Ligi Kuu ya Wanawake Bara kuanza Oktoba
Muktasari:
- Kwa mujibu wa kalenda iliyopangwa Shirikisho la Soka nchini, ligi hiyo itaanza kabla ya kalenda ya FIFA na inatarajiwa kucheza takribani mizunguko mitatu kabla ya kusimama kwa ajili ya kupisha mechi za kimataifa.
LIGI Kuu ya Wanawake Bara (WPL) inatarajiwa kuanza rasmi Oktoba 14, 2026, huku timu 12 zikitarajiwa kuchuana ili kumpata bingwa wa msimu wa 2026/27.
Kwa mujibu wa kalenda iliyopangwa Shirikisho la Soka nchini, ligi hiyo itaanza kabla ya kalenda ya FIFA na inatarajiwa kucheza takribani mizunguko mitatu kabla ya kusimama kwa ajili ya kupisha mechi za kimataifa.
Kabla ya ligi, Ngao ya Jamii inatarajiwa kuchezwa baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake U-20 nchini Poland, ambalo fainali yake imepangwa kufanyika Septemba 27, 2026.
Ngao hiyo itawakutanisha mabingwa Simba dhidi ya watani zao Yanga Princess iliyomaliza nafasi ya tatu huku JKT Queens iliyomaliza nafasi ya pili ikivaana na Mashujaa Queens
Simba Queens na JKT Queens, ndizo klabu pekee zilizowahi kutwaa taji hilo tangu lilipoanzishwa mwaka 2024. Simba Queens ndiyo iliyoandika historia kwa kuwa bingwa wa kwanza wa Ngao hiyo, kabla ya JKT Queens kuchukua mwaka 2025.
Msimu huu, Simba Queens, Yanga Princess, JKT Queens na Mashujaa Queens zitakuwa miongoni mwa timu zitakazoangaliwa zaidi kutokana na ushindani wake wa muda mrefu na uwekezaji unaoendelea kufanyika katika soka la wanawake nchini.
Timu nyingine zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2026/27 ni Alliance Girls ya Mwanza, Bunda Queens na Bunda Girls za Mara, Ceasiaa Queens ya Iringa, Geita Queens ya Geita, Fountain Gate Princess ya Babati, Kilimanjaro Wonders ya Kilimanjaro na Tausi FC ya Dar es Salaam.