Dabi kupigwa Septemba 30, rekodi ikiibeba Simba
Muktasari:
- Mechi ya kwanza itashuhudia Dabi ya Kariakoo baina ya Simba Queens na Yanga Princess huku mechi nyingine ya nusu fainali itawakutanisha mabingwa wa zamani JKT Queens iliyomaliza nafasi ya pili na Mashujaa iliyomaliza nafasi ya nne.
BAADA ya kusubiri kwa muda mrefu hatimaye Ligi Kuu ya Wanawake inarejea ikianza kupigwa mechi mbili za Ngao ya jamii itakayozikutanisha timu nne zilizomaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi.
Mechi ya kwanza itashuhudia Dabi ya Kariakoo baina ya Simba Queens na Yanga Princess huku mechi nyingine ya nusu fainali itawakutanisha mabingwa wa zamani JKT Queens iliyomaliza nafasi ya pili na Mashujaa iliyomaliza nafasi ya nne.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, timu nne zitashuka dimbani Septemba 30, 2026 kupigania tiketi ya kutinga fainali itakayopigwa Oktoba 3, 2026.
UBABE WA SIMBA
Pambano hilo la nusu fainali kati ya Simba Queens na Yanga Princess linatarajiwa kuvuta hisia, huku takwimu na rekodi zikiwabeba zaidi 'Wekundu wa Msimbazi' pindi wanapokutana na watani zao.
Tangu mwaka 2019, timu hizo mbili zimekutana mara 19 katika mashindano mbalimbali. Katika michezo hiyo, Simba Queens imeondoka na ushindi mara 13, huku Yanga Princess ikishinda mara tatu na mechi tatu zikimalizika kwa sare.
Katika michezo ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), timu hizo zimekutana mara 15 ambapo Simba Queens imetawala kwa kushinda mara 11, ikipoteza mara mbili na kutoka sare mara mbili.
Msimu uliopita pekee, Simba iliondoka na pointi zote sita dhidi ya Yanga Princess baada ya kuichapa nyumbani na ugenini kwa jumla ya mabao 4-1.
Mbali na ubabe huo, Simba Queens pia inashikilia rekodi ya ushindi mkubwa zaidi kwenye dabi hiyo baada ya kuichapa Yanga Princess mabao 5-1 mwaka 2020.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Jentrix Shikangwa ambaye kwa sasa anakipiga FC Masar, ndiye anayeongoza kwa kuitesa Yanga Princess baada ya kuifunga mabao saba tangu alipojiunga na timu hiyo msimu wa 2022/23 sawa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Opah Clement.
Kinara wa muda wote wa mabao katika dabi hiyo ni Mwanahamisi Omary 'Gaucho' aliwahi kuifungia Simba mabao 10 dhidi ya Yanga Princess.
Hata hivyo, Yanga Princess imekuwa ikionyesha mabadiliko makubwa na kikosi chake kikiwa na lengo la kuvunja utawala wa Simba Queens, jambo linalofanya pambano hilo la Septemba 30 kuwa la tofauti.