Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa wa Stars na tabia zao tofauti Kigali

JICHO Pict


NIPO Kigali na mastaa mbalimbali wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Kuna mambo mengi ambayo ninayatazama kwa jicho la mwewe kuhusu wachezaji wetu. Tabia zao na maisha yao kwa ujumla.


Tuanze na nani? Aishi Manula. Anaonekana amerudi katika furaha yake. Ndani na nje ya uwanja. Amekuwa mcheshi na anaonekana yupo katika ari yake ya kawaida. Maisha yake katika klabu yake ya mwisho Simba hayakuwa mazuri sana kiasi kwamba kimwili na kiakili hakuonekana kuwa sawa sana. Aishi wa sasa anaonekana kuwa na furaha.


Kutoka Dar es salaam hadi Kigali ndani ya ndege alikuwa anacheza mchezo unaoitwa Ludo pamoja na staa mwezake, Fei Toto. Alionekana kuwa na furaha muda wote. Ni tofauti nilivyowahi kuambiwa kwamba kuna wakati alipata shida ndani ya ndege akiwa na timu yake ya zamani. Hakikuwa kitu cha kawaida sana.

Kitu ambacho kimenishangaza kidogo kwa Aishi ni urafiki wake wa karibu na kipa mwingine wa Taifa Stars ambaye anacheza naye katika Klabu ya Azam, Zuberi Foba. Wote wako hapa na ni marafiki wazuri tu. Mara nyingi makipa wanaowania namba huwa sio marafiki wazuri na kila mmoja huwa anajiona anastahili kucheza kuliko mwenzake.

Juma Kaseja na Ivo Mapunda hawakuwa marafiki wakati wanawania nafasi katika kikosi cha Marcio Maximo. Urafiki wao ulikuja baada ya siku zao za ubora kumalizika. Labda ni vile pia Aishi hamchukulii Foba kama mpinzani wake. Nadhani anamchukulia kama mdogo wake. Nadhani anaona hana miaka mingi ya kuwa katika ubora wake.

Mwingine? Kelvin John. Huyu tulimuita Mbappe wetu. Kelvin anaonekana kujenga vizuri mwili wake. Ameachana na mwili wa utoto na sasa na misuli timilifu ya kucheza kiwango cha juu. Inaonekana pia anajitambua kwa sababu sikuwahi kumuona Kelvin akicheza kiwango bora katika jezi ya timu ya taifa kama alivyocheza katika kipindi cha kwanza cha pambano dhidi ya Liechtenstein.

JICH 02

Inaonekana ligi ya Denmark imemchangamsha zaidi. Kama akiendelea kucheza katika kiwango hiki si ajabu akawa msaada mkubwa kwetu kama ambavyo tuliamini kwamba angejaribu kuvaa viatu vya Mbwana Samatta wakati ule akiwa anachipukia katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17.

Tukiachana na yeye kuna Fei Toto. Hajawahi kuwa ‘serious’ na maisha. Na kama inasemwa na wanasaikolojia kwamba watu wenye furaha wanaishi maisha marefu basi Fei pia ataishi maisha marefu. Fei hataki maongezi ‘serious, na muda wote ni mtu wa utani. Tatizo tu limekuwa kumkosa rafiki yake wa karibu, Pascal Msindo ambaye hakuitwa katika kikosi hiki na badala yake nafasi yake imekwenda kwa Nickson Kibabage.

Mtu mmoja pia akaninong’oneza kwamba Fei pia sio mtu wa mazoezi sana. Hapendi zile mbio za mazoezini. Nikaambiwa kwamba makocha wanampanga Fei kutokana na kiwango chake anachoonyesha katika mechi, lakini sio kiwango anachoonyesha katika mazoezi. Kwenye mechi ana maajabu mengi lakini katika mazoezini ni mvivu. Wapo wachezaji wengi wa namna hii hata majuu.

JICH 03

Kitu kingine? Lugha inawatenganisha wachezaji. Kuna wachezaji watatu ambao muda mwingi wanakuwa pamoja. Mzungu wetu, Tarryn Allarakhia, Haji Mnoga na Charles M’Mombwa muda mwingi wanajikuta wamekaa peke yao kwa sababu wanawasiliana kwa lugha ya Kiingereza zaidi. Hauwezi kuwalaumu. Hawajui kuongea Kiswahili. Wameyashika maneno machache ya Kiswahili.

Hauwezi kuwashangaa sana kwa sababu hata wakati fulani Arsenal ilikuwa ina mastaa wengi wa Kifaransa kina Patrick Vieira, Emmanuel Petit, Giles Grimandi na wengineo. Katika mazoezi na nje ya uwanja muda mwingi zaidi walikuwa wanawasiliana wenyewe kwa sababu walikuwa hawafahamu lugha ya Kiingereza. Ni kitu cha kawaida katika mpira na hauwezi kuita ubaguzi.

Kitu pekee ambacho kinanishangaza labda ni urafiki wa Mnoga na Bakari Nondo Mwamnyeto. Kuna nyakati nyingi huwa nawaona pamoja na sijui wanawasiliana kwa lugha gani. Labda Mwamnyeto anafahamu lugha ya Kiingereza. Sina uhakika na hilo, lakini kumekuwa na maongezi ya mara kwa mara kati ya Mwamnyeto na Mnoga ambaye nafahamu haelewi vyema lugha ya Kiswahili.

JICH 04

Kitu kingine ambacho kimenishangaza ni uwezo wa mlinzi wa Azam FC, Twalib Nuru ambaye amepata nafasi ya kuonyesha uwezo wake baada ya Dickson Job na Ibrahim Bacca kuumia. Nuru ni nuru ya taifa. Urefu wake, utulivu wake umemfanya aaminiwe na makocha wawili wakubwa. Kwanza ameaminiwa na Florent Ibenge katika klabu yake, lakini sasa ameaminiwa na Manuel Gamondi katika kikosi cha timu ya taifa.

Anachopaswa kuimarisha ni kasi yake uwanjani. Pambano dhidi ya Liechtenstein alionekana kuzidiwa kasi kidogo lilipokuja suala la kukimbizana na mchezaji mmoja, vinginevyo alikuwa sahihi katika mambo mengi uwanjani. Ni hazina kubwa kwa taifa na nimemchunguza na kugundua kwamba ana nidhamu pia nje ya uwanja. Anaheshimu wakubwa zake. Atafika mbali.

Kitu kingine ambacho nimegundua ni ukweli kwamba umuhimu uliopitiliza kwa wachezaji wa Simba na Yanga katika kikosi cha Taifa Stars umepungua. Sio kitu kibaya sana katika mpira wetu. Tulihitaji bwawa kubwa la kuvua wachezaji. Katika pambano la kwanza dhidi ya Liechtenstein katika kikosi kilichoanza kulikuwa na mchezaji mmoja tu wa Simba, Suleiman Mwalimu. Kulikuwa na wachezaji wawili tu wa Yanga, Mwamnyeto na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

JICH 05

Zamani tuligawanywa zaidi na Usimba na Uyanga katika kikosi cha Taifa Stars kwa sababu kulikuwa na kundi kubwa la wachezaji kutoka katika timu hizo. Sasa hivi hali imebadilika na kuna wachezaji wengi wanakuja kutoka klabu za nje na wamekuwa wakifanya vizuri. Na katika hili, mmoja kati ya wachezaji ambao wamekuwa wakifanya vyema ni Alphonce Mabula. Hongera kwake.

Wachezaji wengine ambao wamekuwa wakitubeba zaidi kwa sasa ni wachezaji wa Azam. Kuna kundi kubwa la wachezaji wa Azam katika kikosi cha timu ya taifa. Foba, Aishi, Idd Nado, Fei Toto, Twalib na Lameck Lawi. Hii ni achilia mbali kina Msindo ambao wameachwa kwa muda tu katika kikosi. Tunajua kwamba watakuwepo mbele ya safari.

Pamoja na kila kitu nimegundua kwamba wachezaji wanapendana. Hawana sana mambo ya utimu katika kambi ya timu ya taifa. Huwa hawajadili habari za timu zao na wanashirikiana mambo mengi kwa pamoja. Kwa wale ambao wanacheza Ligi Kuu Bara upinzani wa timu zao wanauweka kando na wanaangalia zaidi maslahi ya taifa.