huohuo kuwapa mashabiki burudani ya kiwango cha juu.

Lakini kadri miaka ilivyopita, hali imebadilika, klabu zimeanza kuiona Kagame kama sehemu ya maandalizi ya msimu badala ya mashindano ya kushindania ubingwa.

Nyingine zimekuwa zikikataa kabisa kushiriki na badala yake kuchagua kambi za nje ya nchi au kuendelea na maandalizi yao nyumbani.

Mfano kwa miaka ya hivi karibuni ni klabu za Simba na Yanga. Simba ilikubali kushiriki michuano ya mwaka huu kwa kiasi kikubwa kutokana na ratiba kubana, hivyo hawakuwa na chaguo lingine. Kama isingekuwa hivyo, huenda nayo ingechagua njia nyingine.

Yanga, kwa upande wake, iliamua kubaki Tanzania na kuendelea na maandalizi yake badala ya kwenda Kigali. Azam nayo haijashiriki, hata hivyo, imepiga kambi Kigali, Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.

Mwaka jana, Simba, Yanga na Azam hazikushiriki licha ya mashindano kufanyika Dar es Salaam. Singida Black Stars ilishiriki kama ilivyo mwaka huu.

Hiyo pekee inaonyesha kwa sasa michuano ya CECAFA bado haijafikia kiwango cha kuwafanya vigogo hao waione kama kipaumbele.

Hata hivyo, ujio wa Rais mpya wa CECAFA, Paulos Weldehaimanot Andemariam, unaonekana kuleta matumaini mapya. Tangu alipochukua nafasi hiyo Februari 2026, amekuwa akizungumza wazi kuhusu dhamira ya kuibadilisha CECAFA na kuirejesha kwenye hadhi yake ya zamani.

Kauli yake ya kukiri kwamba kuchelewa kwa malipo ya fedha za zawadi kumeharibu taswira ya mashindano ni ishara uongozi mpya umeanza kutambua chanzo cha tatizo badala ya kukificha.

Iwapo CECAFA inataka kuona Simba, Yanga na klabu nyingine zikianza kuyapa uzito mashindano hayo, kuna mambo matano ambayo hayawezi kuepukika.

KAGA 02

KULIPA FEDHA ZA ZAWADI KWA WAKATI

Hakuna jambo linaloharibu imani ya washiriki kuliko kushinda halafu ukasubiri miezi au mwaka mzima kupata fedha zako.

Mpaka sasa, Singida Black Stars bado inasubiri dola 30,000 ilizoahidiwa baada ya kutwaa ubingwa wa Kagame Cup 2025. Hilo limekuwa moja ya malalamiko makubwa dhidi ya CECAFA.

Andemariam amekiri wazi hali hiyo haiwezi kuendelea ikiwa mashindano yanataka kuheshimika.

Klabu zinahitaji uhakika, zinapotumia mamilioni ya fedha kwa posho na maandalizi, zinapaswa kujua zitapata haki zao mara tu mashindano yanapomalizika, huo ndio msingi wa kujenga uaminifu.

KAGA 03

KUONGEZA THAMANI YA FEDHA ZA ZAWADI

Katika soka la sasa, ukubwa wa mashindano hupimwa pia na thamani ya zawadi zake, kama mshindi wa Kagame ataendelea kupata kiwango kidogo cha fedha ukilinganisha na gharama zinazotumiwa na klabu kushiriki, itaendelea kuwa vigumu kwa timu kubwa kuona faida ya kushiriki.

Kuongeza zawadi hakutawavutia klabu pekee, bali pia kutatoa sababu kwa wadhamini, vituo vya televisheni na washirika wa biashara kuwekeza zaidi katika mashindano hayo.

Fedha kubwa huongeza ushindani na ushindani huongeza thamani ya mashindano.

KAGA 01

RATIBA INAYOZINGATIA KALENDA YA CAF

Hii ndiyo sababu ambayo mara nyingi haizungumzwi sana, kila msimu, Simba na Yanga hujiandaa kwa Ligi ya Mabingwa Afrika, mashindano ambayo yana umuhimu mkubwa zaidi kiushindani na kifedha.

Iwapo ratiba ya Kagame itaendelea kugongana na mipango ya maandalizi ya CAF, klabu zitaendelea kuyaona mashindano hayo kama mzigo.

CECAFA inapaswa kushirikiana kwa karibu na CAF ili kupata dirisha ambalo halitawalazimisha makocha kuchagua kati ya maandalizi ya msimu na kushiriki michuano ya Kagame.

KAGA 04

HADHI YA KIMATAIFA

Rwanda imeonyesha mfano mzuri wa uandaaji wa mashindano, viwanja vya kisasa, hoteli bora, usafiri wa uhakika na mazingira mazuri kwa timu ni mambo ambayo yanawafanya washiriki wajisikie kuthaminiwa.

Lakini hilo pekee halitoshi, CECAFA inapaswa kujenga chapa ya Kagame kama mashindano ambayo kila klabu inataka kushiriki si kwa sababu tu yanachezwa Afrika Mashariki, bali kwa sababu yanatoa mazingira yanayofanana na yale ya mashindano makubwa ya CAF.


KLABU ZA KANDA NYINGINE

Hili linaweza kuwa jambo litakalobadilisha kabisa taswira ya mashindano, Andemariam tayari ameonyesha nia ya kuona siku moja Kagame ikizikutanisha klabu kutoka CECAFA na zile za COSAFA, WAFU, UNAF au UNIFFAC.

Fikiria mashindano yenye Simba, Yanga, Gor Mahia, APR, TP Mazembe, RS Berkane au Orlando Pirates katika kipindi cha maandalizi ya msimu.

Mbali na kuongeza ubora wa mechi, hatua hiyo ingeongeza watazamaji, wadhamini, mapato ya televisheni na hata thamani ya ubingwa wenyewe.

Kwa klabu kubwa, kushiriki mashindano yenye ushindani mkubwa huwa sehemu ya maandalizi bora kuliko kucheza mechi za kirafiki zisizo na presha.

Hakuna anayetarajia mabadiliko haya yatokee kwa siku moja lakini jambo la muhimu ni kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, uongozi wa CECAFA umeanza kukiri hadharani changamoto zilizokuwa zikilikabili Kombe la Kagame na kuweka wazi dhamira ya kuzitatua.

Sasa kinachosubiriwa si ahadi nyingine, bali utekelezaji kwa sababu siku ambayo CECAFA itahakikisha zawadi zinalipwa kwa wakati, itaongeza fedha za ushindi, itapanga ratiba rafiki, itaendelea kuboresha uandaaji na kufungua milango kwa klabu kutoka kanda nyingine, ndipo Kombe la Kagame litarejea kuwa mashindano ambayo Simba, Yanga na vigogo wengine wa Afrika Mashariki hawatayashiriki kwa sababu ya kulazimika, bali kwa sababu watayaona kama sehemu muhimu ya mafanikio yao.

KAGA 05

WADAU WANASEMAJE?

Boniface Bigirimana, mmoja wa wadau wa soka Rwanda, alisema; "Kagame ni mashindano yenye historia kubwa katika ukanda wetu. Ili yarudi kwenye hadhi yake, ni muhimu CECAFA ihakikishe inatimiza wajibu wake kwa klabu zinazoshiriki, klabu zikiona kuna weledi katika uendeshaji, zitayapa uzito zaidi."

Kwa upande wake kocha Mtanzania anayeishi Rwanda, Baraka Hussein alisema: "Klabu kama Simba na Yanga siku hizi zinaangalia zaidi ubora wa maandalizi kuliko jina la mashindano kama Kagame itaongeza ushindani, zawadi na kushirikisha timu zenye ubora mkubwa kutoka kanda nyingine, hakuna sababu ya vigogo hao kutoshiriki kwa vikosi vyao kamili."