Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utabiri wa hali ya hewa kuhusu Djigui Diarra na refa wake


UTABIRI wa hali kuhusu kipa wa Yanga, Djigui Diarra, unaonyesha kwamba atafungiwa mechi kadhaa na Kamati ya Saa 72 kwa kosa la kumghasighasi mwamuzi baada ya kumalizika kwa pambano la Yanga na Mtibwa Sugar pale Dodoma.


Diarra atafungiwa mechi ngapi? Kamati itakuwa makini kwa sababu tayari imeshaingia lawamani kwa kumfungia Suleiman Mwalimu wa Simba mechi tatu tu kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Dodoma Jiji katika siku za nyuma.

Kumbuka kwamba Ibrahim Bacca alifungiwa mechi tano kwa kumpiga mchezaji wa Mbeya City pale Uwanja wa Sokoine. Watu wa Yanga wakahoji kwamba kwanini Bacca alifungiwa mechi nyingi na Mwalimu amefungiwa chache. Ina maana safari hii watu wa Kamati ya Saa 72 watajaribu kuwaridhisha Yanga kwa kumfungia mchezaji wao mechi chache. Na Diarra lazima atafungiwa kwa sababu asipofungiwa wapinzani wa Yanga, Simba watahoji kwanini Diarra hajafungiwa. Na huo unaweza kuwa mtego kwa kamati katika siku za usoni. Lazima kuna mchezaji wa Simba anaweza kufanya vile na wao wakashindwa kufanya chochote kwa sababu watakumbuka kwamba Diarra hakufanywa chochote.

Lakini, utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kwamba huenda Diarra akacheza pambano lijalo kama ambavyo Suleiman Mwalimu alicheza pambano lililofuata dhidi ya Yanga licha ya kwamba alifanya kosa mechi moja kabla ya pambano hilo. Kwamba alipomaliza mechi ya Yanga tu ndio akafungiwa. Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kwamba Kamati ya Saa 72 italazimika kusubiri pambano lijalo la Yanga ndipo itoe adhabu kwa Diarra. Sababu ni moja tu. Wakimfungia Diarra kabla ya pambano lijalo watu wa Yanga watauliza “Mbona Mwalimu alicheza mechi iliyofuata kisha ndio akafungiwa, ina maana mlipendelea ili acheze mechi dhidi yetu sio?” Kutokana na hali hii kamati itajichelewesha kidogo katika kumfungia Diarra ili kuleta usawa wa tukio lilelile la Mwalimu ilimradi kusionekane kuna upendeleo maalumu kwa timu fulani. Wazungu huwa wanaita double standard. Inachekesha sana.

Nchi hii ina maajabu yake. Kuna wakati uamuzi huwa unatolewa kwa ajili ya kumridhisha mtani. Kuna wakati uamuzi unatolewa kwa ajili ya kuwaridhisha wakubwa wa Kariakoo. Ndio hali halisi ambayo tumeishi nayo kwa miaka mingi. Kama unabisha subiri uone.

Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kwamba mwamuzi mkuu wa mechi anaweza kufungiwa kwa kosa la kuruhusu bao la Mtibwa Sugar lisimame. Kwamba kama unamfungia Diarra lazima umfungie mwamuzi kwa sababu ndiye aliyesababisha Diarra amzongezonge kiasi kile. Mtu mwingine ambaye hawezi kusalimika ni mwamuzi msaidizi ambaye alinyoosha kibendera kipindi cha pili wakati Pacome Zouzoua alipovunja mtego wa kuotea na kwenda kumpasi Emmanuel Mwanengo aliyefunga ingawa tayari kibendera kilikuwa juu.

Kuna boksi huwa linaitwa pandora. Sikutaka tulifungue lakini tulilifungua kijinga kwa sababu ya mambo hayahaya ya kubalansi mambo. Tangu siku ile ambayo mwamuzi msaidizi alifungiwa kwa kosa la kunyoosha kibendera chake akimzuia Prince Dube asifunge dhidi ya Simba kule Unguja. Kuanzia hapo nilihoji kama kweli tulikuwa makini katika hilo.

Unaweza kumuadhibu mwamuzi ambaye alikataa bao ambalo lilikuwa halali, lakini haya ya mwamuzi wa pembeni kuadhibiwa kwa sababu ya kunyoosha kibendera cha kuotea kwa mchezaji ambaye hajaotea basi tutaadhibu waamuzi wengi. Na sasa kanuni ileile itatumika. Kwanza kabisa ni kuwapoza Yanga baada ya kumfungia Diarra, lakini pia watu watahoji tofauti ya mazingira ya tukio la Dube na Pacome. Mwamuzi msaidizi naye ataenda na maji.

Lakini nasubiri kuona pia kama kanuni hiyo itakwenda kwa mechi nyingine za kina Mbeya City dhidi ya Coastal Union. Nataka kuona mwamuzi msaidizi akiadhibiwa kwa kosa la kumnyima nafasi halali ya kufunga mshambuliaji wa Dodoma Jiji katika pambano dhidi ya Namungo. Isije kuwa hizi ni sheria za wakubwa tu.

Mwisho wa siku nina mambo mawili hapa. Kwanza kabisa kuondoa utata huu kwa wenzetu wamelewa VAR. Mwamuzi ana nafasi ya pili ya kupima uamuzi wake kupitia video ndogo iliyowekwa uwanjani. Sisi hatuna nafasi hiyo kwa mwamuzi. Kama nilivyowahi kusema hapa. Tutamaliza waamuzi wetu. Kila mkeka wa Kamati ya Saa 72 ukitoka unaweza kukuta kuna mwamuzi mmoja au wawili wamefungiwa. Karibu kila raundi mwamuzi atafungiwa. Hakuwa na nafasi ya kurekebisha makosa yake. Hata hivyo, licha ya kukosekana kwa VAR bado nashindwa pia kuwatetea waamuzi. Kuna wengi tu ambao wanajua nini walipaswa kufanya, lakini wakaamua kukwepa kutimiza wajibu kwa makusudi.

Mpaka leo hatujapata majibu ya lile swali letu maarufu. Waamuzi wetu wanafanya makusudi? Wanahongwa? Wanakosea kibinadamu? Au hawajui sheria? Siku tukipata majibu ya haya tunaweza kupata pa kuanzia. Kwa mfano, kule katika Ligi Kuu England kabla ya mambo ya VAR mwamuzi alikuwa akipuyanga aliondolewa katika raundi ijayo ya ligi. Hakuna adhabu ya miezi mitatu au sita kama huku.

Nadhani wanaamini kwamba mwamuzi hakuwa makini kwa bahati mbaya tu na sio kwamba amehongwa au ana mapenzi na timu fulani. Nashindwa kuwatetea waamuzi wetu kwamba na wao wawe wanaondolewa kuchezesha kwa wiki ijayo tu. Hii ni kwa sababu hawaamini kabisa. Tukifungua mlango wa adhabu nyepesi waamuzi wetu watazidisha madudu. Sasa hivi adhabu ni kali, lakini wanaendelea kufanya madudu kama kawaida. Hawana hofu. Labda wengine wanakuwa na vitita vya kupumzika kwa miezi mitatu ndio maana hawana hofu ya kuvurunda mechi.