Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'Offside' za Dube na Mwalimu, waamuzi wataisha nchini


WALIKAA sehemu fulani mapema wiki hii kujaribu kuwaridhisha Simba na Yanga. Nawazungumzia watu wanaoitwa kamati ya saa 72. Walijaribu kuwapoza wakubwa baada ya mechi yenye vurugu ya kawaida tu pale Unguja. Hakukuwa na jambo la ajabu baada ya mechi.


Kwanza kabisa kuna mswahili aliniuliza kwa nini inaitwa kamati ya saa 72 lakini imechukua maamuzi ya kumfungia Suleiman Mwalimu baada ya siku tisa? Ni kweli inachekesha. Kosa alilofanya Suleiman Mwalimu kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Dodoma Jiji liliendelea kumpa wasaa wa kucheza pambano la Yanga kwa sababu kamati ya saa 72 ilikuwa haijakutana.

Najua utakachoambiwa ukiuliza sababu za adhabu ya Mwalimu kutoka baada ya mechi ya Yanga na si kabla. Lazima utaambiwa wajumbe hawakukutana kwa haraka. Utaambiwa wajumbe wengi walikuwa na udhuru na wengine walikuwa mikoani. Tupo katika dunia ambayo wakubwa wanafanya vikao 'online' katika kitu kinachoitwa zoom meeting lakini sisi lazima tukutane.

Leo kuna mtu yupo Mtwara, mwingine Dubai, mwingine yupo New York na mwingine yupo Jakarta Indonesia lakini wanakubaliana muda wa kufanya kikao na kuchukua maamuzi mazito kama ya kununua kampuni fulani kubwa Japan. Baadae mwanasheria anapewa maelekezo ya nini cha kufanya. Shughuli inakuwa imeishia hapo. Hawahitaji kukutana. Kila mmoja ana mishemishe zake nyingi.

Yanga wana hoja, Mwalimu hakupaswa kucheza katika mechi iliyofuata dhidi yao. Kama ingekuwa kwa wenzetu ilipaswa kuwa hivyo. Lakini huku kwetu Mwalimu sio wa kwanza kunufaika na uzembe wa watu wa kamati ya saa 72 ambao huwa wanakutana kwa tarehe waliyopanga bila ya kujadili uharaka au dharura ya baadhi ya makosa yaliyofanyika na ambayo yanahitaji ufafanuzi kabla ya mechi inayofuata. Iwe kwa mchezaji au kwa mwamuzi au kwa kiongozi fulani.

Siyo kwa Mwalimu tu. Kocha anaweza kufanya vimbwanga leo kisha akakaa katika benchi mechi dhidi ya Coastal Union, halafu mechi ya Namungo, halafu ndio akafungiwa na kukosa mechi za Simba, Mtibwa Sugar na Yanga. Tupo katika dunia hii ya taratibu. Hatuna haraka wala hatupimi athari za mambo mengi.

Kitu kingine ambacho tunaweza kuambiwa na watu wa kamati ni walikuwa wanasubiri ripoti ya kamishna wa pambano ndiyo maana walishindwa kutolea maamuzi mapema. Hilo si ni suala la barua pepe tu kwenda kwa wajumbe mara baada ya kumalizika kwa mechi? Au huwa wanaandika kwa mkono kisha wanaweka katika bahasha na kupeleka TFF kwenyewe?

Lakini nimegundua kamati ya saa 72 inapoleta mkeka wake wa maamuzi huwa inajumlisha matukio mengi tofauti. Kumbe labda huwa wanasubiri kwanza matukio yajae katika makabrasha yao ndio wanapanga siku ya kuja kuamua. Kwa nini kila tukio lisichukuliwe hatua hapo hapo na sio kungoja makabrasha yajae mezani kama meza ya Rais pale Ikulu.  Matokeo yake ndio wanajiweka katika nafasi kama hii ya kuonekana kuwa walipanga kwa makusudi Mwalimu acheze mechi ya Yanga kisha afungiwe mechi zinazofuata.

Sasa tuje katika mechi yenyewe. Kuna mambo mawili hapa. Jambo la kwanza kabisa namna wakubwa wanavyopendelewa. Waamuzi wa pembeni wameadhibiwa kwa makosa ya kukataa bao la Mwalimu, pia kumzuia Prince Dube kufunga akiwa katika nafasi nzuri. Dube hakutuliza mpira wala hakufunga. Kibendera kilikuwa hewani. Waamuzi wamefungiwa miezi mitatu hadi sita.

Tuige kwa wenzetu au tusiige? Kama tukiiga kwa wenzetu basi waamuzi huwa wanaondolewa katika orodha ya waamuzi watakaochezesha mechi za raundi inayofuata.

Hii ni kuwaonya wawe makini. Hauwezi kumfungia mwamuzi miezi mitatu kwa makosa yale. Lakini labda wenzetu wana adhabu ndogo kwa sababu wanaamini waamuzi wao wanakosea kweli kwa bahati mbaya.

Siku hizi hata adhabu hizo hazipo kwa sababu waamuzi wakifanya hayo makosa hapo hapo wanarekebishwa na VAR. Waamuzi wetu wa pembeni siku ile hawakuwa na VAR na hiki kimekuwa kilio kikubwa cha mashabiki wa soka na wadau mbalimbali wanapojadili makosa ya waamuzi. Utasikia tu wachambuzi akina Ramadhan Mbwaduke pale Azam wakisema "Kama kungekuwa na VAR basi mwamuzi angebadili maamuzi yake".

Kwa kilichotokea Unguja nadhani waamuzi walihitaji zaidi msaada wa VAR kwa sababu wazungu wanasema zile ni 'tights call'. Kuna 'offside' za wazi kabisa. Zile za hatua mbili mbele au nyuma. Lakini kuna ambazo zinabana kiasi zinaweza kumdanganya mwamuzi. Sisi wenyewe huwa tunajiona mashujaa wa kujua kuwa mwamuzi hakuwa sahihi kwa sababu tunapata faida ya marudio ya picha mjongeo. Waamuzi hawana nafasi hiyo.

Lakini turudi kwa ile ya Dube. Afadhali ya Mwalimu mpira ulitinga wavuni. Hii ya Dube alikuwa amefanya kitu kinachoitwa na wachambuzi wa sasa mikimbio nyuma ya walinzi. Mwamuzi wa pembeni akaona kama vile ilikuwa offside. Hivi kweli unaweza kumfungia mwamuzi kwa miezi mitatu kwa sababu hiyo? Kama watu wa kamati wakianza kufuatilia hilo jambo kwa makini basi nadhani ligi yetu itakuwa haina waamuzi baada ya miezi miwili tu tangu ianze.

Kule kwa wenzetu mwamuzi wa pembeni angemuacha Dube afunge halafu angenyoosha kibendera chake. Anajua kama alikuwa amekosea basi VAR ingemrekebisha. Kwa hapa ukimuacha afunge halafu ikagundulika kuwa alikuwa ameotea hakuna namna ambayo makosa yako yanaweza kurekebishwa. Labda ndio maana waamuzi wetu walijihami sana katika matukio ya Mwalimu na Dube.

Lakini tujiulize pia. Huwa tunatazama mechi nyingine kibao za Ligi kuu ambazo zinaonyeshwa vema na Azam TV. Mara ngapi kumekuwa na matukio kama ya Dube lakini waamuzi wa pembeni hawafungiwi? Nani anajali kama matukio hayo yanatokea pia katika pambano la Singida Fontaine Gate na Coastal Union pale Manyara? Umewahi kusikia kuna waamuzi wanafungiwa kwa hayo ya offside?

Tunachosikia ni kufungiwa kwa mchezaji fulani kwa kuonyesha imani za kishirikina au kurusha chupa kwa mashabiki au mengineyo. Hatusikii kuna mwamuzi kafungiwa kwa kunyoosha kibendera chake juu kwa Elvis Rupia wakati hakuwa ameotea. Imetokea kwa Dube kwa sababu ilikuwa lazima kuwaridhisha na Yanga. Hata usiku ule tulipojaribu kusema bao la Mwalimu lilikuwa halali jibu lake lilikuwa "mbona hauzungumzii lile la Dube".

Vyovyote ilivyo Simba na Yanga huwa wanawapa maisha magumu TFF, bodi ya Ligi na kamati ya saa 72. Matokeo yake wao wametengewa sheria na kanuni zao, wakati timu nyingine 14 zilizobakia zimetengewa kanuni zao. Wazungu labda waliishi maisha haya miaka tisini iliyopita lakini sisi tunayaishi leo na wakubwa wanazidi kufaidi zao.

Jana ni Machi 8 na imetimia mwaka mmoja tangu Simba walipoghairi ghafla kucheza pambano la Yanga na kweli bodi ya ligi wakahamisha mechi mpaka Machi 15. Yanga nao wakasema hawachezi na kweli hawakucheza. Mpaka Rais wa nchi alipoingilia kati ndipo Simba waliporudi uwanjani kucheza kinyonge tu.  Unadhani Coastal Union au Mashujaa wana ubavu kama huu? Hawana na wala hawawezi kuthubutu kamwe.

Kwa staili hii Simba na Yanga zitaendelea kudeka. Mechi ijayo ya marudiano ikipigwa filimbi Jonathan Sowah ameotea wakati akiwa bado hajaotea mashabiki na mabosi wa Simba watataka mwamuzi msaidizi afungiwe kama ilivyokuwa kwa mwamuzi msaidizi aliyeadhibiwa kwa sababu ya Dube. Ili mradi tu tufananishe matukio na tuendelee kudeka kwa wasimamizi wa mpira.